WATOROSHA MAKONTENA BANDARINI HAWA HAPA,NI BAHKARESA NA WENZAKE,SOMA KAPO KUJUA
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imetaja majina ya kampuni 43 na
wamiliki wa makontena 329 ambayo yalipitishwa bandarini bila kulipiwa na
kufichuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wiki iliyopita.
Aidha, TRA imesema
imesimamisha kazi watumishi wake 35 wanaofanya kazi katika ngazi mbalimbali,
wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika Geti Namba Tano.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk.
Philip Mpango alisema Mamlaka hiyo iliagizwa na Waziri Mkuu Majaliwa kuchukua
hatua mara moja kwa kufuatilia na kubaini wamiliki wa Bandari Kavu (ICD)
zilizohusika katika kashfa hiyo.
Alisema mbali na hilo
walitakiwa kuwatambua wamiliki wa makontena hayo, bidhaa zilizokuwemo,
kuwalipisha wahusika kodi iliyokwepwa pamoja na kuwachukulia hatua watumishi
waliohusika na upotevu huo.
Dk. Mpango aliyataja
makampuni hayo kuwa ni Lotai Steel Tanzania Ltd iliyokuwa na makontena 100,
Tuff Tryes Centre Company 58, Binslum Tyres Company Ltd 33, Tifo Global Mart
Company Limited 30, Ips Roofing Company Limited 20, Rushywheel Tyre Centre Co
Ltd 12 na Kiungani Trading Co Ltd 10.
Makampuni mengine
yaliyotajwa ni Homing International Limited (9), Red East Building Materials Company
Ltd (7), Tybat Trading Co Limited (5), Zing Ent Ltd (4), Juma Kassem
Abdul (3), Salum Link Tyres (3), Ally Masoud Dama (2), Cla Tokyo Limited (2),
Farid Abdullah Salem (2), Salum Continental Co (2), Zuleha Abbas Ali (2) na
Snow Leopard Building (2).
Wamiliki wengine wa
makampuni ambayo yalikuwa na kontena moja moja ni Abdulaziz Mohamed Ally, Ahmed
Saleh Tawred, Ali Amer, Ally Awes Alhamdany, Awadhi Salim Saleh, Fahed Abdallah
Said, Hani Said, Hassan Husrin Suleyman, Humud Suleiman Humud, Kamil Hussein
Ali na Libas Fashion.
Wengine ni Nassir
Salehe Mazrui, Ngiloi Ulomi Enterprises Co Ltd, Omar Hussein Badawy, Said Ahmad
Hamdan, Said Ahmed Said, Salumu Peculier Tyres, Sapato N. Kyando, Simbo Yonah
Kimaro, Strauss International Co. Ltd na Swaleh Mohamed Swaleh.
Alisema kwa ujumla,
makampuni hayo yalipitisha makontena 329 ambayo yaliondolewa kinyume cha
taratibu kutoka ICD ya Azam inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa And Company
Limited.
Dk. Mpango alisema
bidhaa zilizokuwemo ndani ya makontena hayo ni pamoja na matairi ya magari,
samani mbalimbali, betri za magari, vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa zingine
mchanganyiko.
27 WALIOKAMATWA
Aidha, Dk. Mpango
alisema watumishi 35 wa Mamlaka hiyo wanaofanya kazi katika vitengo mbalimbali
wamesimamishwa kazi, wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika geti namba tano.
Alisema watumishi hao
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano huku akisisitiza kuwa mtumishi
yoyote wa TRA atakayebainika kuhusika katika hujuma hiyo atachukuliwa hatua
kali za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi kulingana na makosa
atakayokutwa nayo.
Alisema TRA inaendelea
kupanga safu ya watumishi wake ili kuthibiti upotevu wa malipo ya kodi na
kwamba wanapitia upya taratibu za utoaji leseni kwa Bandari Kavu ili kuondoa
mianya na kuweka udhibiti katika uondoshaji wa mizigo katika bandari zote na
bohari za forodha.
“Pamoja na hatua hizi,
TRA inafuatilia kwa kina ili kubaini mawakala wote wa forodha walioshiriki
katika upotevu wa makontena hayo na kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia
leseni pamoja na adhabu zingine kwa mujibu wa sheria,” alisema Dk. Mpango
Mwishoni mwa wiki
iliyopita serikali ya awamu tano chini ya Rais John Magufuli ilibaini ukwepaji
wa kodi kwa kutorosha makontena 329 ambayo yamenyima serikali kodi ya Sh.
bilioni 80.
Rais Magufuli
alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade huku Jeshi la Polisi
likiwashikilia maofisa kadhaa waandamizi wa Mamlaka hiyo akiwemo
Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki.
Masamaki na wengine
saba walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu jana.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni