MAALIM SEIF AMUONEA HURUMA DK SHEIN,AFUNGUKA YAMOYONI,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
| Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar, akiwa na aliyekuwa Makamu wake, Maalim Seif Shariff Hamad wakati wa utawala wao |
TAREHE 20 Machi 2016, kulifanyika uchaguzi wa
marudio wenye utata katika visiwa vya Zanzibar, ambao ulisuswa na chama kikuu
cha upinzani visiwani humo, Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar (CUF).
Aliyetangazwa mshindi ni Dk.
Ali Mohamed Shein, rais aliyegombea akiwa madarakani, akashindwa kwenye
uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 ambao Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), badala ya kutangaza mshindi, akaufuta kinyume
cha sheria, na kusababisha mgogoro mpya wa kisiasa.
Tayari
Dk. Shein ameapishwa kuongoza Zanzibar kwa ngwe nyingine ya miaka mitano.
MwanaHALISI lilifanya mazungumzo na Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa
CUF, aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, ambaye aligomea uchaguzi
wa marudio.
Yafuatayo
ni maswali na majibu kati yake na gazeti hili, Jumatano iliyopita, siku moja
kabla ya Dk. Shein kuapishwa, kama yalivyoandikwa na mwandishi wetu, Josephat
Isango.
MwanaHALISI: Uchaguzi umefanyika Zanzibar na
nyie mlitoa msimamo kuwa hamtashiriki na kweli hamkushiriki. Nini kinafuata
sasa?
Maalim Seif: Nitajibu kwa namna mbili: Kwanza,
CCM wamwapishe rais wao, watamwapisha Dk Shein na yeye ataunda serikali yake
ataendelea.
Pili,
tunasema Uchaguzi wa 20 Machi haukuwa halali, uchaguzi huru na wa haki
ulifanyika Oktoba 25, wala Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha
Salimu Jecha hakuwa na mamlaka kisheria ua kikatiba ya kufuta, yote yaliyofuata
ni haramu sisi tulitangaza hatutashiriki lakini pia hatutaitambua serikali
iliyoundwa baada ya uchaguzi wa marejeo na hatutaipatia ushirikiano wa namna
yeyote ile.
MwanaHALISI: Huko nyuma mlikuwa mnafanya siasa
ndani na nje, safari hii hamtakuwepo kwenye baraza la wawakilishi, mtaendeshaje
harakati za kudai haki ndani ya Zanzibar?
Maalim Seif: Hili siyo la mwanzo, lilishawahi
kutokea. Wenzetu waliwahi kulazimisha uchaguzi katika majimbo kadhaa ya Pemba,
na sisi tulishiriki kwa aina yake, wananchi walipiga kura za maruhani.
Utakuta
mwakilishi anachaguliwa kwa kura mia mbili, au mia moja tukawa hatupo katika
baraza la wawakilishi, wakati wa Rais Dk. Salmini Amour, vile vile tulisusia,
wawakilishi wetu hawakuwepo lakini chama cha CUF kiliimarika.
Sasa
mara hii tunasema hatumo katika Baraza lakini tumo katika Bunge la Jamhuri ya
Muungano, na wabunge wetu wapo tena wengine ni mawaziri vivuli, kwa hivyo siasa
tutaifanya vizuri maana kila chama kinapopata mitikisiko ndipo kinaimarika
zaidi na wananchi wanakuwa na ari zaidi kukijenga chama chao.
MwanaHALISI: Kule Zanzibar hivi sasa wananchi
wanasubiri kujua nini kinafuata baada ya uchaguzi, na CCM wamechukua hata
majimbo mliyokuwa nayo ya wawakilishi na madiwani, unawaambiaje sasa wananchi
wa Zanzibar?
Maalim Seif: Nawaambia wananchi wa Zanzibar CUF
tunaaamini katika amani, tusifanye jambo lolote litakaloharibu au kuchafua
amani ya nchi, sisi bado tunazo njia za kuendeleza mapambano haya kwa amani.
Hatuitambui
serikali, hatushikirikiani nayo, na hatuko tayari kufanya lolote na serikali ya
Dk. Shein, tutaipinga ndani na nje.
MwanaHALISI: Migogoro Zanzibar imekuwa ya muda
mrefu na ya kihistoria. Umetafuta urais kwa miongo miwili, sasa nini kinaweza
kunusuru Zanzibar kisiasa?
Maalim Seif: Nilidhani maridhianao ya Wazanzibar
ya mwaka 2009 ambayo yalifikiwa baada ya mimi na Dk. Abeid Aman Karume, (Rais
wa Awamu ya Sita) kukubaliana kwamba yaliyopita yamepita tuanze ukurasa mpya.
Nilishuhudia
akimaliza muda wake alisema atahakikisha uchaguzi uliofanyika unakuwa huru na
haki, kwa kiasi kikubwa huu haukuwa wa haki, ulikuwa wa vitisho vya majeshi na
matumizi ya nguvu.
Wakati
ule kila mtu alipiga kura na tukaunda serikali ya kitaifa, na nyie ni mashahidi
kwa miaka mitano tulikwenda vizuri. Hasama zote zilizokuwepo na migogoro
ilimalizika Wazanzibar wakashirikiana bila kujali tofauti za itikadi za
kisiasa.
Walifanya
kazi kwa mashirikiano makubwa. Ni jambo la kusikitisha kwani kwa kile ambacho
CCM wanasema lazima washinde, wamekataa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka
jana, hawana sababu yeyote, sababu zote ni za kupika na muda wote tukiwaambia
leteni ushahidi, walishindwa.
Lakini
sababu wanasema hawawezi kukubali wapinzani kuongoza Zanzibar, walimtaka na
kumlazimisha Jecha afute uchaguzi ule na kuandaa uchaguzi mpya, hivyo mgogoro
huu chanzo ni CCM.
Pia
mimi nilidhani tulishapita huko lakini kwa kuwa CCM wanataka ni lazima
washinde, isiposhinda inaonekana haukuwa wa kidemokrasia, kwa kweli
inasikitisha. Wameturejesha miaka 20 nyuma na sasa katika baadhi ya maeneo
tayari hasama zimeshaanza.
Watu
wa itikadi tofauti hawashirikiani kwa lolote hata kama kwenye masuala ya
mazishi.
Tofauti
ni kwamba hawa wenzetu (CCM) wanaangalia suala la madaraka tu lakini masuala
mapana ya maslahi ya nchi hawana habari nayo, sisi hatukubali hivyo.
Otherwise
(vinginenvyo) wafute mfumo wa vyama vingi, wabaki na chama kimoja, lakini kama
kuna mfumo wa vyama vingi basi kuna kushindwa na kushinda. Haiwezekani wao
lazima washinde.
Hatuwezi
kukubali hili maana tukikubali na kuacha mambo yaende yanavyoenda, inawezekana
mwaka 2020 upinzani unaweza kushinda huku bara lakini CCM wakakataa.
Tumeona
mfano mzuri katika sakata la uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar hadi Rais John
Magufuli alipotoa kauli ndio CCM wakarudi nyuma.
Hatukubali
kabisa, hili halitaishia hapa, tutatetea haki za wananchi, tutatetea maamuzi
yao kwa njia za amani kabisa.
MwanaHALISI: Inaonekana kuwa katika matokeo
yaliyotangazwa na tume, Wazanzibari walijitokeza kwa wingi kupiga kura hata
wale wa Pemba ambapo ni ngome ya CUF.
Maalim Seif: Kila kitu kilishapikwa hata kabla
ya uchaguzi, tunashukuru baadhi ya vyombo vya habari vilionyesha jinsi hali
ilivyokuwa, sio Pemba tu bali hata Unguja.
Unguja
walijitokeza wanawake tena wazee, lakini wanaume na vijana hawakuonekana, ila
tukasema hawa watapika matokeo. Ushindi tuliopata ni kuwa watu waliitikia wito
wetu, na kweli hawakujitokeza kupiga kura.
