TUNDU LISSU AMESHINDAKA KABISA,AENDELEA KUIBWAGA SERIKALI MAHAKAMANI,SOMA HAPO KUJUA
Serikali imeendelea kupigwa mweleka katika kesi ya
uchochezi dhidi ya mshitakiwa Tundu Lissu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kutupa pingamizi la Wakili wa Serikali wakitaka wakili Peter Kibatala
kujitoa kumtetea mwanasiasa huyo.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa
tiketi ya Chadema alipandishwa kizimbani Agosti 5, na kusomewa mashtaka matatu,
mawili kati yake yakiwa ni ya uchochezi na moja la kuidharau mahakama.
Pigo la kwanza la upande wa mashtaka ni pale Lissu
alipopangua hoja na kufanikiwa kupata dhamana, wakati kesi hiyo ilipofikishwa
mahakamani kwa mara ya kwanza.
Jana ilikuwa ushindi mwingine kwa upande wa utetezi,
baada ya Mahakama kutupa pingamizi la upande wa mashtaka lililotaka Kibatala
ajitoe katika jopo la mawakili wanaomtetea Lissu.
Upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali
Mkuu, Faraja Nchimbi, uliweka pingamizi hilo kwa maelezo Kibatala ni shahidi
wao kwa kuwa alikuwapo siku na mahali wakati Lissu akitoa maneno yanayodaiwa ya
uchochezi.
Wakili Kibatala ambaye ni kiongozi wa jopo la
mawakili wanaomtetea Lissu, alipinga hoja za Serikali za kutaka ajitoe katika
kesi hiyo, mvutano ambao ulisababisha kesi hiyo kuahirishwa mara mbili.
Wakili Kibatala alipinga kuwa hakuna kifungu cha sheria
kinachomzuia wakili kumtetea mteja wake kwa sababu tu ya kushuhudia akitoa
maelezo yake Polisi.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali, Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, hakukubaliana na hoja za
upande wa Jamhuri (mashtaka) na hivyo akalitupa pingamizi hilo.
Hakimu Mkeha alikubaliana na hoja za wakili Kibatala
kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachomzuia kumtetea Lissu.
Alisisitiza kuwa Kibatala ataendelea kuwa wakili wa
Lissu katika kesi hiyo na kwamba kama upande wa mashtaka ukimhitaji awe shahidi
wao utalazimika kumuomba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 19