HABARI KUBWA LEO,WIZI WA ESRCOW,WABUNGE WAIBAMIZA IKULU YA KIKWETE,NI KUWASAFISHA WEZI ,SOMA HAPA KUJUA
![]() |
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba akihojiwa na moja ya kituo cha radio |
KASHFA ya uchotwaji fedha za Umma katika
Akaunti ya Tegeta Escrow Sh. 306 bilioni, iliyofunguliwa kwenye Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) bado haijazimika, licha ya Serikali kujaribu kuwasafisha baadhi
ya watuhumiwa ikidai hawahusiki. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter
Serukamba (CCM) ndiye ameifufua bungeni akisema, kitendo hatua ya Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuwasafisha baadhi ya watuhumiwa wa kashfa hiyo
ni ubaguzi na usanii usikubalika.
Wiki iliyopita,
Ikulu ilitangaza kuwasafisha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliachim Maswi na waziri wake, Prof. Sospeter Muhongo kwamba tume
iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yao, haikuwakuta na hatia katika suala la
miamala ya fedha za Escrow.
Pia, Ikulu
kupitia kwa Balozi Sefue, iliwasafisha mawaziri watatu waliojiuzulu kwa
shinikizo la Bunge katika kashfa ya oparesheni tokomeza, ikisema licha ya
wananchi kupoteza maisha, kuteswa na mifugo kuuawa na askari waliotekeleza
oparesheni hiyo, lakini viongozi hao hawakuhusika moja kwa moja.
Mawaziri hao ni
Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na
Utalii) na Dk. Mathayo David (Mifugo na Uvuvi).
Ikumbukwe kuwa sakata la escrow liliibuliwa bungeni na mbunge wa
Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na baada ya ukaguzi wa Mdhibiti na
Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) kufanyika, ilithibitika kwamba miamala hiyo
ilifanyika kinyume cha sheria huku baadhi ya viongozi wakiwa wamenufaika na
mgawo wa fedha hizo.
Akichangia
hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa
fedha 2015/16, katika eneo la utawala bora, Serukamba amesema “hii staili
inayojaribu kutumika ni ya kizamani ya kusafisha watu kiani, imepitwa na
wakati”.
Huku
akisikilizwa na kushangiliwa na wabunge wengi, Serukamba amesema “kama Balozi
Sefue anasema Maswi na mawaziri hao ni safi, basi atwambie Andrew Chenge
(Bariadi Magharibi), Prof. Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), William Ngeleja
(Geita), uchafu wao ni upi wakati walipata mgawo halali?
Change,
Ngeleja na Victor Mwambalaswa (Lupa), walivuliwa uenyekiti wa kamati za Bunge
baada ya kuthibitika kuwa walipokea mgawo wa fedha hizo kutoka kwa mmoja wa
wamiliki wa IPTL, James Rugemalira bila kutangaza maslahi kama sheria ya
maadili ya viongozi wa umma inavyotaka.
Katika mtiririko huo, mawaziri Tibaijuka, Muhongo na aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema walijiuzulu kutokana na kashfa hiyo huku
baadhi ya watendaji katika mamlaka mbalimbali za serikali wakifikishwa
mahakamani na kwenye Baraza la Sekretarieti ya Viongozi wa Umma.
Akizungumza kwa masikitiko kuhusu uamuzi huo wa Ikulu, Serukamba
alishauri kuwa, “Chenge, Ngeleja, Werema, Mwambalaswa na mawaziri wengine
waliowahi kujiuzulu kama sehemu ya uwajibikaji nao wasafishwe na kurudishwa
katika nafasi zao.”
“Bunge hapa tuliomba ripoti ya oparesheni tokomeza lakini
haijawahi kuletwa ila anajitokeza katibu mkuu kiongozi kusafisha baadhi ya
watu. Huu ni usanii wa kuwasaidia watu wachache na kuumiza wengine kwa malengo
binafsi. Hatuwezi kuwa na serikali yenye “double standards”.
“Lazima wakina Chenge, Tibaijuka na wengine wote mawaziri
waliojiuzulu huko nyuma kwa kashfa ya Richmond nao waundiwe tume wasafishwe
kama wakina Maswi, vinginevyo mna ajenda binafsi ya kujisafisha,” amesema.
Serukama ameongeza kuwa, wako watumishi wa Ikulu wenye tuhuma za
escrow lakini bado wanaendelea kubaki kazini huku watumishi wengine wa umma
katika taasisi zingine wakifikishwa mahakamani kwa jambo hilohilo na hivyo
kuhoji hii ni serikali gani yenye ubaguzi wa aina hiyo?
“Kama ni kuunda Judicial Inquiry (Tume ya kimahakama), basi
ifanyike kwa watuhumiwa wote. Hiki si Chama Cha Mapinduzi tunachokijua. Sasa
kinachofuata hata hao mliowapeleka mahakamani kwa suala hilo watawashinda
kutokana na uamuzi huu wa kusafisha baadhi ya watu.
“Katibu Mkuu Kiongozi anasema hiyo ripoti ya tokomeza hawezi
kuileta bungeni badala yake anaisoma nusu nusu na kuwasafisha baadhi ya watu.
Huu ni ubaguzi na labda tuambiwe kuna watu mnaowalenga lakini haitawezekana,”
alisisitiza Serukamba
Chanzo ni Mwanahalisioline
No comments
Post a Comment