Zinazobamba

WAZIRI NAPE AYAFUNGIA MAGAZETI 473,SOMA HAPO KUJUA


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEinNzRVEvaF9vDhlGd57QP1_w6E-nu5VptTKK1wdlm5XU4YjEetd7wgdOxp6ToOjonXASoPyTQCErcgin47ZXY7X8Uo3o4QMU5CE6oXE4TlwQftmQKsWsQ-I0DLljoysCVv5cFV5q52ROs/s1600/OTH_7757.JPG




Na: Frank Mvungi - Maelezo
Serikali imefuta usajili wa magazeti 473 kupitia tangazo lake lililochapishwa katika Gazeti la Serikali lenye namba 195, (Supplement No. 23) la tarehe 10/06/2016 kutokana na Magazeti hayo kutochapishwa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye wakati akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam.

Mhe. Nnauye alifafanua kuwa kutokana na kufutwa kwa viapo vya usajili wa magazeti hayo, mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza magazeti yaliyotajwa katika tangazo hilo kwa njia ya nakala ngumu au kieletroniki atakuwa anakiuka sheria ya magazeti sura ya 229 kifungu cha 6 na hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Iwapo kuna mmiliki wa gazeti ambaye angependa kuendelea na biashara hii baada ya kufutwa magazeti hayo, milango iko wazi kwa ajili ya kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata taratibu zilizopo” alisisitiza Mhe. Nnauye.

Akifafanua Mhe. Nnauye amesema kuwa wamiliki wa magazeti 473 yakiwemo Alasiri, Pambamoto, Mipasho, Mirindimo, na Taifa Tanzania ambao viapo vyao vimefutwa, wahakikishe kwamba hawavunji sheria kwa kuanza biashara hii ya magazeti bila kufuata taratibu za kujisajili upya na endapo watakiuka maelekezo hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Kwa mujibu wa kifungu cha 23 (1), Waziri mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya Habari amepewa mamlaka ya kufuta hati za viapo zilizoandikishwa na gazeti ambalo halikutolewa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo baada ya kutangaza kusudio la kuyafuta magazeti husika kupitia Gazeti la Serikali.

Wizara imefanya mapitio ya viapo vya usajili wa magazeti yote na Ofisi ya Waziri mwenye dhamana ya Habari imejiridhisha kuwa kuna idadi ya magazeti 473 ambayo yamesajiliwa lakini hayajachapishwa kwa zaidi ya miaka mitatu.


Kufuatia hali hiyo, tangazo la serikali Na. 65 la tarehe 22 Machi, 2013 lilitolewa kwa ajili ya kutangaza kusudio la kufuta viapo vya usajili wa magazeti 550 na kupewa fursa ya kujitetea au kuonyesha nia ya kuendelea kuchapisha.

Baada ya tangazo hilo magazeti 77 yalionyesha nia yakuendelea kuchapisha, kwa mantiki hiyo hadi sasa kufuatia orodha ya wakati huo pamoja na kupewa muda mrefu zaidi ya unaotakiwa kuna magazeti 473 ambayo hayachapishwi na yamekosa sifa ya kuendelea kutambulika na msajili wa magazeti kwa mujibu wa sheria.

Aidha Mhe. Nnauye ametoa pongezi kwa wamiliki wa vyombo vya habari ambao wamekuwa wakifuata sheria na taratibu zinazosimamia tasnia ya habari ili kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi kwani Serikali inathamini sana mchango wa huduma ya vyombo hivyo.

Kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya Msajili wa Magazeti iliyopo chini ya Idara ya Habari (MAELEZO), Tanzania inayo magazeti na majarida 881 yaliyosajiliwa kisheria. Hata hivyo licha ya magazeti na majarida kusajiliwa yapo baadhi yameshidwa kuchapishwa na wamiliki mara baada ya kusajiliwa na mengine yalichapishwa kwa muda mfupi na kuacha kabisa uchapishaji.