Zinazobamba

Operesheni ya jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram


Operesheni ya jeshi la Nigeria dhidi ya Boko Haram
Operesheni ya jeshi la Nigeria katika jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika imepelekea maelfu ya raia kuwa wakimbizi. Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limeanzisha operesheni kabambe katika maeneo ya Borno kwa minajili ya kulisafisha eneo hilo na wapiganaji wanaofungamana na Boko Haram. 

Inaonekana kuwa, udhaifu na kutokuwa na ubavu jeshi wa kupambana na Boko Haram ni mambo ambayo yanatajwa na weledi wa mambo kuwa, yamechangia kuzorota zaidi usalama wa jimbo la Borno. Katika masiku ya hivi karibuni maelfu ya wakazi wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wamelazimika kugura na kukimbilia katika mikoa ya jirani au katika maeneo ya mpakani na Cameroon wakisalimisha roho kutokana na usalama wa maeneo yao kuharibika kabisa.

Inaelezwa kuwa, wakimbizi hao wanakabiliwa na matatizo chungu nzima. Ripoti zinaonesha kuwa, hadi sasa jeshi la Nigeria limeshindwa kuyakomboa maeneo mengi yanayodhibitiwa na Boko Haram au hata raia waliotekwa nyara na wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi. Mashambulio ya Boko Haram katika vijiji vya kaskazini masdhariki mwa Nigeria yamesababisha mamia ya watu kuuawa na wanawake na watoto wengi kuchukuliwa mateka.

 Ripoti zinaonesha kuwa, shambulio dhidi ya makanisa mawili, kuchomwa moto vituo vya polisi na majengo ya serikali ni sehemu nyingine ya jinai za wanamgambo wa Boko Haram huko Nigeria. Kushadidi kwa harakati za Boko Haram kumezifanya nchi jirani na nchi hiyo kama Cameroon kuingiwa na wasi wasi wa kukabiliwa na mashambulio ya kundi hilo la kigaidi. Licha ya kuwa jeshi la Cameroon limejiweka tayari kukabiliana na mashambulio tarajiwa ya Boko Haram, lakini viongozi na wananchi wa nchi hiyo wameingiwa na wasi wasi mkubwa juu ya kutokea mashambulio hayo. Kukosekana udhibiti wa kutosha wa mipakani ni moja ya mambo yaliyorahisisha kutoka na kuingia katika nchi nyingine wapiganaji wa Boko Haram. 

Weledi wa mambo wanautaja uwezo wa kifedha na kisilaha wa Boko Haram kuwa, sababu nyingine ya kuendelea kupanuka harakati zake. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, kundi la Boko Haram limekuwa likipata misaada ya fedha na silaha kutoka kwa nchi za Magharibi na liko katika mkondo wa kutekeleza siasa za kikoloni za nchi hizo huko Nigeria.


 Hii ni katika hali ambayo, kundi jingine la wajuzi wa mambo linaamini kuwa, kundi la Boko Haram linategemea misaada ya ndani na lina uhusiano wa kifedha wa kiwango fulani na makundi mengine yenye kuchupa mipaka. Katika upande mwingine himaya ya kifedha ya kundi la al-Qaeda kwa Boko Haram ni ndogo ikilinganishwa na fedha inazozipata kundi hilo kupitia vitendo vya utekekaji nyara na kudai vikomboleo. Katika upande mwingine, kudhoofika uchumi na ongezeko la ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana ni mambo ambayo yamerahisisha hatua za Boko Haram katika kuajiri wapiganaji na hivyo kujiongezea wanacham siku baada ya siku.

No comments