MSIDANGANYWE NA WANASIASA WASIO WA KWELI
MGOMBEA
urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema
mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa kwa kuzungusha mikono, bali
yatakuja kwa kufanya kazi.
Kutokana
na hali hiyo, amesema yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko ya kweli
yanayokwenda na vitendo katika kujenga uchumi wa nchi na watu wake.
Dk.
Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti, alipokuwa
akizungumza wakati wa mikutano ya kampeni iliyofanyika katika majimbo
ya Buchosa, Geita na Busanda.
Katika mazungumzo yake, Mgufuli aliwataka Watanzania wasidanganywe na baadhi ya wanasiasa wanaowataka wasiipigie kura CCM.
Alisema
kwamba, pamoja na baadhi ya wanasiasa kukesha wakihamasisha mabadiliko
kwa kutoichagua CCM, jambo hilo halitawezekana kwa kuwa ni sawa na ndoto
za mchana.
“Ninasema
hapa, eti kuna watu wanahangaika kuzungusha mikono na kusema wanaleta
mabadiliko, ni lazima wajue mabadiliko hayawezi kuja kwa mtindo huo.
“China hivi sasa inatisha kwa kuwa na uchumi wa daraja la kwanza duniani na kuna hatari hata ya kutaka kuizidi Marekani.
“Kwa mfumo wao huo, hawakukiondoa madarakani chama tawala ila walifanya mabadiliko ya ndani ya chama na Serikali.
“Ndiyo
maana Magufuli ninakuja na mabadiliko ya kwenda ndani ya Serikali na
ndani ya CCM. Katika hili, sina mchezo ndugu zangu Watanzania, naomba
mniamini,” alisema Dk. Magufuli.
Kwa kuwa Watanzania wameshaamua kumpa urais Oktoba 25, mwaka huu, jambo atakalo anza nalo ni kuunda mahakama ya mafisadi.
Alisema,
amezaliwa katika familia maskini na hatakuwa tayari kuona wajasiriamali
wadogo wakinyanyaswa na hata kutozwa ushuru ambao umekuwa
ukiwakandamiza katika biashara zao.
Alisema
anajua eneo la Nkome ni maarufu kwa kilimo cha mananasi daraja la
kwanza, lakini bado wakulima wamekuwa wakikosa soko la uhakika.
Kutokana na hali hiyo, atatimiza mkakati wa Serikali yake kwa kujenga kiwanda cha juisi katika eneo hilo.
“Ni aibu kwa nchi yetu inayozalisha matunda kwa wingi, kukosa kiwanda cha kusindika matunda.
“Napenda
kuahidi hapa, nitajenga kiwanda cha juisi kitakachosaidia wakulima wa
mananasi kuwa na soko la uhakika badala ya kwenda Geita mjini au Mwanza.
“Tukijenga
kiwanda hapa, tutatoa ajira kwa vijana na tutatengeneza juisi yetu
badala ya kila siku kuagiza kutoka nje ya nchi, hii ni aibu,” alisema.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni