WAZIRI NYALANDU AZIDI KUIMALIZA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII,SASA ANASHIRIKIANA NA MAKADA WA CCM KUIMALIZA WIZARA HIYO SOMA HAPA UONE JINSI NYALANDU ANAVYOIMALIZA NCHI
WINGU la ufisadi, rushwa na upendeleo limetanda tena katika Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya watendaji wake kudaiwa kugawa vibali vya kupasua mbao katika msitu wa serikali Sao Hill uliopo wilayani Mufindi Mkoani Iringa kwa watu wasio na sifa.
Taarifa zilizokusanywa na Raia Mwema
kwa wiki mbili sasa kutoka vyanzo mbalimbali zinabainisha kuwa vibali vya
kupasua mbao kwa mwaka huu 2014-15 vimetolewa kwa upendeleo huku rushwa
ikitawala mchakato mzima wa zoezi hilo.
Wanaotuhumiwa kwa ufisadi huo
ni pamoja na kamati ya ugawaji yamsitu ambayo inawahusisha menejimenti ya Sao
Hill, Maafisa wa Idara ya Misitu katika Wizara ya Maliasili na Utalii na Naibu
Waziri wa Wizara hiyo Mahmoud Mgimwa.
Kwa kawaida vibali hutolewa kwa
wafanyabiashara wenye sifa muhimu, kama kuwa na leseni ya biashara ya mbao na
pia mashine za kupasua mbao za viwango vya juu (kiwanda) za kati na
wajasiriamali wadogo.
Hata hivyo, kinyume cha utaratibu
huo katika utoaji vibali kwa mwaka huu inadaiwa kuwa idadi kubwa ya majina ya
watu na taasisi zilizopewa vibali ni ya watu wasiofanya biashara hiyo kabisa
wakiwemo wanafunzi.
Orodha ya waliopewa vibali
Katika uchunguzi wake Raia Mwema
imebaini kuwa katika orodha iliyotolewa na Kamati ya Ugawaji kuna majina mengi
ya vigogo na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa na
wafanyabiashara ambao ni ndugu na marafiki wa karibu wa viongozi hao.
Orodha hiyo pia ina majina ya
mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini na chama cha Wandishi wa Habari
Mkoa wa Iringa ambavyo kimsingi hazifanyi biashara ya mbao.
Katika orodha hiyo (nakala tunayo) pia
wamo watu wanaodaiwa kuwa majirani, na ndugu wa karibu wa Naibu Waziri Mgimwa
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini (CCM).
Kutajwa kwa Naibu Waziri
huyo kumechochea zaidi madai ya kuwapo kwa ufisadi katika zoezi hilo hasa
ikizingatiwa kuwa yeye ni Mbunge wa eneo hilo na pia ni Waziri
anayehusika moja kwa moja na Wizara inayosimamia msitu huo.
Viongozi wa CCM wanaotajwa kupewa
hekta za uvunaji miti ni pamoja na Spika wa Bunge la Tanzania Anne Makinda
kupitia kampuni yake ya Makinda One to One Co.Ltd ambayo imepewa mita za ujazo
450 kuvuna miti aina ya misindano.
Orodha hiyo pia inamhusisha
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Deo Sanga (Jah People) ambaye pia ni
Mbunge wa Makambako ambaye kampuni yake ya Jah People Transport Ltd
imemegewa mita za ujazo 200 huku yeye binafsi pia akipewe mita nyingine za
ujazo 200.
Aidha, orodha hiyo ya vigogo wa
CCM pia inamhusisha Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi
Chana, kupitia kampuni ya Pindi Chana Garage iliyogawiwa mita 200 za ujazo huku
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mufindi Yasin Daud Mlowe, kuptia kampuni tatu
tofauti akipatiwa jumla ya mita za ujazo 600.
Mjumbe wa CCM (Mkutano Mkuu) Mkoa
wa Iringa, Godfrey Mosha amemegewa vitalu viwili kupitia kampuni zake za
Mufindi Wood Plantation & Industries na Mufindi Environmental Trust
(MUET) jumla ya mita za ujazo 400.
Orodha hiyo pia inaoonyesha kuwa
mke wa Mosha ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Wilaya ya
Mufindi Marselina M. Mkini amepewa mita za ujazo 200 na Mariam Angetile
Hidda ambaye anatajwa kuwa ni Mke wa Mkurugenzi Jiji la
Mwanza Khalifa Hidda.
