UKUTA YA CHADEMA YAMUIBUA MZEE KINGUNGE,AIBUKA NA KUWAANGUKIA VIONGOZI WASTAAFU,ASEMA AMANI YA TANZANIA INAKWENDA SHIMONI,SOMA HAPO KUJUA

NCHI inatikiswa. Amani ya nchi inaelekea
kutoweka.Viongozi wastaafu wako wapi? Mbona kimya?anaandika Charles William.
Ni yowe la Kingunge Ngombale-Mwiru, mwanasiasa mkongwe nchini
alilolitoa leo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari
kuhusu mvutano kati ya Chadema na serikali unaoendelea kwa sasa.
Chadema
kimeingia kwenye mvutano mkubwa na serikali kutokana na dhamira yake ya kufanya
mikutano na maandamano nchi nzima chini ya mwavuli wa Umoja wa Kupinga Udikteta
(Ukuta).
Hivi karibuni,
Rais John Magufuli alisisitiza kutoruhusu maandamano na mikutano ya kisiasa na
kuagiza kuwa, wanaotaka kufanya mikutano wafanye ndani ya mipaka ya majimbo yao
na si vinginevyo jambo ambalo Chadema wanapinga.
Hali hiyo
imeibua mtikisiko mkubwa nchini huku kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na
viongozi wa dini, wanasiasa, wasomi na wananchi wa kawaida wakitaka kupatikana suluhu
kabla ya Septemba Mosi, tarehe iliyopangwa kuanza maandamano na mikutano hiyo.
Kwenye mkutano
wake na wanahabari Kingunge anawalaumu viongozi wastaafu wakiwemo marais pamoja
na mawaziri wakuu kwa kukaa kimwa wakati huu ambao nchi inatikishwa huku Katiba
ya Jamhuri ikisiginwa.
Miongoni mwa
viongozi wanaolalamikiwa kutosikika ama kuchukua hatua zozote ili kuilinda
Katiba ni pamoja na Marais Wastaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na
Aman Abeid Karume (Zanzibar).
Viongozi wengine
waliotajwa ni Mawaziri Wakuu Wastaafu, Cleopa Msuya; Jaji Mstaafu, Joseph
Warioba.
“Mzee Mwinyi
yupo kimya, Mkapa kimya, Warioba kimya, Cleopa Msuya kimya, Amani Karume
kimya,” amesema Kingunge na kuongeza;
“Ukimya huu
unatokana na nini? Hawa wote waliwahi kula viapo vya utii kwa Katiba. Mimi
nahoji, wazee wenzangu vipi mnakuwa kimya? Nawaambia kuwa mnachofanya si sawa.
“Naomba wazee
wote tujitokeze kuhesabiwa katika hili la uvunjifu wa Katiba na sheria.”
Kingunge ambaye
alihamia Chadema akitokea CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kutokana na
kutoridhishwa na namna mchakato wa kumpata mgombea urais kutoka chama hicho
amesema, Chadema inatumia haki yake ya kikatiba.
“Naomba Rais
Magufuli, akubali kuitisha kikao na Chadema ambacho pia wazee wastaafu
watahudhuria, akifanya hivyo hata sisi wazee tutawageukia Chadema na kuwambia
wasitishe mpango wao wa maandamano,” amesema.
Amesema kwamba,
kibaya zaidi Jeshi la Polisi linaandaa bunduki kwa ajili ya kupambana na raia
ambao hawana kitu na kuwa, hali hiyo haipaswi kuvumiliwa.
Mwanasiasa huo
amesema, Chadema wameamua kutetea haki yao ya kikatiba na kisheria kwa kufanyaa
maandamano kote nchini, na kina wafuasi wengi hivyo si jambo la kubeza.
“Upande wa pili,
lipo Jeshi la Polisi na watawala ambao wanaahidi kuwakabili. Kwa bahati mbaya
polisi na watawala hawatetei Katiba wala Sheria,” amesema.
Amesema kuwa,
Tanzania kwa sasa inakabiliwa na ombwe la uongozi na kwamba, nchi imekosa
watawala wenye sifa thabiti ya kuongoza taifa.
“Kwa hakika,
tatizo kubwa la sasa la nchi yetu ni ombwe la kiuongozi, kwasababu kama ni
watawala tunao kweli kweli, lakini tunachokosa ni watawala wenye maarifa ya
kiuongozi.
“Inashangaza
kuona wazee wastaafu kukaa kimya wakati nchi inakabiliwa na tatizo linaloweza
kutuangamiza.
“Upande mmoja
unanoa mapanga, unaanda bunduki kwa ajili ya kuchinja na kuua na upande wa pili
wapo raia tu, tena wasio na silaha zozote.”
Kingunge
anasema, wananchi ambao serikali na Jeshi la Polisi wanajiandaa kupambana nao,
wanalilia Katiba na sheria zifuatwe.
“Laiti kama
Chadema wangekuwa hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila sababu ya
kuwashughulikia, lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria, kuna umuhimu wa
kuyapa uzito madai yao,” amesema Kingunge.
Mwanasiasa huyo
amesema kuwa, mvutano wa sasa sio wa Chadema na serikali isipokuwa ni suala la
wananchi wote wa wenye mapenzi mema na taifa lao.
“Hili ni suala
la kila mtu anayependa utawala wa Katiba, Sheria na Utawala Bora,” amesema.
Mara kadhaa Rais
Magufuli amekuwa akinukuliwa akitoa kauli za vitisha kwa upinzani pia kuhofisha
wananchi.
Hivi karibuni
akiwa Sengerema, Mwanza Rais Magufuli alisema, “Jamani wana Sengerema nyie
wenyewe mnafahamu matukio ya watu kupoteza maisha nchini Rwanda.
“… watu walikufa
sana, sasa na nyie mnataka na sisi tuingie katika hali hiyo?” aliuliza Rais
Magufuli kwenye mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Mnadani, Kata ya
Nyampulukano.
Alisema kuwa,
katika utawala wake hatakubali kuona chokochoko kutoka vyama vya siasa ambavyo
hakutaja majina huku akidai, kama wanataka kufanya hivyo wasubiri hadi
ang’atuke.
“Wao wasubiri
siku nikitoka ndio waje wavuruge amani ya nchi, lakini kama mimi nipo hakuna
atakayekuja kuvuruga amani na kama wanataka kufanya hivyo, wasubiri mpaka siku
niondoka,” amesema.