DC HAPI WA KINONDONI ACHACHAMAA,ATUMBUA JIBU HILI LEO,SOMA HAPO KUJUA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mh Ally Hapi leo
ametengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya
Mwananyamala Dkt. Delila Mushi kwa kosa la kupandisha bei ya baadhi ya huduma
kinyume cha taratibu na sheria.
Mushi amedaiwa kupandisha bei ya huduma hizo baada
ya kukaa kikao cha hospitali pasipo kuipeleka hoja ya kupandisha bei katika
kikao cha Idara ya Manispaa na huduma za jamii.
Taratibu alizotakiwa kufuata Mushi ni kuipeleka hoja
hiyo Manispaa, ambapo ingejadiliwa kwenye kikao cha huduma za jamii kisha
baraza la madiwani kuipitia na kuitolea maamuzi jambo ambalo hakulifanya badala
yake alipandisha bei pasipo kupitia taratibu hizo.
Bei ya huduma zilizopandishwa ni pamoja na bei ya
kadi ambapo wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo bila ya barua ya
rufaa kutoka vituo vya afya na zahanati zilizo karibu nao, walitakiwa kulipa sh
10,000 badala ya 6,000.
“Hakuna jambo baya kama kiongozi kufanya
maamuzi pasipo kufuata utaratibu halafu maamuzi hayo yakaathiri wananchi
wanyonge, mkurugenzi nakuagiza hiyo bei ya kadi irudi kama ilivyokuwa awali,
huwezi mlipisha mgonjwa kiasi kikubwa cha fedha huku huduma unazotoa haziendani
na bei hiyo, ” amesema Hapi.
“Hakuna sababu ya anayekaimu nafasi ya
mganga mkuu kwa sasa kubaki na wadhifa huo wakati haumtoshi, atatafutwa
mwIngine kuja kuwa mganga Mkuu, ” amesema.
Kwa sasa ameteuliwa Dkt. Daniel Nkungu kukaimu kwa
muda wadhifa huo hadi atakapoteuliwa mganga mwingine kushika wadhifa huo.
Hata hivyo, Baada ya Hapi kutoa agizo la kutenguliwa
uteuzi wa Dkt. Mushi na kuamuru Wagonjwa kulipa bei ya kadi ya awali, baadhi ya
wahudumu wa mapokezi waligoma kutoa huduma kwa madai kuwa mifumo ya utoaji
risiti imeharibika.
Mariam Hamisi Sahabani mkazi wa Kinondoni,
alifafanua jinsi wahudumu hao walivyogoma baada ya mkuu wa wilaya kuondoka.
“Baada ya Mheshimiwa kuondoka wamegoma
kutoa huduma kwa kigezo kuwa mashine ilikuwa mbovu, inawezekanaje? Mbona wakati
tunalipa 10,000 mashine zilifanya kazi, iweje sasa zisifanye? ” alihoji.
Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na wananchi
waliokuwepo kwenye hospitali hiyo, Mganga mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt.
Aziz Msuya alisema atawasimamisha kazi waliogoma kutoa huduma kwa kuwa walikuwa
na lengo la kupinga kauli ya serikali.
“Naagiza huduma ianze kutolewa kuanzia
sasa, na watakaogoma kutoa huduma nitawasimamisha kazi kuanzia kesho, ” amesema
Msuya.