ZITTO KABWE AKOLEZA MOTO WA OPARESHENI UKUTA,SOMA HAPO KUJUA
Wakati viongozi wa dini wakiendelea na jitihanda za
kusaka suluhu kati ya upande wa Serikali na Chadema kuhusu namna ya kuzuia kwa
amani kufanyika kwa Operesheni ya chama hicho iliyopewa jina la UKUTA, Septemba
1, Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe ametoa maoni yake.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini amesema
kuwa haoni haja ya kufanyika kwa vikao hivyo vya kusaka maridhiano kwani
Chadema wanachotaka kufanya kiko kikatiba.
“Sioni ni kwanini tunahangaika na vikao
vya maridhiano na tahariri nyingi kuhusu shughuli ya CHADEMA kufanya operesheni
yao ya UKUTA. Kuandamana ni Haki ya KIKATIBA. Tuache watu watimize Haki yao Kwa
amani. Kuzuia watu kufanya jambo lao la kikatiba ndio kuvunja amani. Wanaotaka
kuandamana waandamane na wanaotaka kufanya Kazi zao nyingine tuendelee na Kazi
zetu. Kwanini kutekeleza Haki ya kikatiba iwe ni kuvunja amani? Kwanini?,” Zitto
ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Hata hivyo, vikao vya maridhiano vinavyoendelea
tayari vimeonesha kuzaa matunda kwenye suala la mgogoro wa Bunge ambapo wabunge
wa vyama vya upinzani wameridhia kurejea Bungeni katika vikao vitakavyoanza
mapema mwezi ujao.
Serikali imeendelea kuwaonya watu wote wanaopanga
kuandamana Septemba 1 huku viongozi wa Chadema wakisisitiza kuwa siku hiyo
watafanya maandamano kama walivyopanga.
Hali hiyo imepelekea kumtoa hadharani Kingunge
Ngombale Mwiru ambaye ameomba marais wastaafu kumshauri Rais Magufuli ili
kuruhusu Serikali kukaa na Chadema kusaka muafaka wa masuala ya kisiasa nchini.