WAZIRI MKUU AWATANGAZIA KIAMA WAKUU WA SHULE WASIOKUWA NA SHAHADA,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa
halmashauri na Maofisa Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa
Elimu Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa
shule za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.
“Maofisa Elimu na Wakurugenzi msije
mkawaondoa wale walimu wakuu kwa zile sifa nilizosema bado muda ukifika
tutatangaza.Msije mkawakurupusha sasa hivi waacheni waendelee na kazi zao
tutatoa muda ili wajipange viziri,” aliema.
Agosti 20 mwaka huu Waziri Mkuu alisema
Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari
wanatakiwa kuwa na shahada huku walimu wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na
diploma.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano,
Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini.
Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima
awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa
elimu katika shule za sekondari na msingi.
“Wakuu wa shule za sekondari na waratibu
wa elimu kata wasiokuwa na shahada wasiondolewe katika nafasi zao kabla ya
kupewa nafasi ya kwenda kujiendeleza kwa masomo ili waweze kuwa na vigezo vya
kuendelea kushika nyadhifa hizo,” alisema.
Alisema katika kuboresha maslahi ya walimu Serikali
imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka.
Waratibu Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za
sekondari na walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.
Waziri Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye
nyadhifa hizo ni vema Wakurugenzi wakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili
na wao wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi
karibuni.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka wazazi
na walezi kwenda kuwaandisha watoto wenye umri wa miaka mitano katika shule za
awali ambapo watapata fursa ya kujengewa msingi mzuri wa masomo kabla ya kuanza
darasa la kwanza.
Pia aliagiza shule zote za msingi nchini zisizokuwa
na madarasa ya awali kuhakikisha wanaanzisha madarasa hayo haraka na kuanza
kutoa elimu hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, AGOSTI 25, 2016.