Namhurumia
kweli Dk. Shein, ikiwa anaamini kapata kura zile anajidanganya, maana hata
alipopiga kura yeye alizungukwa na vikosi tu lakini wananchi walikuwa wachache.
Wazanzibar
waliitikia wito wetu, hawakwenda kupiga kura, na wengi wao waliungana.
Tuliambiwa wengine walipewa kura sita hadi kumi ili watumbukize tu, masuala
yalikuwa wazi. Jecha alitangaza matokeo feki, ni yao ya kujidanganya.
MwanaHALISI: Je, mmeshawasha taa kabisa kuwa
hamtashiriki tena uchaguzi kama siasa za Zanzibar zinaenda kama CCM
wanavyotaka, unadhani nini kifanyike?
Maalim Seif: Kama yatatokea maridhiano
yatakayoongozwa na kusimamiwa na vyombo na taasisi huru za kidemokrasia, bila
vitisho vya majeshi na polisi – vyombo vya dola vikae pembeni – kuwa na vyombo
huru vya habari vinavyotenda haki na tume huru, sio hii iliyopo Zanzibar chini
ya Jecha, hapo CUF kitaweza kufikiri kushiriki uchaguzi.
MwanaHALISI: Msimamo mkali wa CUF juu ya muundo
wa muungano unawezekana ndio unaipa hofu CCM ambayo umesema imekuwa haikubali
kuacha madaraka visiwani Zanzibar, labda huo msimamo wenu mkali kabisa juu ya
muundo wa muungano wa kuitaka Zanzibar yenye mamlaka kamili ndio hofu kuu ya
CCM na Mpo tayari kubadilisha msimao wenu?
Maalim Seif: Mimi niseme visingizio tu hivyo;
hata nilipokutana na Rais Jakaya Kikwete kabla ya kuondoka, aliniambia,
“Maalim, CCM inakuogopa.” Nikamuuliza, “kwanini waniogope?” Akasema, “kwa
sababu utavunja muungano!” Mimi nikamuuliza, “Rais, hivi na wewe unaamini kweli
mimi naweza kuvunja Muungano?
Rais
wa Jamhuri ya Muungano ndiye mwenye vyombo vyote, ndiye mwenye jeshi, polisi,
usalama wa taifa na vyombo vyengine. Rais wa Zanzibar ana nini? Sasa vipi huyu
mtu dhaifu hana chochote atavunja Muungano?”
Kwa
hivyo, hizi ni sababu tu. Lakini niseme tu, kwamba Muungano hautovunjwa na CUF.
Muungano utavunjwa na CCM. Haiwezekani kabisa kabisa kabisa Wazanzibari kila
mwaka wanafanya maamuzi halafu Serikali ya Muungano na CCM Bara wanaingilia,
wanawapa watu ambao wamekataliwa. Hivi unadhani leo waulize Wazanzibari,
wangapi wana imani na Muungano? Ikiwa wanataka Muungano wa majeshi, well and
good (sawa, vizuri), lakini mimi naamini katika Muungano ambao umo kwenye nyoyo
za wananchi.
Hasa
kwa vitendo ambavyo wanatufanyia wenzetu CCM wa Bara, Wazanzibari hawawezi kuwa
na imani na Muungano huo hata siku moja; kwamba hawa hatuwataki, ninyi
mnalazimisha hao hao, halafu unatazamia Mzanzibari awe na imani na Muungano!
Kwa hivyo, Muungano utavunjwa na CCM, tena CCM Bara na Serikali ya Muungano.
MwanaHALISI: Kwanini unaamini CCM Bara wanataka
kuvunja Muungano?
Maalim
Seif: Wao wanavyosema hawataki. Wanataka kulazimisha, lakini watavunja
Muungano, kwa sababu ya vitendo vyao kama nilivyosema. Muungano lazima uwe
katika nyoyo za wananchi. Huu Muungano ambao wanasema wa kulazimisha, wataweka
majeshi miaka nyote kule Zanzibar, vitendo hivyo ndivyo vitakavyosababisha
Muungano kudhoofika na mwisho kuvunjika.

No comments
Post a Comment