MAGAIDI WALITESA TAIFA ,WAFANYA UNYAMA MKOANI MOROGORO,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
Mmoja wa majeruhi wa bomu lililorushwa kwa mkono katika Kijiji cha Msolwa wilayani Kilombero jana akiwa Hospitali ya Mt Kizito iliyopo Mikumi mkoani Morogoro. Picha na Liliani Lucas |
Morogoro. Tishio la ugaidi limezidi kuwa tete
baada ya watu wanaoshukiwa kufanya vitendo hivyo kulipua bomu na kusababisha
watu watano kujeruhiwa wakati wakitoka kwenye maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi katika Kijiji cha Msolwa Ujamaa, kilichoko Kata ya Sanje wilayani
Kilombero.
Hili ni tukio la pili kutokea kwenye Wilaya ya Kilombero mkoani
Morogoro baada ya watu tisa kukamatwa kwenye Msikiti wa Suni wakiwa na silaha
na vifaa vingine vinavyohusishwa na harakati za kigaidi.
Mbali na matukio hayo ya Morogoro, hivi karibuni vikosi vya
ulinzi na usalama vilipambana vikali na watu wanaoshukiwa kuwa ni magaidi
kwenye mapango ya kihistoria ya Amboni mkoani Tanga. Hadi sasa polisi haijatoa
taarifa ya kina kuhusu tukio hilo lililopoteza maisha ya mwanajeshi mmoja.
Kamanda wa polisi mkoani Morogoro hakuweza kupatikana
kuzungumzia suala hilo, wakati msemaji wa Jeshi la Polisi alisema tukio hilo
liko ndani ya mipaka ya mkoa hivyo linatakiwa lizungumzwe na mamlaka hiyo
badala ya makao makuu ya chombo hicho cha dola.
Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea walieleza kuwa bomu hilo
lilirushwa kuelekea kwenye gari la mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilombero saa 2:00 usiku. Bomu hilo lilirushwa na watu wawili ambao awali
walidhibitiwa na wananchi baada ya kuwashuku kuwa siyo raia wema.
Baada ya kuwatilia shaka, wananchi waliwaweka watu hao chini ya
ulinzi na wakati wakiwapekua, walitoa bomu na kulirusha kwenye gari hilo
lililokuwa limeegeshwa na kujeruhi watu watano, akiwamo dereva.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, David Ligazio aliwataja
waliojeruhiwa katika tuko hilo kuwa ni Novatus Ngapi, ambaye ni dereva na
Thomas Manjole, ambaye ni mgambo na hali yake inadaiwa kuwa siyo nzuri.
Wengine waliojeruhiwa ni Amos Msopole, Azama Naniyunya, ambao
wamelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi wilayani Kilosa
na Anna Pius ambaye amepata majeraha kidogo na kuruhusiwa.
Ligazio, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo,
alisema baada ya kumaliza kuhutubia alikuwa akizungumza na wananchi huku
akielekea kwenye gari na ndipo aliposikia kishindo kikubwa na kuona vioo vya
gari yake vikivunjika na watu kadhaa kujeruhiwa.
Ofisa mtendaji wa Kata ya Sanje, Hawa Ndachuwa alisema siku ya
tukio watu wawili walikodi pikipiki kutoka Kata ya Kidatu na kuomba
wapelekwe Kata ya Mkula na walipofika Msolwa Ujamaa, dereva wa bodaboda
aliwatilia shaka na kujifanya anawaomba wamuongezee fedha za malipo kwani
walipatana kiasi kidogo mwanzoni wakati safari ilikuwa ya mbali.
Ndachuwa alisema ilibidi watu hao wakubali kumuongezea fedha na
walimwambia watafute sehemu ya kutolea fedha na yeye akawapeleka eneo la
kutolea fedha. Alisema wakati watu hao wakihangaika kutoa fedha, mwendesha
bodaboda huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji ambao waliwasiliana na
polisi kwa ajili ya kuwafuata na kuwapekua watuhumiwa hao.
Alisema baada ya watu hao kuwa katika mabishano, wananchi
walipatwa na mshtuko kutokana na mavazi waliyovaa na kisha kuwaweka chini ya
ulinzi na kuanza kuwapekua.
Upekuzi huo ulifanyika chini ya usimamizi wa mgambo wa kijiji
ambao walifika baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa watuhumiwa hao.
Mtendaji huyo alisema kuwa wakati wanaendelea kuwapekua,
mtuhumiwa mmoja alikutwa na viberiti vya gesi na wakati upekuzi ukiendelea,
mtuhumiwa mwingine alikataa kutoa ushirikiano na wananchi walizidi kumtilia
shaka baada ya kuona kuwa ana kitu kakihifadhi kwenye mifuko ya suruali yake.
Alisema wakati wanaendelea kuwapekua, mtuhumiwa wa kwanza
alifanikiwa kukimbia na wakati wanajiandaa kumkamata, wa pili alitoa kitu kama
bomu na kurusha lilipo gari la mwenyekiti na ukatokea mlipuko mkubwa. Wakati
wananchi wakikimbia huku na kule mtuhumiwa huyo naye aliwatoroka na kukimbilia
kusikojulikana.
Ndachuwa alisema katika mlipuko huo mgambo huyo alivunjika mguu
na mkono, huku dereva wa mwenyekiti akiumia begani na wote wanne kuchukuliwa na
kupelekwa katika kituo cha afya Nyandeo na baada kuhamishwa Hospitali ya
Mtakatifu Kizito iliyopo tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa kwa ajili ya
matibabu.
Hata hivyo, mtendaji huyo wa kata alisema kuwa polisi
walifika eneo la tukio na kuahidi kulitaarifu Jeshi la Wananchi ambalo lina
wataalamu wa mabomu kwa ajili ya uchunguzi. Alisema juhudi za kuwasaka
watuhumiwa hao pia zinaendelea baada ya kutokea taarifa kuwa wamekimbilia kwenye
Milima ya Uduzungwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Lephy Gembe alithibiti kutokea kwa
tukio hilo.
Akizungumza kwa simu jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mtakatifu
Kizito, Maximiliam Mwenda alisema wamepokea majeruhi wanne ambao hadi sasa
wanapatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri, huku hali ya Thomas Manjole
ikiwa siyo ya kuridhisha.
Katika tukio la Aprili 14 lililohusishwa na ugaidi, mtu mmoja
alichomwa moto na wananchi wenye hasira akiwa na risasi sita tano za bunduki
aina ya SMG na moja ya mark iv pamoja na ‘detonators fuse’ mbili zikiwa katika
mfuko mdogo wa jeshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo hakuweza
kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Chanzo ni Gazeti la mwananchi
Post Comment
No comments
Post a Comment