DK MWAKA AIBUA MAPYA, NI KUHUSU KUFUNGIWA KWAKE,SOMA HAPO KUJUA
HATUA iliyochukuliwa ya kufungia kituo cha tiba
asili cha tabibu Dk. Juma Mwaka ‘Foreplan’ pamoja na vituo vingine viwili,
kumesukumwa na maslahi binafsi, anaandika Regina Mkonde.
Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala nchini limelalamikiwa kuchukuwa hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa
msukumo wa binafsi ya baadhi ya watumishi wa baraza hilo na kwamba, sababu
zilizotolewa ni za ‘kipuuzi’.
Pia
imeleezwa kwamba, hatua hiyo ni juhudi za kurudisha nyuma ama kukwamisha kwa
makusudi juhudi za waganga wa Tiba Asili.
Hayo
yamesemwa leo na Mohamed Matokeo, Mwenyekiti wa Baraza la Waganga wa Tiba,
Ushauri na Utafiti wa Dawa Asili Tanzania (Bawata) wakati akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
“Bawata
tukiwa chombo huru cha waganga wa tiba asili, tunasikitika sana utendaji kazi
unaofanywa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ambacho ni chombo cha
kiserikali kilichopewa mamlaka ya kusimamia taaluma hii na kuiendeleza,” amesema
na kuongeza;
“Lakini
baraza hilo limekuwa ni chombo kinachorudisha nyuma fani ya tiba asili hapa
nchini, kwani limekuwa likikwamisha kwa makusudi juhudi za waganga wa tiba
asili walioonesha ufanisi katika kutoa huduma ya tiba asili.
Imekuwa
kawaida kwa baraza hilo kuitisha au kuwafungia waganga wa tiba asili na vituo
vyao kwa sababu zinazoonekana ni za kibinafsi.”
Matokeo
ametoa mfano wa tukio lililotokea jana la kufungwa kwa baadhi ya vituo vya tiba
asili ambapo amesema kuwa, wahusika walifungiwa pasipo kupewa nafasi ya
kujitetea na au kuhojiwa.
“Sisi
bawata tunapinga hatua hii ya kiuonevu kwani wametoa maamuzi ya kuwafungia bila
ya kuwahoji wahusika, tena hawa ni waganga halali kisheria wamesajiliwa na
wanalipa kodi vizuri,” amesema.
Sharifu
Karama, Katibu Mkuu Taifa wa Bawata amedai kuwa, kuna baadhi ya watumishi wa
afya wanaojishughulisha na uuzaji wa dawa za tiba asili kwamba ndiyo
wanaochochea kukandamizwa kwa masilahi ya waganga wa tiba asili nchini.
“Kuna
baadhi ya watumishi wa afya wanauza dawa za tiba asili katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, ambapo kwenye jengo la serikali.
“Kutokana
na hali hiyo, Bawata tunaamini kwamba, baraza la tiba asili na tiba mbadala
linaongozwa na waganga wa kisasa na kwamba tuna taarifa kuwa, kuna baadhi ya
viongozi wa baraza hilo nao wanauza dawa asili kwa hiyo wanalitumia baraza
kutimiza hadhma yao,” amesema.
Hata
hivyo, Foreplan ilianza kuwindwa na Hamis Kigwangala, Naibu Waziri wa Afya
baada ya kufanya ziara ya kushtukiza tarehe 15 Desemba mwaka jana na kuibua maswali
mengi.
Ziara
hiyo ilihitimishwa kwa kutolewa siku saba za uchunguzi na kwamba,
kinachofanyika sasa kinatajwa kuwa ni matokeo ya ‘dhamira’ iliyooneshwa baada
ya ziara hiyo.