Zinazobamba

SERIKALI ITENGE BAJETI MAALUM KWA AJIRI YA CEmONC-UTEPE MWEUPE

Mratibu wa Taifa wa muungano wa utepe mweupe wa uzazi salama (White Ribon Alliance) Bi. Rose Mlay  akifafanua jambo kwa Waandishi wa habari waliohudhuria semina ya siku moja kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari kupaza sauti juu ya Tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi. Bi. Mlay anasema hilo ni janga ambalo halisemwi na kumuomba Mh. Rais Magufuli kulitupia macho.

Meneja mipango wa muungano wa utepe Mweupe wa uzazi salama Sizarina Hamisi akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari


Imetosha! Ndivyo unavyoweza kusema ukisikiliza kwa makini Takwimu za vifo vinavyotokana na uzazi. Kila siku Nchini Tanzania kuna wanawake 24 wanapoteza maisha, Zaidi ya watoto 144 hufariki lakini pia kama hiyo haitoshi Takwimu zinaonyesha kila mwanamke mmoja anapofariki huacha wenzake 30 wakipata ulemavu wa kudumu kama vile fistula au miguu kupooza.

Takwimu zinaendelea kuonyesha kwa mwaka Tanzania inapoteza wanawake 8,000, watoto 48,000 na kunatengeneza walemavu wa kudumu wapatao 240,000.

Ukipiga jumla yake hapo utagundua kwa kila mwaka Tanzania inapoteza nguvu kazi wapatao 296,000, nilikuwa najaribu kujiuliza hapa, ni kwa nini hasa?.

Hivi hatujachoka kupoteza nguvu kazi hii, wahusika wanaliona hili? Na Nini kifanyike. Kwa kweli  neno kwa nini hasa limekuwa lefu. Ni mnyororo unaoanzia mbali kushuka hadi ngazi ya kata.

Mapema hii leo Fullhabari. Blog ilipata bahati ya kuzungumza na Mratibu wa Kitaifa wa White Ribon Alliance Bi.Rose Mlay kuhusu suala la vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, nikataka hasa kufahamu njia zinazoweza kuondokana tatizo hilo linalotia aibu Taifa letu.

Akizungumzia Suala hilo,Bi.  Mlay  amesema kabla ya kuangalia suluhisho la tatizo hilo, Jamii pamoja na Serikali yetu inapaswa kukubali kwa vitendo kuwa vifo vya uzazi havikubaliki, kuanzia hapo tuanze kuzichambua sababu za vifo hivyo na kwa nini hasa zipo.

Ameongeza kusema Taifa likiamua kulifanya suala hilo kuwa ajenda, hakuna kitakachoshindikana kwani ni suala ambalo linahitaji msukumo wa kisiasa kuliondoa.

Amesema, ukiangalia ukubwa wa tatizo ni dhahili kuna haja viongozi kukaa chini kuangalia ni kwa jinsi gani wanaweza kuleta msukumo wa kisiasa kama ilivyoweza kufanya katika sekta zingine za Elimu ambako kumeonekana mafanikio makubwa ya madawati.

Amesema ieleweke kuwa watoto wote wanapaswa kulindwa tokea wakiwa tumboni, na kwamba kama Taifa likiamua kufanya kampeni ya kutokomeza vifo vinavyotokana na uzazi inawezekana.

“Tuone aibu kwa taifa kama la Tanzania kuwa nchi ya pili kwa idadi ya watu wanaokufa kutokana na  uzazi katika ukanda wa Afrika Mashariki” Nchi zingine kitendo cha kufa mama anayejifungua ni suala la aibu na wahusika lazima wachukuliwe hatua. Alisema Mlay.


Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mada.

Aidha Mlay amesema Mbali na Msukumo wa Kisiasa, lakini jambo kubwa ni kuongeza na kuilinda bajeti ya huduma kamili za dharura za uzazi salama (CEmONC) 

Akifafanua kuhusu CEmONC, Mlay amesema huo ndio muarobaini wa vifo vinavyotokana na uzazi, kwa sababu vifo vingi vinahitaji huduma za dharura ambazo bajeti yake inatakiwa kuandaliwa mapema.

Amesema asilimia 70 ya vifo vya akina mama na watoto wachanga wakati wa kujifungua vinasababishwa na sababu kuu tano; ambazo ni Kuvuja damu,Kifafa cha mimba, Maambukizi baada ya kujifungua,kutoka kwa mimba pamoja na uchungu pingamizi. Hivyo kunahaja ya kuandaa bajeti maalum kukidhi mahitaji hayo.

Mlay anasema kwa muda mrefu bajeti inayotengwa kwa wizara ya afya imekuwa na mambo mengi ya kufanya, ili kukabiliana na vifo hivyo hakuna budi Serikali kupitia Wizara ya fedha na mipango kupanga bajeti maalum kwa ajili ya CEmoNC.