UTEUZI WA MAWAZIRI UZINGATIE JINSIA- TGNP
TGNP Mtandao, Action Aid Tanzania, FemAct pamoja na wanaharakati ngazi ya jamii tumekuwa tukifuatilia kwa ukaribu mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia hatua za awali, upigaji kura na baada ya matokeo kutangazwa. Nia yetu ni kufuatilia na kudai ushiriki kamilifu wa wanawake kwenye mchakato mzima kama wagombea na wapiga kura.
Tunawapongeza Wanawake wote
walioshiriki kwa kujitokeza kujindikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga
kura, waliojitokeza kupiga kura na zaidi kabisa Wanawake wote waliogombea
nafasi mbalimbali za uongozi bila kuvisahau vyama vya siasa na jamii zotezilizowawaunga
mkono na kufanikisha ushindi.
Tunawapongeza wanawake wote
waliothubutu kujitokeza katika kinyanganyiro za uchaguzi kuanzia ngazi ya
uteuzi ndani ya vyama na hatimaye baadhi yao kuingia kama wagombea. Kipekee tunampongeza
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu kwa kudhubutu
na kufanikiwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais Mwanamke tangu taifa letu
kupata uhuru. Pamoja na hayo tunampongeza aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya
chama cha ACT wazalendo Anna Mghwira kwa kuwa mgombea pekee mwanamke wa nafasi
ya Urais kwa udhubutu na ujasiri aliouonesha. Tunatambua na kuthamini jitihada
zake sio kugombea kwake tu, bali hata jinsi alivyobeba ajenda za msingi za wanawake
na wananchi wa kawaida wakati wa kampeni.
Ndugu
waandishi wa habari, takwimu zinaonesha kuwa, idadi ya wanawake mawaziri
iliongezeka kutoka 14.8% (2003/05) kufikia 31.25% (2013/15) wakati idadi ya
manaibu waziri wanawake ikipungua kutoka 30% (2003/05) hadi 24% (2013/15).
Aidha, idadi ya makatibu wakuu wa wizara wanawake ilipungua kutoka 28%
(2003/05) hadi 18.2% (2013/15) wakati idadi ya manaibu katibu wakuu wa wizara
wanawake ikiongezeka kutoka 12.5%(2003/05)
hadi 40.7% (2013/15).
Tanzania ni moja kati ya Mataifa yaliyosaini
mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kikanda inayoweka misingi ya usawa kwa
binadamu ikiwemo haki na usawa katika ushiriki
kwenye uongozi wa ngazi zote. Moja kati ya Mikataba hiyo ni Tamko la Umoja wa
Matifa la Haki za Binadamu(UDHR:1948), Mkataba wa Kimataifa wa Kutokomeza aina
zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW: 1979, Articles 7: a, b na c), Mpango
Kazi wa Beijing (1995), Mkataba wa Ziada wa Maputo, na Mkataba wa Nyongeza wa
jinsia na Maendeleo kusini mwa Africa (SADC Gender Protocol,) ambayo inaelekeza
serikali husika kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi sawa na wanaume katika
ngazi mbalimbali za uongozi.
Hivyo basi tunategemea kulingana na
ahadi za viongozi wetu wakati wanaomba kura kuwa watasimamia utekelezaji wa
mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa, ni matarajio yetu kuwa serikali
mpya chini ya Mhe. Rais John Magufuli
itatekeleza kwa vitendo ahadi hizo hususan katika kuwateua Wanawake zaidi
katika nafasi za juu za uongozi katika mihimili mikuu mikuu mitatu ya serikali
(Mahakama, baraza la mawaziri na bunge).
Pia ikumbukwe kuwa, Mhe. Rais
Mstaafu Jakaya Kikwete akiwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa viongozi wa
nchi wanachama uliofanyika mwaka huu 2015 nchini Marekani aliahidi kuwa
Tanzania itasimamia utekelezaji wa kanuni ya 50/50 na kuweka mifumo mizuri ya
ufuatiliaji na uwajibikaji wa utekelezaji wa masuala yote ya usawa wa kijinsia
na matamko ya kimataifa na kikanda katika ngazi ya taifa na jamii.
Kwa kuzingatia hayo, tunasisitiza
kuwa Baraza la Mawaziri lijalo pamoja na nafasi zote za uteuzi serikalini
zibebe sura ya usawa wa Kijinsia. Nafasi nyinginezo ni pamoja na uteuzi wa
wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa
wizara mbalimbali, wakurugenzi na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma
kadhalika uteuzi wa bodi mbalimbali katika mashirika na taasisi hizo bila
kusahau uteuzi katika mihimili ya mahakama na bunge. Ni matarajio yetu kuwa,
mamlaka za kiuteuzi ikiwa ni pamoja na Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wa wizara
mbalimbali watazingatia kikamilifu usawa wa kijinsia katika uteuzi wowote
watakaofanya. TGNP Mtandao na Action Aid tutahakikisha kuwa tunafuatilia kwa
karibu teuzi zitakazofanyika.
Mwisho tunawataka Wanawake wote
waliochaguliwa kwenye nafasi za uongozi Ubunge na udiwani kuwajibika kikamilifu
kwa kuitumikia Jamii iliyowapa ridhaa, waoneshe mfano wa kuigwa kwa kujenga
hoja za msingi zenye maslahi mapana kwa Jamii hasa Wanawake wanapokuwa kwenye Bunge au vikao vya
Halmashauri ili kuleta tija na mabadiliko chanya kwa Jamii. Tunarajia kama
ilivyokuwa katika awamu zilizopita sisi asasi za kiraia tutaendelea
kushirikiana na serikali iliyoingia madarakani katika kuleta maendeleo ya
Taifa.
No comments
Post a Comment