BAVICHA YAIJIBU POLISI,NI KUHUSU OPARESHENI UKUTA,SASA MAPAMBANO YAFIKIA PATAMU,SOMA HAPO KUJU
![]() |
|
Picha kubwa ni Jeshi la polisi
wakipambana na wafuasi wa Chadema, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
– Zanzibar (Picha ndogo ya kwanza)
|
BARAZA la Vijana Taifa la Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Bavicha), limesema Jeshi la Polisi linawajibu wa kikatiba wa kulinda
operesheni yao ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta),anaandika Faki Sosi.
Pastrobas Katambi, Mwenyekiti
wa Bavicha, akizungumza na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya chama hicho
jijini Dar es Salaam, amesema vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa katiba na
kwamba vinahaki ya kupatiwa ulinzi vinapofanya mikutano ya hadhara na maandamano.
Katambi amesema jeshi hilo litakuwa linatimiza
jukumu lake la kikatiba likishirikiana na Chadema kufanikisha maandamano
yaliyopangwa kufanyika nchi nzima Septemba mosi.
Amesema ni upotoshaji mkubwa wa hali halisi pale
jeshi la polisi linaposhiriki kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayolenga
kuyadhibiti maandamano hayo.
Amesema wapo viongozi wa CCM wenye nia mbaya ambao
wanaeneza kampeni kwamba maandamano hayo ni ya uchochezi.
“Sio kweli kuwa Ukuta ni uchochezi na wanaosema
hivyo wanalenga kupitisha ajenda yao ya kukichafua chama pamoja na kupandikiza
chuki kwa wananchi dhidi ya Chadema,” amesema.
Katambi amesema wakuu wa wilaya na mikoa na wenyewe
wanajukumu la kusimamia sheria na katiba ya nchi badala ya kuchukua mkondo wa
kutaka kukandamiza demokrasia.
Amesema ni udhaifu tu wa mamlaka ya uteuzi wa
viongozi serikalini kuteua makada wa CCM kuwa ndio wanaoshika nyadhifa hizo
ambazo huwafanya moja kwa moja kuwa wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama
kwenye maeneo yao. Hiyo huwasukuma kutumikia wananchi kwa utashi wa kisiasa
kuliko kuzingatia sheria.
Katambi amesema Bavicha limejipanga kuwalinda
viongozi wa chama ili wasije kukamatwa kama inavyosemekana polisi kuazimia
kufanya hivyo kabla ya siku ya maandamano.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) umetangaza kuandaa maandamano nchi nzima tarehe 31 mwezi huu.
Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa umoja huo amewaambia
waandishi wa habari leo kwamba maandamano hayo ni ya kumpongeza Rais John
Magufuli kwa alichosema “hatua anazochukua Rais huyo katika kuinua uchumi.”
Shaka amesema wamemuandikia barua Inspekta Jenerali
wa Polisi (IGP) Ernest Mangu kutaka ruhusa ya kufanya maandamano hayo aliyosema
ni ya amani.
Msemaji wa jeshi hilo hakupatikana kuthibitisha kama
wamepokea barua hiyo.
Habari hii kwanisani ya Mwanahalisi oline
