BAVICHA YAKINUKISHA DODOMA,POLISI WAHAHA KILA KONA,SOMA HAPO KUJU
Gari la Polisi la maji ya kuwasha likituliza ghasia |
MJI wa Dodoma umezingirwa na Jeshi la
Polisi. Gari la maji ya kuwasha na yaliyobeba polisi muda huu ndiyo
yanayoonekana kwa wingi kwenye maeneo mbalimbali tofauti na ilivyo kawaida,anaandika Dany Tibason.
Polisi wanaonekana kuwa tayari kwa lolote, wamejaa kwenye magari
yao huku wakizunguka maeneo mbalimbali ya Mji wa Dodoma sambamba na gari la
maji ya kuwasha ili kukabiliana na kile kinachojulikana kuwa ni vijana wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (Bavicha).
Kwa wiki mbili
sasa kuna kutupiana maneno kati ya Jeshi la Polisi, Bavicha na Umoja wa Vijana
wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuhusu kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa CCM mjini
Dodoma wiki mbili zijazo.
Bavicha
wamedhamiria kuzuia mkutano huo uliolenga kukabidhiwa uenyekiti wa CCM kwa Dk.
John Magufuli kutoka kwa mwenyekiti wa sasa, Dk. Jakaya Kikwete.
Awali, Jeshi la
Polisi lilipiga marufuku mikutano yote ya hadhara na ya ndani ya vyama vya
siasa, hali ambayo imeathiri mikutano ya Chadema hivyo Bavicha kudhamiria
mkutano wa CCM kutofanyika. Marufuku ya mikutano ya kisiasa ilianza kutolewa na
Rais Magufuli
Kutokana na
dhamira hiyo, UVCCM walionya mkutano wao kutoingiliwa na yoyote, hata hivyo
Jeshi la Polisi limeshindwa kuzuia mkutano huo huku wakibadili kauli kwamba,
mikutano ya ndani haikuzuiliwa.
Bavicha
wamedhamiria kukutana Dodoma ‘kuisaidia’ polisi kuvuruga mkutano huo, hata
hivyo polisi inatetea mkutano huo.
Mjini Dodoma
leo, wananchi wamelazimika kusimamisha shughuli zao na kushangaa magari zaidi
ya 20 yakiwemo ya kuwasha, magari ya askari wa mbwa na askari wengi wakiwa na
sare zao, silaha za moto pamoja na mabomu ya machozi.
Kwa mujibu wa
Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma amedai, ni mazoezi ya
kawaida ambayo wameamua kuyafanya muda wa mchana badala usiku kama walivyozoea.
Mambosasa
amesema, wamelazimika kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa vya kipolisi ili
wananchi waweze kutambua kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lipo imara zaidi.
Amesema, mazoezi
hayo ni sehemu tu ya mazoezi huku akitamba kuwa, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma
lipo imara “na asiwepo mtu yoyote ambaye atajaribu kuingilia kazi za polisi.”
“Wale wote ambao
watajipendekeza kwa madai ya kutaka kulisaidia Jeshi la Polisi, watakipata cha
mtema kuni,” amesema na kuongeza;
“Hakika nataka
kuwaeleza wananchi, asiwepo mtu wa kujaribu kwani tutawakamata na ijulikane
wazi kuwa, kuingia rumande ni rahisi lakini kutoka itakuwa ngumu.”
Patrick Ole
Sosopi, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha Taifa amesema, kitendo cha Jeshi la Polisi
kuzunguka mji mzima kwa kuonesha vifaa vyao vya kivita ni dalili za uoga.
“Kitika kitendo
ambacho kimefanya na Jeshi la Polisi ni dalili uoga na inaonesha ni jinsi gani
Bavicha walivyo na nguvu kiasi cha kulitikisa jeshi hadi kufikia hatua ya
kufanya vitisho,” amesema Sosopi.