MATUMAINI YAREJEA KESI YA MBUNGE LEMA,MAHAKAMA YAIVAA SERIKALI,SOMA HAPO KUJUA
Mwenyekiti wa kikao cha jopo la Majaji watatu wa
Mahakama ya Rufaa, kinachoendelea Arusha, Bernard Luanda, leo amegeuka mbogo
kwa wanasheria wa serikali kwa kitendo cha kumnyima Mbunge wa Arusha Mjini
Godbless Lema dhamana kwa lengo la kumnyima haki.
Akizungumza Mahakamani hapo leo mbele ya majaji
wenzake Stella Mugasha na Jaji Kipenka Mussa, Luanda amesema haipendezi na
haingii akilini mtu (Lema) kushikiliwa kwa miezi minne bila sababu kwa misingi
ya kumnyima haki.
“Tunaomba ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
serikai (DPP) muwe makini sana maana mnatufanya wanasheria wote hatuna akili na
mnachafua Mahakama, kwa hali ya kawaida mtu mumshikilie kwa misingi ya
kisheria, lakini katika kesi hii tumepitia jalada hatujaona kitu chochote cha
kumshikilia Lema hadi leo na imetushitua sana,”
alisema huku akishauriana na wenzake mara kwa mara kwa masikitiko.
Aliendelea kusema kuwa ofisi ya DPP inaitia najisi
taaluma hiyo, kitu kipo wazi ila wanafanya vitu vya ajabu na havipendezi.
Alihoji jaji Luanda kuwa “Tumesoma faili lote
tunashangaa hivi kweli ofisi ya mwanasheria mkuu ina wanasheria kweli na kama
wapo kwa nini huyu mtu (Lema) awe ndani mpaka leo?”.
Alisema kwa kuwa mikono yao kisheria imefungwa
hawawezi kufanya chochote kwa leo na kuwataka Mawakili upande wa Lema kurudi
Mahakama Kuu, kuendelea na maamuzi ya dhamana.
Hali hiyo ilitokana na Wakili wa serikali Faraja
Nchimbi kusimama mahakamani hapo na kuomba kuiondoa rufaa hiyo kwa madai kuwa
ipo nje ya uwezo wake.
“Waheshimiwa Majaji baada ya timu yetu
ya wanasheria kupitia kwa kina rufaa hii kwa sababu zisizozuilika tumeona
hatupo tayari kuendelea na rufaa hii, maana hatukupeleka kusudio (Notisi) kwa
msajili muda ulipita, hivyo tunaomba kuiondoa na uamuzi wa kuiondoa rufaa hii
tumeufikia Ijumaa muda uliisha kuja mahakamani,”.
Alisema Nchimbi.
Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Lema Peter
Kibatala, alisimama na kusema upande wao hawana pingamizi ila waliomba hoja za
awali za rufaa hiyo ziondolewe Mahakamani hapo bila kunakiliwa.
Baada ya ombi hilo Jaji Kipenka Mussa alipokea kwa
niaba ya Majaji wenzake na kukubali ombi la kuiondoa rufaa hiyo namba 9/2017.
Aidha Jaji Luanda alimkaribisha jaji Stella Mugasha
pia kuongea kwa niaba yao ambapo alisema mahakama imekubali ombi la pili la
kuiondoa rufaa namba 10/2017, baada ya Wakili Paul Kadushi kuomba kuiondoa pia.
Wakili wa Lema Peter Kibatala, alilazimika kusimama
tena Mahakamani hapo kusema kuwa upande wao unasikitika kuona ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP wanatumia Mahakama kwa njia ya kumnyima
haki mteja wao, hivyo aliomba mahakama hiyo iwatatulie tatizo la kisheria
lililojitokeza hadi mteja wao awe ndani hadi sasa.
Kibatala aliongea hayo huku akishindwa kujizuia na
kumwaga chozi la huzuni mahakamani hapo mbele ya Majaji hao.