Zinazobamba

SPIKA NDUGAI AWAUMBUA WABUNGE WANAOPINGA POSHO,SOMA HAPO KUJUA

Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto
Pichani ni Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabweni miongoni mwa wabunge wanaolalamikia posho kupitia mitandaoni

Siku moja baada ya Mbunge mpya wa Jimbo la Singida Magharibi kukataa kuchukua posho zake za vikao vya Bunge kwa kipindi cha miaka mitano ya ubunge wake badala yake zisaidie shughuli mbalimbali za maendeleo jimboni kwake,  Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema jambo hilo haliwezekani labda yapelekwe mapendekezo ya kupunguzwa posho hiyo.

Alisema posho inayotolewa kwa kila Mbunge ya Sh.  220,000 ni kwa ajili ya kuwawezesha wabunge kujikimu kwa siku za vikao vya Bunge, hivyo  kupunguza ni kuwafanya waishi maisha magumu.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Ndugai posho hiyo ni kwa ajili ya kuwawezesha wabunge kulala hoteli zenye hadhi kwa ajili ya usalama wao.

“Lengo la posho hizi ni kuwawezesha wabunge kuzitumia kwa ajili ya malazi na matumizi mengine, hao wanaosema zipelekwe kwenye matumizi mengine ni vyema wakatambua kuna utaratibu wa namna ya kutoa fedha za Bunge na siyo kuzihamisha kwenda kaunti nyingine,” alisema.  

Hata hivyo, alisema wapo tayari kupokea maoni na mapendekezo ya kiwango gani kinafaa wabunge kulipwa, lakini siyo Bunge kupeleka fedha kwenye maeneo  mengine kama wengine walivyoomba.

Alisema Bunge haliwezi kufanya malipo yoyote nje ya akaunti ya Mbunge mwenyewe.

Ndugai alisema malipo yoyote kwa Mbunge au wabunge hufanyika kwa utaratibu uliowekwa ambao haiwezekani kubadilishwa kutokana na kanuni za kihasibu.

Akizungumza na Nipashe jana, Ndugai alisema malipo yoyote yaliyopo bungeni yamewekwa kwa kuzingatia mambo mengi bila kukurupuka.

Alisema kulingana na taratibu za serikali na Bunge, hairuhusiwi kuelekeza Katibu wa Bunge kutuma fedha kwenye akaunti ambayo siyo ya Mbunge.

“Bunge litaanzaje kulipa watu ambao haliwajui?, hicho kitu hakiwezekani kihasibu, kwaninini mbunge anayehusika asichukue hiyo hela kama utaratibu unavyotaka halafu yeye mwenyewe ndiyo akatoe katika akaunti, tatizo lao ni nini katika kufanya hivyo na kutaka Bunge lifanye?” alihoji.

Ndugai alisema kihasibu watahojiwa, hivyo ni vyema wabunge wenye nia hiyo wakazipokea wao wenyewe na kuzipeleka wanapotaka.

“Utahojiwa huyu ulimlipa kwasababu gani?. Ni kawaida kwa wabunge wageni wanapoingia wanafikiri kuna hela nyingi lakini wanapomaliza miaka mitano wanagundua hela haitoshi wanaanza ugomvi na serikali,” alisema.

Kuhusu kupitia sheria au kanuni zinazofanya wabunge walipwe posho, Ndugai alisema vikao vya kujadili jambo hilo vilishakaa na mapendekezo yapo Ikulu.

“Ile Tume ya Huduma za Bunge ndiyo huwa inakaa na ilishafanya hivyo na mapendekezo yapo Ikulu,” alisema Spika.
Hivi karibuni, Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu, alitangaza kutochukua posho zake za vikao vya Bunge zinazozidi Sh. milioni 200 katika kipindi chake chote cha miaka mitano atakayokuwa akitumikia nafasi hiyo.

 Kingu aliIandikia Ofisi ya Bunge akiomba asilipwe yeye bali fedha hizo zipelekwe kwa wananchi wa jimbo lake ili zisaidie shughuli za maendeleo ambapo ni posho za kila kikao Sh. 220,000  ambazo kwa mwaka mzima wenye vikao takriban 182 huwa ni sawa na Sh. milioni 40.04 na kwa miaka yote mitano ni Sh. milioni 200.20. 

Alisema haoni kuwa ni sahihi kwa yeye (Mbunge) kupokea posho za vikao wakati atakuwa pia akilipwa mshahara kila mwezi na posho ya kujikimu kila mara atakapokuwa akitimiza majukumu yake nje ya kituo cha kazi.

MAONI YA WABUNGE
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Nipashe kuhusiana na posho hizo, walisema ni muhimu kwao kwani mishahara pekee haitoshi kushughulika na matatizo ya wananchi.

Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema posho anayoipokea kwa ajili ya vikao vya Bunge hawezi kuacha kuipokea kwa sababu inamsaidia katika shughuli mbalimbali hasa kwa wananchi wake.

“Mshahara pekee yake bila posho hautoshi na Mbunge anayepinga uwepo wa posho labda ana fedha nyingi zinazomuwezesha kutekeleza majukumu yake, wananchi wamekuwa wakitutegemea zaidi kwa matatizo yao binafsi na hizi posho ndio zinatusaidia,” alisema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), alisema jambo hilo ni gumu kwani wananchi wamekuwa wakiwageuza wabunge wao ATM kwa kuwaomba fedha.

“Wengine wanaweza kupinga uwepo wa posho hizo kwa sababu wamepata mikopo wanajiona wana fedha nyingi, lakini baada ya miaka miwili watakuwa na hali mbaya sana kifedha na ndiyo watafahamu umuhimu wa posho,” alisema.

Alisema fedha hizo za wabunge zimekuwa zikitumika katika hali ya misiba, harusi na ada za shule kwa wananchi wao. 

JUKWAA HURU LAPINGA POSHO
Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania, limetoa tamko la kuwataka wananchi kuwashinikiza wabunge wao kukataa posho za vikao vya Bunge ili fedha hizo zitumike kwenye shughuli za maendeleo.

Aidha, limesema litafanya maandamano ya amani nchi nzima kuhamasisha wananchi kuwaunga mkono kuwataka wabunge kutumia fedha hizo kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali badala ya kutumia kama posho zao binafsi.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa jukwaa hilo, Mtela Mwampamba, alisema wananchi wanatakiwa kumuunga  mkono Rais John Magufuli kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya fedha za umma kwa kuwataka wabunge wao waliowachagua kukataa posho kama njia ya kupunguza matumizi ya serikali yasiyo ya lazima.

Alisema kazi ya Mbunge ni kuwawakilisha wananchi wake bungeni na si kuwanyonya, hivyo taifa linapaswa kuwa na nidhamu ya matumizi ya kodi za wananchi na mgawanyo sawa wa keki ya taifa. 

Mwampamba alisema wabunge kuendelea kulipana posho hizo ni ishara ya unyonyaji, dhuluma na kuongeza pengo kati ya wenye nacho na wasionacho nchini jambo linalokuza chuki na hasira miongoni mwa wananchi wa hali ya kawaida dhidi ya viongozi wao na serikali kwa ujumla.
CHANZO: NIPASHE


Hakuna maoni