Zinazobamba

WAZIRI NCHEMBA KUWA MGENI RASMI SIKU YA VIJANA.DK MARWA AWATAKA VIJANA KUJITOKEZA,SOMA HAPO KUJUA


Pichani ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba(picha na Maktaba)

 NA KAROLI VINSENT
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika siku ya vijana inayofanyika leo katika viwanja vya Zakhiem Mbagala jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Dar es Salaam na Ofisa Miradi wa Shirika la umoja wa mataifa la idadi ya watu Duniani, Daktari Majaliwa Marwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu siku hiyo iliyopangwa kuwakutanisha vijana zaidi ya 1000 kutoka maeneo mbali mbali.

Amesema Vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo kwa kuwa Shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali wamepanga kutoa elimu kwa vijana ya kuweza kujitambua na kuacha masuala ya kuwa tegemezi.


"Katika siku ya Kesho tumepanga kufanya mambo mbali mbali ikiwemo yale ya ujasiriamali pamoja na kujenga uelewa wa masuala ya afya kwa vijana ili tuweze kujenga taifa ambalo litakuwa na watu wenye afya bora pamoja na wenye kipato," amesema Dkt.Marwa.

Dkt. Marwa ameongeza kuwa Vijana wanapaswa kufuata kauli mbiu ya Mwaka huu isemayo 'Kijana, Sepesha Umaskini Ongeza uzalishaji kwa maendeleo endelevu' ili kuweza kufanya maliasili zilizopo katika nchi hii ziweze kusaidia vizazi vya mbeleni.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi wa Shirika la PSI Tanzania,Pludence Masaku amesema kuwa kwa hivi sasa nchini kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana kupata ujauzito kabla ya kujiandaa hivyo vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuweza kupata elimu itakayowawezesha kuweka mpangilio wa Familia zao.

Alisema kuwa Shirika hilo litatoa huduma za afya katika maadhimisho hayo pamoja na kutoa semina kwa vijana itakayoweza kuwasaidia katika kuendesha maisha yao pamoja na kusaidia kukuza ustawi wa jamii.

"Ili taifa liweze kupata maendeleo ni lazima watu wajiandae kila idara ikiwemo ile ya afya, hivyo siku ya kesho sisi tutaitumia kwaajili ya kutoa semina na elimu mbali mbali kwa vijana ili waweze kupanga wakati ambao wanataka kupata watoto na sio kuzaa holela holela na kupeleka kushindwa kuwalea watoto wao," alisema Masaku.

...Mwisho...