Majina mengine ambayo yanatiliwa
shaka kuwa hayakustahili kupewa vibali ni pamoja na Inocent Menrard Kigola
anayedaiwa kuwa mtoto wa Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini (mwanafunzi) ,
Halima Mahmoud Mgagula anayedaiwa kuwa mtoto wa Mgimwa na Evarist Mangala
ambaye aliwahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa.
Kuna pia watu wanaodaiwa
kuwa karibu na wakuu wa wilaya kadhaa za Mkoa wa Iringa, Wenyeviti wa
Halmashauri, Madiwani, Maafisa wa Polisi ngazi ya Mkoa na watumishi wa juu wa
idara nyingine nyeti za serikali.
“Hawa ni viongozi wa CCM na serikali
na wengi wao hawana hata leseni ya biashara ya mbao wala hawana sifa ya kupewa
vitalu vya miti, hivyo kilichofanywa na kamati ya ugawaji ni ukiukwaji mkubwa
sheria na taratibu,” alieleza mtoa taarifa wetu.
Taarifa zinabainisha kuwa mmoja wa
wafanyabiashara maarufu wilayani Mufindi, Hezron Ng’umbi, ambaye anadaiwa kuwa
na uhusiano wa karibu na Naibu Waziri Mgimwa amemegewa vitalu zaidi ya vitano
kupitia kampuni zake na ndugu zake wa karibu.
Kampuni zinadaiwa kuhusishwa na
mfanyabiashara huyo ni pamoja na C.F Investiment Co.Ltd., Mtili G. Enterprises,
Mtili Sawmill & Timber, Ng’umbi Services &Timber, Sitex
Enterprises, CFN Enterprises na West Solution Ltd.
Katika orodha hiyo pia inawahusisha
ndugu wa karibu wa mfanyabiashara huyo ambaye ni pamoja na Chesco Fransis
Ng’umbi, Christian Fransis Ng’umbi, Agness Elias Mwagala, Rehema Yeriko Mwagala
na Stewart F. Ng’umbi.
“Majina hayo yote ni yanahusishwa na
huyo mfanyabiashara Hezron Ng’umbi ambaye kwa njia ambazo tunadhani si halali
amepewa vitalu vya kuvuna miti zaidi ya vitalu saba kinyume cha utaratibu kuwa
kila mwombaji atapatiwa kitalu kimoja,” kilieleza chanzo chetu.
Aidha uchambuzi wa majina hayo
unaonyesha kuna majina 31 yanayodaiwa kuwa ni ya watu wenye maslahi ya moja kwa
moja na Naibu Waziri Mgimwa na inadaiwa kuwa wamepewa vibali kwa ushawishi
wake.
Jinsi biashara inavyofanyika
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa baada
ya wahusika kupewa vibali hivyo, huviuza kwa wafanyabiashara wakubwa wa mbao
kwa bei kati ya shilingi milioni 7-13 kulingana na mapatano na hivyo kupata
faida bila kuwekeza chochote.
Wandishi wa habari wa gazeti hili
walifanya mazungumzo na baadhi ya wafanyabiashara wa mbao mjini Mufindi ambao
walikuwa katika harakati za kutafuta wadau wenye vibali ili wavinunue kwa
ajili ya viwanda vyao.
“Kama una kibali hakuna shida.
Tuna fedha za kutosha na nitakulipa kupitia benki au hata fedha taslimu,
ukitaka hakuna tatizo,” alisema mfanyabiashara mmoja huku akiwa amezungukwa na
madalali wanaomtafutia vibali vya kununua.
Uchunguzi zaidi
unaonyesha ya kuwa wengi wa watu waliopata vibali wametumia ushawishi wa nafasi
zao za uongozi pamoja na baadhi wakitumia njia za rushwa.
Akizungumza na Raia Mwema mmoja
wa wadau wa biashara ya mbao George Kavenuke ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano
Mkuu CCM, Mkoa wa Iringa, alieleza kuwa kilichofanyika na Kamati ya Ugawaji na
Wizara ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wananchi wa Mufindi.
