Zinazobamba

SHULE YA MSINGI IBN JAZARY YANG’ARA MTIHANI WA TAIFA DARASA LA SABA 2015, YABEBA SHULE ZINGINE ZA KIISLAMU.




SHULE YA IBN JAZARY YANG’ARA MTIHANI WA TAIFA DARASA LA SABA 2015

  • ·       Yaongoza shule zote za binafsi na serikali

  • ·       Shule yapanga mikakati ya kuongoza kitaifa
Kiongozi wa shule ya msingi ya kiislamu ya Ibn Jazary  sheikh Othman Kapolo(mwenye kanzu nyeupe) akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa shule hiyo. Shule ya Ibn Jazary imeshika namba moja kwa mkoa wa Pwani

SHULE ya msingi ya kiislamu ya Ibn Jazary iliyopo mkoa wa Pwani wilayani Mkuranga imeandika historia mpya katika rubaa za Elimu baada ya kufanikiwa kuongoza katika matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa hivi karibuni
Shule hiyo imefanikiwa kuziongoza shule maalufu za serikali na binafsi katika mkoa wa pwani baada ya wanafunzi wake kupata ufaulu wa daraja la kwanza“A”  na kuifanya shule hiyo kushika nafasi ya kwanza kiwilaya na Mkoa .
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya serikali iliyotangazwa na baraza la mitihani nchini (NECTA), shule hiyo iliyokuwa  na jumla ya wanafunzi 57 ni watoto wawili pekee ndiyo waliopata daraja la pili “B” matokeo yaliyowafanya kuwa wa kwanza katika wilaya ya Mkuranga kati ya shule 106 na ya kwanza kimkoa kati ya shule 530 na ya 111 kitaifa kati ya shule 16096.
Akizungumza na gazeti Imaan, muangalizi mkuu wa shule hiyo sheikh Othman Kapolo alisema wamefurahishwa sana na taarifa ya matokeo hayo na kwamba wanawapongeza vijana kwa kutowaangusha walimu na kuitanga shule vizuri
“Tunashukuru wanafunzi wetu wamefaulu vizuri, na masomo ambao wamefaulu kwa daraja “A” kwa wanafunzi wote ni masomo ya Kingereza na hisabati wote wamepata “A”. Utaona hapo ndugu mwandishi jinsi gani watoto walivyoweza kuonyesha uhodari wao katika masomo yanayoogopwa” Alisema
Aidha akizungumzia jitihada zilizofanyika hadi kufikia mafanikio hayo, sheikh Kapolo alisema walimu pamoja na uwongozi wa shule ulisimama kidete kuhakikisha vijana wanapata mazoezi ya kutosha baada ya kumaliza slabus zao.
Alisema anawashukuru wazazi, walimu na uwongozi wa shule kwa ushirikiano wao walionyesha wakati wanawaandaa vijana hadi kufikia mafanikio hayo na kwamba ushindi waliopata vijana si wao peke yao bali ni ushindi wa shule, walimu na wazazi kwa ujumla wake


Ameongeza kusema anaamini matokeo hayo hayakuja kwa bahati mbaya,bali yametokana na moyo wa kujituma kwa wanafunzi na walimu na kuiletea sifa shule kwa ufaulu walioupata 

“Kufaulisha wanafunzi wote  57 si jambo la bahati kwani tumeshuhudia shule zingine zikishindwa kufanya hivyo katika mitihani yao ya mwisho," alisema.
Amesisitiza kuwa walimu wa shule zingine hususani za kiislamu nao wanapaswa kuwa na moyo wa uzalendo wa kufundisha kwa ari na moyo wa kujituma ili kuboresha  elimu ndani ya shule hizo

