DK MENGI AIKABA KOO TENA IKULU YA KIKWETE,NI KUHUSU ZITTO KABWE,SOMA HAPO KUJUA
![]() |
Pichani ni Dk Mengi picha na Ma |
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, ameeleza
kusikitishwa dhidi ya majibu yaliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais
Ikulu kuhusu taarifa za kamchafua zilizochapishwa na gazeti la Taifa Imara
Machi 20, mwaka huu.
Dk. Mengi, alisema jana kuwa majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi
wa Kurugenzi hiyo, Salva Rweyemamu, siyo ya busara kwani yanapuuza usalama wa
maisha yake.
“Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu
jambo ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye,” alisema Dk. Mengi
na kuongeza:
“Ukiangalia, ukisoma kiundani majibu ya barua ya Rweyemamu, nina
kila sababu ya kuhofia usalama wa maisha yangu. Shughuli zake Ikulu ni za
kuheshimiwa, lakini awe na busara katika shughuli zake….kunishauri eti niende
polisi kuhusu suala hilo ni kama kunifanya nionekane sina busara kama yeye.”
Alisema uhai wa mtu siyo jambo dogo wala siyo la kupuuzwa na
kwamba busara ilihitajika katika kushughulikia suala hilo, lakini haikuwa hivyo
kwani majibu hayo yamesababisha tatizo hilo dhidi ya usalama wa maisha yake
kuwa pale pale.
Machi 23, mwaka huu, gazeti la Taifa Imara, lilichapisha habari
iliyoeleza kuwa, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alimchongea Dk.
Mengi kwa Rais Kikwete, kwamba ndiye kinara wa kuihujumu serikali yake na
alikuwa anamshawishi Zitto kujiunga na mipango hiyo.
Habari hiyo iliendelea kudai kuwa, Dk. Mengi aliapa
kumshughulikia Rais Kikwete kwa nguvu zake zote amalizapo muda wake wa urais
huku Rais Kikwete naye akiapa kupambana na yeye (Dk. Mengi).
Aprili 17 mwaka huu, katika mkutano wake na waandishi wa habari,
Dk. Mengi alisema, tuhuma hizo dhidi yake zilimshtua sana na kumpa hofu
kubwa kwa usalama wa maisha yake hivyo kuilaumu kurugenzi ya mawasiliano Ikulu
na Idara ya Habari (Maelezo) kwa kukaa kimya zaidi ya wiki tatu bila
kutoa ufafanuzi wowote kuhusu habari hiyo ambayo pia inamhusu Rais na kuiacha
kusambaa.
“Nilitoa kauli kwamba, tuhuma hizo dhidi yangu zilinishtua sana
na kwamba tamko la Mheshimiwa Rais kwamba atapambana nami lilinipa hofu kubwa
kuhusu usalama wa maisha yangu,” alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema majibu yaliyotolewa na kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais Ikulu, yalieleza kuwa Rais hakuwahi kuwa na mawasiliano na
Zitto Kabwe kama ilivyoelezwa na kwamba haikufanya lolote kutokana na kubanwa
na majukumu, hivyo kupuuza habari hizo kwa kuziona ni ndogo na za upuuzi.
“Salva hakufanya lolote eti kutokana na kuwa na majukumu mengi
na alipuuza habari hizo kwa sababu aliziona ni jambo dogo na upuuzi,”
alifafanua Dk. Mengi na kuongeza:
“Bwana Rweyemamu alisema pia kwamba alinishangaa kwa kutokutoa
taarifa katika kituo chochote cha Polisi kuhusu hofu ya usalama wa maisha
yangu. Majibu haya ya Salva yanaongeza hofu ya usalama wa maisha yangu, jambo
ambalo siyo dogo na la kupuuzwa kama anavyoona yeye.”
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni