MAHAKAMA YAMWINDA DK MENGI,SASA AEKEWA MTEGO,SOMA HAPO KUJUA

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara imeamuru
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi afike mahakamani
kujieleza kwa nini asifungwe gerezani kwa kushindwa kutekeleza hukumu inayohusu
malipo ya Sh bilioni 1.2.
Mengi anatakiwa kufika mahakamani hapo Agosti 24,
mwaka huu kujieleza kutokana na kushindwa kutekeleza hukumu iliyomtaka kuwalipa
wafanyabiashara watatu, Muganyizi Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles
Mgweo, Sh bilioni 1.2.
Alitakiwa kuwalipa fedha hizo kutokana na mgogoro wa
malipo ya uuzwaji wa hisa katika Kampuni ya Douglas Lake Minerals Ltd ambayo
kwa sasa inaitwa Handeni Gold Inc.
Kwa mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani,
Mengi anatakiwa kufika mahakamani hapo Agosti 24, mwaka huu ili ajieleze kwa
nini asifungwe gerezani kama mfungwa wa madai kama sehemu ya kukazia hukumu
hiyo.
Mahakama imetoa hati hiyo kutokana na
wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi katika hatua ya kukazia hukumu
iliyotolewa Januari 28, mwaka huu na Jaji Agathon Nchimbi wa mahakama hiyo.
Katika hati ya kiapo ya wafanyabiashara hao,
inadaiwa walifungua kesi dhidi ya Mengi na Kampuni ya K.M. Prospecting Limited,
wakidai malipo yaliyokuwa yamebakia ya dola 428,750, 100,000 na 70,000, kwa
kila mmoja.