“Ugawaji huu ni batili. Vibali
vimetolewa bila kuzingatia vigezo. Kuna wajasiriamali wenye mashine za kupasua
mbao ambao wamewekeza fedha zao hawajapewa vipaumbele katika ugawaji jambo
ambalo si haki kabisa,” alisema Kavenuka.
“Kwa msingi huo tunamtaka Waziri
mhusika (Maliasili na Utalii) Lazaro Nyalandu kufuta haraka vibali vyote ili
utaratibu ufanyike upya na waliohusika na uzembe huu wachukuliwe hatua,”
alisema Kavenuka.
Mfanyabiashara mwingine William
Mgowole alieleza kuwa hatua ya kunyimwa vibali pamoja na kwamba wana sifa na
wameifanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 35 ni kuwanyima haki wananchi wa Wilaya
Mufindi.
“Binafsi nimeifanya kazi hii kwa zaidi
ya miaka 30 nimewekeza nguvu, fedha na rasilimali zangu nyingi, ghafla leo
naambiwa kwamba sina sifa ya kupewa kitalu cha kuvuna miti, lakini wakati huo
kuna watu wamepwa vibali zaidi ya kimoja bila kuwa na sifa na
badala yake wanafanya ulanguzi jambo hili halikubaliki,” alisema Mgowole.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inaathari
kubwa kwa maisha na uchumi wa wananchi wengi wa wilaya hiyo ambao
wanategemea biashara hiyo kama njia ya kujikumu kimaisha na itawandoa katika
ajira watu zaidi ya 2000 ambao walikuwa wameajiriwa katika viwanda vya kati.
Majibu ya wanaotuhumiwa
Akizunguzia madai hayo Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii Mahmoud Mgimwa aliliambia Raia Mwema kuwa taarifa hizo
ni uzushi mtupu na hahusiki kwa namna yoyote katika ugawaji wa vitalu vya miti
ya kupasua mbao.
“Mimi kama Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii sihusiki kwa njia yoyote na ugawaji wa vitalu, kuna
Wakala wa Misitu (TFS) pamoja na menejimenti ya mashamba
ya Sao Hill. Majukumu ya ugawaji yameachwa mikononi mwao,” alisema.
“Madai yanayoenezwa yamelenga
kunichafua kisiasa hasa ukizingatia kuwa mwakani tunafanya uchaguzi. Kuna watu
wameanza kupitapita kuwalaghai wananchi na moja ya turufu zao ni kunichafua
kupitia habari za ugawaji wa vitalu vya miti,”alisema Mgimwa.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba
hilo Saleh Beleko alikiri kuwapo malalamiko katika ugawaji lakini akatuma
lawama kwa TFS ambao ndio waliohusika kutoa orodha ya mwisho ya
waliofanikiwa kupata vibali.
“Sisi kama menejimenti ya shamba
kazi yetu ni kupokea maombi ya watu wote na tukishapokea tunapeleka Dar es
Salaam kwa TFS ambao hutuletea orodha ya walioidhinishwa na kazi
yetu ni kuitangaza,” alisema Beleko.
Juhudi za kumpata Mtendaji Mkuu wa
TFS, Juma Mgowo, hazikuweza kufanikiwa kama ambavyo waandishi walivyoshindwa
kuwapata, hadi tukienda mitamboni, Spika Makinda, Chana, Sanga na wengine
wanaotajwa kwenye nyaraka za mgao huo wa vitalu vya mbao.
Kwa upande wake mfanyabiasha
Hezron Ng’umbi ambaye anatuhumiwa kutumia ukwasi wake kujilimbikizia
vitalu alikanusha madai hayo na kuongeza kuwa hata yeye ni mhanga wa ugawaji
uliofanyika.
“Makampuni na majina
yanayohusishwa na mimi siyafahamu, nimepewa mita za ujazo 450 kwa jina
langu la Chesco Fransis. Kiasi hiki ni kidogo sana. Nitavuna kwa wiki
mbili baada ya hapo inabidi nifunge kiwanda kwa sababu nitakuwa sina
malighafi,” alisema.
Aliongeza kuwa kiwanda chake
kimeajiri zaidi ya watu 60, ambao hata ajira yao itakoma baada ya kumaliza
kupasua mbao katika eneo alililopewa na kusisitiza kuwa ugawaji wa
msitu huo kwa mwaka huu umekiuka taratibu.
Chanzo ni Gazeti la Raia Mwema
No comments
Post a Comment