WANAHARAKATI WA HAKI ZA BINADAMU WAMUONYA JPM,NI KUHUSU OPARESHENI UKUTA YA CHADEMA,SOMA HAPO KUJUA
Kituo cha Sheria na Msaada wa Haki za Binadamu
(LHRC) kimemshauri Rais John Pombe Magufuli kufuta kauli zenye utata kwa madai
kuwa zinakiuka haki za binadamu na siasa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo jijini Dar
es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo Bisimba amesema kauli
hizo zinaweza zikaathiri mtu mmoja na jamii kwa ujumla endapo zikiwa kinyume na
sheria pamoja na katiba za nchi, “Kituo kinatambua nguvu ya kauli ya Rais Kuwa
hutoa agizo la kiutekelezaji wa vyombo vyote serikalini na ikiwa kinyume
inaweza ikasababisha madhara makubwa kwa mtu mmoja ama jamii kiujumla, ”Alisema
Bisimba
Bisimba amemsisitiza Rais Magufuli kufuta kauli
zenye utata ikiwemo kauli ya kufuta shughuli za kisiasa mpaka mwaka 2020 kwa
kuwa iko kinyume na Ibara za 3(1) na 20(1) ya katiba na vyama vya siasa,
“Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia haki za siasa zikikandamizwa kwa
matamko ya viongozi mbalimbali wa juu wa serikali akiwemo Rais Magufuli mfano
akiwa ziarani mkoani singida alitoa tamko la kuzuia shughuli zote za kisiasa
hadi mwaka 2020,” amesema na kuongeza.
“Pia Waziri mkuu Kassim Majaliwa akiwa Ruangwa Lindi
alitoa tamko la kuzuiwa mikusanyiko yenye mlengo wa kisiasa ingawa alikanusha
tamko hilo alipokuwa bungeni, wakuu wa mikoa pia walitoa matamko mbalimbali la
polisi kuzuia sehemu nyingine wanasiasa wasikutane”
Amesema kutokana na kauli hizo imeshuhudiwa baadhi
ya viongozi wa vyama vya siasa kutoa matamko na maazimio yenye kuashiria chuki,
uhasama na sintofahamu kwa jamii na kuelekea kuuvunja umoja na amani ya Taifa,
“Msajili wa vyama vya siasa asimame katika nafasi yake ya mratibu, msimamizi na
mbeba bendera ya maendeleo ya vyama vya siasa na ukuaji wa demokrasia na
kutojiingiza katika kuonekana kuegemea upande au chama chochote, ili kusaidia
kujenga mshikamano wa Taifa.