MBOWE WA CHADEMA AANZA KUSAKAMWA,SERIKALI YAMSHIKILIA BANGO MALI ZAKE,SOMA HAPO KUJUA
Zimebaki wiki tatu kabla Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) kuchukua jengo la Bilicanas lililokodiwa na Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuendesha biashara ya ukumbi
wa starehe.
Jengo hilo lipo eneo la Posta jijini Dar es
Salaam.Awali, NHC ilikuwa imetoa notisi ya siku 60 kwa wadaiwa sugu ambao wamepanga
katika majengo yake akiwamo Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi
Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai
taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla ya Sh. bilioni 15.
Notisi ya siku 60 ya kuondoka Bilicanas pamoja na
majengo ya wadaiwa wengine ilishatolewa, Mchechu alisema na kwamba sasa
zimesalia wiki tatu.
Alisema baada ya muda huo kumalizika, utekelezaji wa
kuondolewa katika majengo hayo utaanza ukiambatana na uchukuaji wa hatua za
kisheria.
Mchechu alisema mbali ya Bilicanas, wadaiwa wengine
ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni mbili, Benki ya
Azania (Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa (Sh. milioni 631).
Wadaiwa wengine walitajwa kuwa ni Wizara ya Afya na
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sh. bilioni mbili), Tume ya Utumishi (Sh.
milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.
Mchechu alisema ukusanyaji wa madeni hayo kwa nguvu
ni mkakati wa shirika hilo kukusanya fedha ili kusaidia ujenzi wa nyumba za
watumishi wanaohamia Dodoma.
Alipoulizwa iwapo mkakati huo una uhusiano wowote na
masuala ya kisiasa kutokana na kumtaja Mbowe kuwa ni kati ya wadaiwa sugu,
Mchechu alisisitiza hakuna uhusiano wa siasa na zoezi hilo kwani wateja wote
wanachukuliwa sawa.
“Mwaka huu ujenzi unaanza Dodoma," alisema
Mchechu, hivyo fedha tunazodai zitatusaidia kukamilisha uwekezaji mjini
humo."
“Ndiyo maana tumetoa kwa tunaowadai notisi ya miezi
miwili, vinginevyo wataondolewa katika majengo ya shirika kama kanuni
zinavyotaka.
“Hakuna uhusiano wowote kati ya shirika kukusanya
fedha linazodai na watu binafsi akiwamo Mbowe, taasisi za umma na binafsi.
“Lengo ni kukusanya madeni ambayo baadhi yake
yalisimama kutokana na mengine kuwa na kesi mahakamani.”
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwa ujenzi wa
nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.
Alisema ujenzi huo unatarajia kuanza mara moja na
utachukua miezi 12.
Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni 60 za ujenzi wa
nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.
Alisema shirika hilo limenunua ekari 240 eneo la
Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi na Chemba ekari nne pia ikiwa ni kuunga
mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia Dodoma.
Alisema fedha nyingine zitapatikana baada ya nyumba
97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.
Aidha, Mchechu alisema kitendo cha Serikali kuhamia
Dodoma kitatoa fursa kwa Jiji la Dar es Salaam kujiimarisha kibiashara tofauti
na ilivyo sasa ambapo linakwamishwa na foleni kubwa za magari kutokana na
shughuli nyingi za serikali kufanyika.
“Dar es Salaam kuna bandari, uwanja wa ndege,"
alisema na kuongeza: “Hivyo suala la kiuchumi litaimarika zaidi kutokana na
shughuli nyingi za Serikali kuhamia Dodoma. Hii itasaidia uchumi wa nchi
kusambaa katika maeneo tofauti nchini.”
Uwekezaji wa NHC jijini Dar es Salaam upo kwa
asilimia 70, alisema na kwamba ufanisi wa Jiji utaongezeka hususani katika
usafiri na sekta nyingine kiuchumi.