Ameshauri walimu ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu wajitahidi kusahau ugumu huo na kujikita zaidi katika mafundisho, na hiyo ndiyo siri ya mafanikio
Katika hatua nyingine sheikh Kapolo amewatangazia wazazi wanaotafuta nafasi za watoto wao kusoma kwamba nafasi bado zipo katika shule hiyo ya Ibn Jazary na wanatarajia kufanya usahili wa awamu ya pili mwezi wa 12 mwaka huu.
Amesema shule ipo eneo la Vikindu wilaya ya Mkuranga na kwamba ipo katika mazingira mazuri yatakayowafanya vijana kusoma kwa bidii na pia yatawajenga kiimani kwani shule inajitahidi kufundisha Qur’an tukufu.
Kuhusu ufanisi wa mafunzo ya Qur’an Sheikh Kaporo alisema shule hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwawezesha watoto kuhifadhi Qur’an kwani kwa takwimu zilizopo kati ya watoto wote waliomaliza mwaka huu mtoto aliyehifadhi juzuu chache ni 5 lakini wengi wao wapo kati ya juzuu 25 hadi 30.
Aidha sheikh Kapolo ametaja sababu nyingine ya vijana kufanya vizuri ni kutokana na uwezo waliouonyesha katika kuhifadhi kitabu kitukufu cha Qur’an hivyo kwao ilikuwa kazi rahisi kuhifadhi masomo mbalimbali waliyokuwa wanafundisha.
Akizungumzia historia ya ufaulu wa shule hiyo ambayo imeanzishwa mwaka 2006, Sheikh Kapolo alisema shule hiyo ilikuwa na historia nzuri kwani mwaka jana iliweza kushika nafasi ya tatu kiwilaya na nafasi ya 9 kimkoa jambo linalofanya wazazi wengi kuiamini shule na kuleta watoto wao.
“Tunawaaomba wazazi watuamini walete watoto wao hapa shuleni, sisi tumejipanga kufanya kazi kuhakikisha tunafikia malengo makubwa zaidi ya haya tuliyoyapata mwaka huu”Aliongeza.
Mafanikio ya shule za kiislamu katika tasnia ya Elimu yatakuwa kichocheo sahihi ya kuhamasisha shule zingine zinazoendesha na jamii ya kiislamu kuona kwamba ni wakati wa kuamua kuingia kwenye ushindani kwani inawezekana kuongoza hata ngazi ya taifa.
Naye mkuu wa shule ya Ibn Jazary Bw. Seif Swalehe alielezea mafanikio hayo kuwa yalionekana toka katika mtihani wa majaribio(MOCK) ambapo shule hiyo ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kiwilaya hadi mkoa.
Akizungumzia kujipanga kwa shule  hiyo ili kuweza kuibuka kinara wa ngazi ya taifa, Mwl Swalehe alisema wataendeleza mbinu yao ya kufanya kazi kwa upendo na ari ya hali ya juu pamoja na kuwashirikisha wazazi ili wawape uhuru watoto wao kujisomea kwa muda mrefu
Aidha kwa upande wao wazazi hawakusita kuonyesha furaha yao baada ya vijana wao kufaulu kwa daraja la kwanza na hivyo kujihakikishia nafasi ya kusoma katika miongoni mwa shule bora hapa nchini.
Toka mwaka 2012 shule ya msingi Ibn Jazary imekuwa ikipandisha wastani wake wa ufaulu mwaka hadi mwaka na pia wastani wa wanafunzi wanaopata daraja la kwanza umeendelea kuongezeka.
Shule nyingine ya kiislamu ilizofanya vizuri katika mtihani huo wa darasa la saba ni shule ya mchepuo wa kiingereza ya Mudio Islamic iliyopo wilaya ya hai baada ya kufanikiwa kuibuka kinara katika wilaya hiyo.
Shule hiyo ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kati ya shule 117 huku kimkoa ikishika nafasi ya sita kati ya shule 932 na kitaifa ikishika nafasi ya 143 kati ya 16096. Idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani ni 52 na walipata wastani wa 207.1346
Mwisho



No comments