KASSIM MAJALIWA ACHIWA JUKUMU LA KUPAMBANA NA MADAWA YA KULEVYA,SOMA HAPO KUJUA

Jacquiline Mrisho na Eliphace Marwa – MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli amemkabidhi Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kazi ya kuzuia na
kupambana na dawa za kulevya akiwa kama Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Dawa
hizo nchini.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es
Salaam wakati akiwaapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Peter
Makakala, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Rogers William Sianga pamoja na mabalozi watatu Mhe. Omary Yusuph Mzee,
Mhe.Joseph Edward Sokoine pamoja na Mhe. Grace Aron Mgovano aliowateua hivi
karibuni.
Dkt. Magufuli amesema kuwa Waziri Mkuu anatajwa
kwenye Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ambapo Wajumbe
wake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Waziri wa Elimu ana Mafunzo ya Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha na
Mipango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Nalipongeza sana Bunge la kipindi cha mwaka 2010 – 2015
chini ya Spika mstaafu, Mhe. Anne Makinda lililopitisha Sheria hii baada ya
kuona sheria za mwanzo za kupambana na dawa za kulevya hazina nguvu hivyo
Wabunge wa wakati ule walisimama kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao
wakapitisha sheria hii,” alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Dkt.
Jakaya Kikwete kwa kusaini sheria hiyo haraka mara baada ya Bunge hilo
kuipitisha kwa sababu alijua madhara ya dawa za kulevya katika nchi yetu.
Amefafanua kuwa sheria imeeleza wazi katika kifungu
cha 10 cha Sheria Na.5 ya mwaka 2015 kuwa jukumu la kupambana na dawa za
kulevya linasimamiwa na Serikali pekee yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamo wa Rais, Waziri
Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri
za Wilaya au mtu yoyote atakayekuwa amepewa mamlaka ya kusimamia Serikali.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa
amesema kuwa Taifa limeendelea kushuhudia kizazi chetu kikiendelea kudidimia
kwa sababu ya matumizi ya dawa za kulevya na Serikali kwa mipango yake
imeendelea kukemea, kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya
wazalishaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa hizo.
“Jambo hili limeleta athari kubwa sana kwani vijana
wetu wengi wamepoteza uwezo wa kujisimamia katika shughuli zao za maendeleo kwa
sababu baada ya matumizi tumeona athari kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa kwa
mwili, uwezo wa kutafakari pamoja na kutoweka kwa uwezo wa kufanya
kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Taifa hili la
Watanzania kwa kiasi kikubwa linawategemea vijana waweze kuleta msukumo wa
maendeleo ndani ya nchi hivyo jambo hili likiachiwa linaweza kuleta athari
kubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo yetu kwa ujumla wake.
Alisisitiza kuwa vita hii ilianza, inaendelea na
itaendelea kupiganwa hadi imalizike hivyo Watanzania hawana budi kuunga mkono
jitihada zozote zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na matumizi yake kwa namna yoyote ile, kila mmoja anatakiwa
kushiriki kikamilifu ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya ndani ya nchi hii.