KATIBU MKUU APONGEZA VYOMBO VYA HABARI , ASEMA NI MFANO WA KUIGWA
Na mwandishi Maalum.
Vyombo vya habari
nchini vimepongezwa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutoa taarifa kwa wananchi
wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwezi wa 10 mwaka huu.
Pongezi hizo
zimetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akiongea na viongozi wa menejimenti ya wizara
na taasisi zake kwenye kikao cha kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Prof. Gabriel
alisema kipindi cha uchaguzi vyombo vya habari vilifaya kazi kubwa ya
kuwahabarisha wananchi habari za uchaguzi kwa kuzingatia weledi wa taaluma yao
na hivyo kuwawezesha wananchi kujua mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea
hapa nchini.
Katibu Mkuu huyo
ambaye hicho kilikuwa ni kikao chake cha kwanza tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu
wa wizara hiyo mwishoni mwa mwezi wa kumi aliahidi kuwatumikia na kuwaheshimu
wafanyakazi wa wizara yake huku akisimamia majukumu ya kazi kwa kufauata
kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa Umma.
“Hiki ni kikao chetu
cha kujipanga kwa ajili ya kazi, ni vyema tukajipanga huku tukijuwa matarajio
ya Mhe. Rais kwetu ni yapi, wananchi tunaowatumikia wanategemea kupata
nini kutoka kwetu na mimi kama Katibu Mkuu natarajia kupata nini kutoka
kwenu”, Prof. Gabriel alisema.
Akimkaribisha Katibu
Mkuu huyo kuongea na viongozi hao Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
watu Titus Mkapa alisema kikao hicho ni maalum kwa ajili ya wizara kujadili
utekelezaji wa mipango ya wizara kwa kasi.
Wakitoa maoni yao
kwa nyakati tofauti viongozi hao waliiomba Serikali iangalie upya bajeti
ya wizara hiyo ambayo ni ndogo ili iweze kuongezwa na kuwawezesha
kufanya kazi zao kwa ufaisi zaidi.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TasuBa)
Michael Kadinde alisema chuo hicho kimekuwa kikizalisha ajira kwa wanafunzi
wanaosoma hapo mara baada ya kumaliza masomo yao lakini wanafunzi wengi
wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na ada.
“Kuna baadhi ya
wanafunzi wanajiunga na chuo hiki wakiwa na elimu ya darasa la saba, na hivi
sasa Serikali itaanza kutoa elimu bure kwa wanafunzi kwa darasa la kwanza hadi
kidato cha nne”.
“Ninaiomba Serikali
iweze kuwaangalia wanafunzi hawa wa darasa la saba ambao wanasoma chuoni kwetu
ili nao waweze kupata elimu bure sawa na wanafunzi wa Sekondari”, alisisitiza
Kadinde.
Kikao hicho
kimeitishwa kufuatia kikao cha Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makatibu
wakuu, manaibu makatibu wakuu na watendaji wakuu wa Serikali
kilichofayika mwishoni mwa wiki ambapo alieleza matarajio yake na
matarajio ya wananchi katika uongozi wake. Hivyo aliagiza kila sekta ikae na
kujipanga kufanya kazi ili kukidhi matarajio ya wananchi.
No comments
Post a Comment