JAJI ALIYERUHUSU UCHOTWAJI WA MABILIONI YA ESCROW KUHUKUMU HATMA YA UBUNGE WA KAFULILA,SOMA HAPO KUJUA
Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kupinga matokeo ya
uchaguzi itaanza kusikilizwa leo na Jaji John Utamwa katika Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Tabora.
Kafulila aliyekuwa
Mbunge kinara katika kuibua ufisadi wa sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh.
bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), anakutana ‘uso kwa uso’ na Jaji Utamwa, ambaye ndio alitoa hukumu tata
iliyosababisha kuibuka kwa kashfa ya ufisadi wa fedha hizo.
Jaji Utamwa aliitoa
hukumu hiyo, Septemba 8, 2013 kwa kumwamuru Kabidhi Wasihi, kukabidhi mtambo wa
Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)
kwa mmiliki wake mpya ambaye ni kampuni ya Pan Africa Power Solutions Tanzania
Limited (PAP) baada ya kukubaliana na maombi ya aliyekuwa mbia wa IPTL, kampuni
ya Engineering and Marketing Limited (VIP) iliyoondoa kesi yake kwa lengo la
kuifilisi IPTL.
Hukumu hiyo ndio
ilikuwa chanzo cha Kafulila kuibua kashfa hiyo bungeni kwa kuwahusisha vigogo
mbalimbali wa serikali na ufisadi huo.
Hatua hiyo ya Kafulila
ilisababisha serikali kumuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kuchunguza kashfa hiyo.
Takukuru na CAG
ziliwasilisha matokeo ya uchunguzi huo kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC).
Taarifa ya uchunguzi
huo iliyowasilishwa bungeni mwishoni mwa mwaka jana na aliyekuwa Mwenyekiti wa
PAC, Zitto Kabwe, iliwahusisha vigogo kadhaa wa serikali wakiwamo waliopewa
mgawo wa mamilioni ya Shilingi kupitia benki mbalimbali nchini.
Kashfa hiyo
ilisababisha kujiuzulu kwa Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali, Jaji
Frederick Werema na pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Aliyekuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alifutwa kazi na
Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Pia wabunge kadhaa
waliondolewa katika nafasi za uenyekiti wa kamati za Bunge na baadhi ya
watendaji wa serikali walifunguliwa mashauri katika Baraza la Maadili huku
wengine wakifunguliwa kesi mahakamani.
KESI YA KUPINGA
MATOKEO YA UBUNGE
Jaji Utamwa atasikiliza
leo ombi la malipo ya dhamana ambalo Kafulila atatakiwa kulipa kwa kufungua
kesi ya kulalamikia matokeo.
Kafulila anaomba
apunguziwe kiasi cha dhamana ili asilipe Sh. milioni 15 kwa kuwalalamikia
walalamikiwa watatu.
Walalamikiwa hao ni
aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Husna Mwilima, aliyeshinda
katika uchaguzi wa ubunge wa Oktoba 25, mwaka huu kwa kupata kura 34, 453 dhidi
ya kura 33,382 alizopata Kafulila.
Mlalamikiwa mwingine
ni aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Uvinza, mkoani Kigoma, Ruben Mfune, na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju.
Kwa mujibu wa sheria,
mlalamikaji anapofungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge mahakamani, anatakiwa
kuweka dhamana ya Sh. milioni tano kwa kila mlalamikiwa. Kwa maana hiyo,
Kafulila atatakiwa kuweka Sh. milioni 15 kwa walalamikiwa wote watatu, hivyo,
anaiomba Mahakama ipunguze kiasi hicho.
Katika kesi
hiyo, Kafulila analalamika kuwa matokeo yaliyotangazwa na msimamizi huyo wa
uchaguzi hayakuwa ya halali, hivyo kuiomba Makakama kumtangaza yeye kwa maelezo
kuwa ndiye mshindi halali.
Kadhalika, anaiomba
Mahakama kuiamuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kujumlisha upya matokeo hayo
kutoka katika vituo 382, ambavyo anadai ana fomu zake za matokeo na baada ya
hapo kumtangaza mshindi.
Kafulila pia
anamlalamikia msimamizi wa uchaguzi huo kwa kutangaza matokeo hayo kufuatia
shinikizo la Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Issa Machibya na viongozi wengine wa
serikali wa wilaya ya Uvinza.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni