Zinazobamba

HUU NI UOGA AU RAIS KIKWETE ANAWAKOMOA CCM,SOMA HAPA KUJUA



http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2014/07/Jakaya-Kikwete1.jpg 
Pichani ni Rais Jakaya Kikwete

Na Edsoni Kamukara  
    KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imemaliza kikako chake
muhimu mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na
kuazimia mambo ya kitoto sana wakati huu ambapo hali ya nchi ni tete.

          CC imebariki Bunge la Katiba liendelee na vikao vyake licha ya
kutambua kwamba theluthi mbili ya kura ya uamuzi hasa upande wa
Zanzibar haipatikani.

           Katika maazimio yao hayo ambayo nadiriki kuyaita ya kitoto, CCM
inamtwisha zigo Katibu Mkuu wao, Abdulrahman Kinana, aendelee kusaka
             suluhu na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
lakini nyuma ya pazia Bunge likiendelea na wajumbe wao wakila posho za
wafuja jasho.

                Huu ni mzaha, ni dharau iliyopitiliza kwa wananchi, ni mchoko wa fikra


     na vile vile ni dalili za kuanguka kwa serikali ya CCM kwa sababu
viongozi makini katika nchi ambazo zinazingatia demokrasia ya
kuwatumikia wale waliowachagua, CC ndicho chombo kikuu cha juu
kinachomshauri Rais kuhusu nini kifanyike katika masuala nyeti ya
Taifa.



              Mchakato wa Katiba mpya umekwama mikononi mwa Bunge la Maalum la
Katiba. Rais Jakaya Kikwete ama kwa hofu ya chama chake au kwa
makusudi tu ya kuwaangusha wenye nia ya kuwania urais kupitia CCM,
ndiye alikuwa wa kwanza kuvuruga mjadala wa Bunge hilo wakati
akilihutubia na kulizindua.

            Hotuba yake ndiyo iliwageuza misimamo wajumbe wa CCM na washirika wao
na hivyo kuibuka na hoja ya kupinga mapendekezo ya wananchi katika
rasimu iliyokabidhiwa kwa Bunge Maalum na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, iliyoundwa na Rais Kikwete mwenyewe.

              Katika hotuba ile ya kulizindua Bunge, Rais Kikwete alisema kuwa
muundo wa serikali tatu unaopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba
hautekelezeki na kwamba labda uanze baada ya yeye kuwa ameondoka
madarakani.

                Ukiachilia mbali vitisho vingi alivyotoa vya kuwatia hofu wananchi
kwamba mfumo huo ukipita nchi itapinduliwa na jeshi, Rais Kikwete
aliweka bayana kwamba wao katika CCM msimamo wao ni serikali mbili
halafu eti anawataka wajumbe wajadiliane kwa kutumia akili zao
wakichanganya na za kuambiwa.

              Hii ilikuwa ni hotuba dhaifu sana na yenye kuchekesha kwa kiongozi
mkuu kama Rais wa nchi. Nasema ni dhaifu na yenye kuchekesha, kwani
haiwezekani kiongozi wetu ambaye ndiye dira yetu anaweka msimamo na
             kuapa kwamba mfumo unaopendekezwa utatekelezeka akiwa ameondoka
madarakani kisha tuendelee kujidanganya kwamba kuna Bunge linaendelea
kujadili rasimu.

             Biblia Takatifu inasema kuwa; ‘makwazo hayana budi kuja, lakini ole
wake mtu ambaye anasababisha makwazo hayo; kwa maana mtu huyo
anastahili kufungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini’.

               Kama utawala wa kikoloni ungerejeshwa leo halafu nikapata bahati ya
kuchagua adhabu ya kuwapa viongozi wakuu wa CCM, basi ningeomba
arudishwe Mjerumani ili awacharaze viboko hadharani kutokana na mizaha
yao katika maisha tete ya kero za wananchi.

            Nadhani hatuhitaji kwenda shule kusoma ili kutambua kwamba serikali ya
CCM haitaki Katiba mpya. Uthibitisho wa hili ni mizaha na michezo ya
rafu inayoendelea tangu kuanza kwa mchakato huo hadi sasa
nawanapofikia hatua ya kuhalalisha kodi za wananchi zitafunwe huku
wakijua hawawezi kukamilisha kuandika katiba hiyo bila uwepo wa kundi
la wajumbe wa UKAWA.

               Ni bahati mbaya sana, adhabu hiyo ninayoitamani haiwezi kutekelezeka
sasa kutokana na kinga ya haki za binadamu inayoendesha ulimwengu.

            Lakini nadhani wananchi wanapaswa kuanza kujipanga ili kuiadhibu CCM
kupitia sanduku la kura.

Nasema hili kwa mara ya tatu kwamba kama tungekuwa na wananchi jasiri,
               basi maandamano ya kushinikiza Bunge la Katiba lisitishwe yangekuwa
yanaendelea kwa amani kila kosa ikiwa ni pamoja na kuweka azimio kwa
wajumbe wa Bunge hilo kurejesha posho walizotafuna bila kukamilisha
kazi waliyopewa.

               Ninapotazama mchezo huu unaoendesha na CCM, najikuta nikibakia na
maswali mawili makubwa ya kama tumekwama kutokana na uoga wa Rais
Kikwete kwa chama chake au ni mkakati wa kuwakomoa wagombea urais
wajao ndani ya CCM?

              Hata hivyo, kila ninapotafakari kwa upana hoja ya uoga, naona kama
haina mashiko kwa sababu zifuatazo. Mosi, Rais ni amiri jeshi mkuu wa
vikosi vya ulinzi na usalama. Huu anayo mamlaka yote, hivyo hawezi
kumwogopa mtu.

               Lakini nikijaribu kwenda mbali naona huu kama umekuwa utaratibu wa
Rais Kikwete kukwepa lawama kwa marafiki zake na ndiyo maana
ameshindwa kutoa msimamo dhabiti kwa masuala nyeti ya nchi na hivyo
kuacha mpasuko mkubwa.

          Pia hili la uoga linakosa zaidi mashiko hasa ikizingatiwa kwamba Rais
Kikwete haogombei tena, hivyo hana hofu ya kukosa kura. Sasa swali
linabakia ni kwanini ameanzisha mchakato kisha kauvuruga mwenyewe?

              Pili, ukijiegemeza kwenye hoja ya kukomoana ndani ya CCM. Unaweza
ukashawishika haraka kwamba pengine ndio maana Rais Kikwete ameamua
kuwa kimya kwamba watabebeshwa msalaba watakaojitokeza kuomba urais
kupitia CCM.

              Kwa sababu wakati huo, yeye hatakuwa mgombea, hivyo ahadi zake zote
alizoshindwa kutekeleza pamoja na mkwamo wa katiba mpya ambayo
mchakato wake umetumia mabilioni ya shilingi wataulizwa wale
watakaogombea kwa CCM.

             Hii maana yake nini? Rais alianzisha mchakato wa katiba mpya kwa lengo
gani ikiwa alifahamu kwamba CCM wanamzidi nguvu? Kwanini amekubali
kodi za wafuka jasho ziendelee kuchezewa kwa jambo ambalo halitafika
mwisho? Hii ndiyo siasa safi na uongozi bora aliyoridhi kwa Nyerere?

Tafakari

No comments