MAALIM SEF AZIDI KUITISHA CCM SOMA HAPO KUJUA

MAALIM Seif
Shariff Hamad, mwanasiasa anayepigania haki ya kuongoza Zanzibar baada ya
kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa Oktoba 25, amesema hakuna sababu ya
viongozi wa CCM kumhofia. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
“Kwani wanaogopa nini wakati nimeshasema mimi
katika uongozi wangu sitalipiza kisasi kwa mtu yeyote. Sina muda wa
kushughulika na mtu katika wakati ambao ninajukumu la kushughulikia maendeleo
ya wananchi,” ameema.
Maalim Seif ambaye kura za vituoni zilizoridhiwa na mawakala wa
vyama vyote pamoja na maofisa wasimamizi wa uchaguzi majimboni, zinemuonesha
kuwa alishinda uchaguzi, ametoa kauli hiyo alipohutubia wajumbe wa mkutano mkuu
na kamati tendaji za wilaya za CUF kisiwani Pemba.
Alikwenda Pemba jana kukamilisha jukumu la kuwaeleza viongozi
waandamizi wa CUF hatima ya mkwamo wa uchaguzi, ikiwa ni wiki mbili tangu
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta
uchaguzi wote Zanzibar.
Alifanya mkutano kama huo juzi Jumatatu kwa wajumbe na viongozi
wa mikoa mitatu ya Unguja, kwenye ukumbi wa Majid, Mombasa, mjini hapa.
Amesema hakuna sababu ya viongozi wa CCM kupata hofu ya
kuongozwa na Maalim Seif kwa sababu ameshapewa ridhaa na wananchi wenye mamlaka
ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.
“Mimi ndiye rais niliyechaguliwa, ndiye ninayeangalia serikali
nitakayoiongoza itakuaje, tena nimeshasema tutaendeleza serikali ya umoja wa
kitaifa na kwa sababu vyama vyetu vimepata viti sawa vya uwakilishi, tutatoa
mawaziri kwa idadi sawa,” amesema.
Amemsihi Dk. Ali Mohamed Shein akubali matokeo ya uchaguzi
yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi kama alivyokubali yeye katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010.
Amesema kwa busara kabisa, “Dk. Shein awe muungwana kwa kuridhia
maamuzi ya wananchi waliopiga kura Oktoba 25 na kunichagua niwe kiongozi wao…
yeye amemaliza muda wake kikatiba tangu Novemba 2, asifanye kinyongo.”
Salamu hizo alizitoa kwa viongozi wa Unguja ambako alisikika
akitamba kuwa haba wasiwasi kuwa ndiye rais mpya na anachosubiri ni “kuitwa kwa
ajili ya kuapishwa na kushika nafasi mara moja.”
“Nanyi msiwe na wasiwasi wowote. Mimi ndiye rais wenu mpya na
tayari nimeanza kutengeneza serikali nitakayoiongoza ambayo itaendelea kuwa ya
mfumo wa umoja wa kitaifa kwa kuchanganya mawaziri kutoka chama chetu CUF na
wenzetu CCM, tutakuwa na mawaziri sawa kwa sawa,” amesema.
Katika serikali iliyomaliza muda wake kufuatia uchaguzi wa mwezi
uliopita, Serikali iliyoundwa na Dk. Shein ilikuwa na mawaziri saba wa kila
upande wa vyama hivyo vya CCM na CUF.
Katika uchaguzi wa safari hii, kila chama kimepata viti 27, CUF
ikivuna viti vyote 18 vya kisiwani Pemba kwenye ngome yake isiyoshindika, na
CCM ikipata viti vyake Unguja.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi chini ya mfumo wa
vyama vingi tangu 1995, CUF imeongeza viti Unguja kufikia tisa. Katika uchaguzi
wa nyuma, ilifikisha viti vitano.
CCM mbali na kutopata kiti chochote cha uwakilishi na ubunge
Pemba, imekosa hata diwani mmoja katika wadi zote kisiwani humo. Katika
uchaguzi wa 2010, ilipata madiwani wawili huko.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, chama
kinachoshindwa uchaguzi kwa kupata zaidi ya asilimia tano ya kura, kitatoa jina
la kiongozi atakayeteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa rais.
Safari hii, na kama Tume itamtangaza Maalim Seif aliyepata kura
nyingi, kuwa ndiye mshindi wa wadhifa wa urais, CUF itatoa makamu wa pili,
ambaye atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali kwenye Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar.
CUF iliteuliwa viongozi wake kuongoza wizara ya Habari;
Miundombinu na Mawasiliano; Katiba na Sheria; Afya na Ustawi wa Jamii; Kilimo
na Uvuvi na Biashara, Viwanda na Masoko na waziri wan chi Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa rais.
No comments
Post a Comment