CHAMA CHA ACT WAZALENDO WAIPINGA ELIMU BURE YA MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Pichani ni Viongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo |
TAMKO LILOTOLEWA NA VIJANA WA CHAMA ACT-WAZALENDO KUHUSU ELIMU BURE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Serikali ya awamu ya tano imeanza kutekeleza mpango wa elimu
bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.
Katika
kutekeleza mpango huo hutolewa ruzuku ya Tsh 25,000 kwa kila mwanafunzi wa
sekondari na Tsh 10,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi kwa mwaka
Fedha hizi za ruzuku ni sawa na wastani wa shilling 68 kwa
mwanafunzi mmoja wa sekondari kwa siku na shilling 27 kwa mwanafunzi wa shule
ya msingi kwa siku.
Sisi Ngome ya vijana ya ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar-Es-salaam
tumestushwa na kiasi hiki ambacho ni kidogo kisichoweza kukidhi mahitaji muhimu
ya upatikanaji wa elimu bora nchini
Kwa maana hiyo basi kama serikali imedhamiria kutekeleza mpango
wa elimu bure nchini kupitia utoaji wa ruzuku mashuleni tunaitaka iangalie upya
kiasi hicho kama kinalingana na upatikanaji wa elimu iliyo bora na ifanye mambo
yafuatayo
1.Serikali iongeze kiasi hiki cha ruzuku ili kiweze kukidhi
dhana ya elimu bure na mahitaji ya mashule yetu kufikia kiwango cha shilling
40,000 kwa kila mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka ambapo ni sawa na wastani wa
shilingi 109 kwa siku, na shilingi 25,000 kwa mwanafunzi wa shule ya msingi kwa
mwaka ambapo ni sawa na wastani wa shilingi 68 kwa siku.
2. Tunaitaka serikali iwekee uzio Fedha hizi ili zisijekutumika
kwa ajili ya matumizi mengine yoyote ya serikali nje ya upatikanaji wa elimu
katika eneo husika.
3. Fedha hizi zitumwe moja kwa moja kwenye akaunti za kila shule
na halmashauri zihakikishe kuwa hakuna akaunti hewa
4. Pia tunaiomba serikali itoe mchanganuo wa matumizi ya Fedha
hizi ili kuondoa mgogoro kati ya uongozi ya shule na wazazi.
Ngome ya vijana ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar Es salaam tunaziomba
kamati za shule na wazazi kufuatilia kwa karibu fedha hizi za ruzuku na
matumizi yake kwenye shule zetu.
Kuhusu Bomoa Bomoa inayoendelea
Ngome ya vijana ya ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar Es salaam inaitaka
serikali kuzingatia UTU wakati wa utekelezaji wa sheria kwenye suala la
bomoabomoa.
Kwa kuwa serikali ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha watu wake
wanakuwa katika mazingira salama tunaitaka iwasaidie wahanga wa bomoa bomoa
hiyo hasa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar Es salaam kwa
kuwapatia maeneo ya kujisitiri kwa wakati huu huku mpango endelevu wa
kuhakikisha madhara kama hayo hayajirudii ukiwa unafanyiwa kazi.
Tunaitaka serikali katika kutekeleza sharia yake hiyo ya
kuwaondoa waliojenga mabondeni ihakikishe inawawajibisha na wale wote
waliozembea katika majukumu yao na kuwafanya wananchi kujenga katika maeneo
yasiyo ruhusiwa
Mwisho Ngome ya vijana ACT-wazalendo Mkoa wa Dar Es Salaam
inawapa pole watanzania wote walioathirika na uharibifu wowote uliojitokeza
kipindi hiki cha mvua zilizonyesha na zinazoendelea kunyesha nchini,Kwa
kuharibikiwa Mali zao kama nyumba na mashamba na miundombinu ya kwenye maeneo
Yao.
Karama Kaila
Mwenyekiti WA Ngome ya Vijana Mkoa WA Dar-Es-Salaam.
Imetolewa ,leo januari 24/2016
Hakuna maoni
Chapisha Maoni