DK SHEIN ASUSIWA URAIS WAKE,MABALOZI WA MAREKANI NA EU WAMWACHA SOLEMBA,SOMA HAPO KUJUA

Mabalozi kutoka Marekani na Nchi za Umoja wa Ulaya, wameendelea
kuonyesha msimamo wao wa kutoridhishwa na uchaguzi wa marudio Zanzibar baada ya
jana kususia mwaliko wa kushiriki sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed Shein.
Wanadiplomaasia hao
walipewa mwaliko rasmi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), lakini
waliiambia kuwa hawatashiriki sherehe hizo.
Mkurugenzi wa Mambo ya
Nje Zanzibar, Silima Kombo Haji, aliliambia Nipashe kuwa serikali ilitoa
mwaliko rasmi kwa Mabalozi wote wa nchi za Afrika na Ulaya kuhudhuria sherehe
hizo, lakini Mabalozi wa Umoja wa Ulaya na Marekani walijibu kuwa
hawatahudhuria bila kutoa sababu zozote.
“Tumewaalika na
mialiko imewafikia na kutujibu kuwa hawatahudhuria. Hatukuwa na sababu ya
kuwang’ang’ania," alisema Haji.
Hata hivyo, alisema
licha ya Mabalozi wa Marekani na Umoja wa Ulaya kutohudhuria sherehe hizo,
Mabalozi wa nchi nyingine walioalikwa walihudhuria sherehe hizo na wengine
kutuma wawakilishi wao.
Aliwataja Mabalozi wa
nchi waliohudhuria sherehe hizo ambao wengi ni kutoka nchi za Afrika kuwa ni
Balozi wa Cuba, Zimbabwe, DRC, Indonesia, Iran, Kenya, Kuwait, Malawi, Msumbiji
na Oman.
Wengine ni Palestina,
Ruwanda, Algeria, Angola, Burundi, China, Japan, Libia, Pakistan, Umoja wa Nchi
za Kiarabu, India, Uganda, Uturuki, Urusi na Mratibu Mkaazi wa UN.
Nipashe lilipomuuliza
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Roeland van de Geer, endapo walipata mwaliko huo
na sababu za kutohudhuria sherehe hizo, alisema ushirika wao usingeakisi dhamira
ya tamko lililotolewa na Balozi mbalimbali nchini Machi 21, mwaka huu.
Tamko hilo lilitolewa
na Mabalozi na Wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa
Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania,
Sweden, Switzerland, Uingereza na Marekani.
“Tumesikitishwa na
uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) wa kuendesha marudio ya uchaguzi
uliofanyika 25 Oktoba 2015, bila kuwapo makubaliano ya pamoja baina ya pande
kinzani na ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani humo uliotokana na
majadilino baina ya pande husika.
“Ili uwe wa kuaminika
na kukubalika ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa
dhati matakwa ya watu,” lilisema tamko lao la awali na kuongeza:
“Tunarejea wito wetu
kwa Serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua uongozi katika suala la Zanzibar
na kujielekeza katika kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro huu kwa kupitia
mazungumzo baina ya pande husika kwa lengo la kudumisha amani na umoja."
Mabalozi wamekuwa na
msuguano na Serikali ya Zanzibar kwa kupinga kitendo cha Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (Zec) kufuta uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwa kile
wanachodai kuwa haukuwa na kasoro yoyote na kwamba ulikuwa huru na haki.
Mwenyekiti wa Zec,
Jecha Salim Jecha, Oktoba 28, mwaka jana, alifuta uchaguzi mkuu kwa madai kuwa
haukuwa huru na haki, lakini waangalizi wa kimataifa wakisema kuwa ulikuwa huru
na haki.
Wanadiplomasia hao
hawakufurahishwa na kitendo cha Mwenyekiti huyo wa Zec kufuta uchaguzi, hivyo
kutounga mkono uamuzi wa Zec kurudia uchaguzi ambao ulifanyika Machi 20, mwaka
huu na Dk. Shein kushinda kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
CHANZO:
NIPASHE
No comments
Post a Comment