EXCLUSIVE---NANI ANAFAA KUMRITHI HECHE BAVICHA?SOMA HAPA KUJUA ZAIDI
![]() |
| Pichani ni Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe picha na Maktaba |
Na Edson Kamukara
NIKIWA kijana ninayeamini katika siasa za mabadiliko, najiona nina
wajibu na kila sababu ya kutoa maoni na ushauri wangu kwa viongozi wa Baraza la
Vijana Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), unaomaliza muda
wake ili wahakikishe wanapata warithi makini.
Swali hili na nani anafaa
kumrithi Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, kwa leo nitalijibu kwa kutaja sifa
za mtu anayehitajika kuliongoza baraza hilo nyeti ambalo naweza kulifananisha
kama nguzo mhimu ndani ya CHADEMA.
Ila katika makala yangu ijayo,
nitawataja moja kwa moja wagombea hao kwa majina ili kutoa mwangaza kwa
wajumbe, wapime kama wanazo sifa za kuitoa BAVICHA hapa ilipo na kuisogeza
katika hatua nyingine ya kuwawezesha vijana kuikomboa nchi yao mikononi mwa mafisadi.
Ninapomtaja Heche, sina shaka kwamba
ni kiongozi ambaye amejijengea umaarufu wa kutosha kwa kipindi alichoiongoza
BAVICHA kama mwenyekiti aliyerithi mikoba ya mtangulizi wake John Mnyika.
Nimemfahamu Heche kwa miaka kadhaa
tukiwa pamoja katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Mwanza (SAUT). Huyu
tumekutana na kufahamiana katika siasa kupitia tawi letu la chuo, nikiwa
mwenyekiti mwanzilishi wa tawi hilo.
Heche alijiunga SAUT mwaka mmoja
nyuma yangu, ingawa ilituchukua muda mfupi mimi na viongozi wenzagu kufahamiana
naye kutokana na ujasiri wake wa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala
ya CHADEMA.
Wakati tunafikia kipindi cha ukomo wa
uongozi wetu, Heche alikuwa ni mtu ambaye kila mmoja wetu alitamani arithi
nafasi mojawapo kati ya mwenyekiti au katibu wa chama.
Tamanio letu lilitimia tena katika
mazingira ya kushangaza kidogo kwa sababu Heche alishinda uchaguzi na kuwabwaga
wagombea wengine katika nafasi ya ukatibu bila kuwepo kujinadi kwa wapiga kura.
Hii ndiyo ilikuwa sababu yangu ya kwanza
kuamini uwezo wake na kukubalika kwake kwa wenzake, japo hakuma maarufu sana
bali wajumbe walithamini uwezo na ujasiri wake aliouonyesha wakati tukiwekewa
mizengwe na viongozi wa CCM tawi hadi mkoa kuhakikisha tawi letu halifunguliwi.
Hata aliponishirikisha kusudio
lake na kutaka kuwania uenyekiti wa BAVICHA Taifa, nilimpa matumaini kwa vile
niliamini ndiye mtu sahihi aliyepaswa kurithi mikoba ya Mnyika aliyekuwa
ameitumikia BAVICHA kwa mafanikio makubwa.
Nasema tena kwamba Heche
aliiongoza BAVICHA akiwa si maarufu lakini anaondoka akiwa amepata umaarufu
mkubwa kwa sababu alitumikia wadhifa huo akiwa na nia, malengo na madhumuni ya
kuieneza CHADEMA kupitia baraza hilo.
Heche hakugombea uenyekiti
kutafuta sifa ya kukuza umaarufu wa jina lake, hakutumia rushwa ili achaguliwe,
hakuwa na kundi nyuma yake lililomtanguliza ili alinde maslahi yake na kubwa
zaidi alikipenda CHADEMA kwa moyo wa dhati akiamini katika mabadiliko ya kuona
siku moja kikiwa chama tawala.
Si kusudio langu kumsifia Heche
katika makala haya, isipokuwa nilikuwa najenga msingi wa hoja yangu ili nipate
kueleweka ninapouliza ni nani anafaa kumrithi mwenyekiti huyu BAVICHA.
Ni kweli wamejitokeza vijana
wengi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za BAVICHA kila mmoja
kulingana na matamanio yake. Niseme nawapongeza wote ambao wameisha chukua fomu
hizo na kuzirudisha bila kujali kama wanatosha au hawatoshi kivigezo.
Kujitokeza kuchukua fomu ni
ushujaa, achilia mbali kwamba ni haki ya kikatiba. Sasa kazi ya kumpata mgombea
makini wa kuivusha CHADEMA hapa ilipo na kwenda mbali zaidi, itategemea mchujo
wataoufanya wakina Heche na wenzeke kisha majina hayo kuamuliwa kwa wajumbe wa
BAVICHA.
Iwapo mchujo wa wakaina Heche
utaegemea kwenye ushwahiba, rushwa, ubinafsi, kulindana, umaarufu, eneo
analotoka mgombea, dini, kabila na upuuzi mwingine, ni dhahiri watakuwa
wameiuza na kuizika rasmi BAVICHA.
Katika kuteua wagombea, husuasani
nafasi ya mwenyekiti na makamu wake, Heche na wenzake lazima wajikumbushe
usaliti wa akina Juliana Shonza, Habib Mchange, Mwampamba na wengineo, ambao
waliingia kwenye mchakato wakati huo kwa kulinda matakwa ya wafadhili wao
kisiasa na sio kukijenga CHADEMA.
Lazima watambue kuwa hata
kwenye kundi kubwa hili la vijana waliojitokeza kuomba kuwarithi, wengi wana
malengo yao binafsi wala hawako kwa ajili ya kukipigania CHADEMA kisonge mbele
kushika dola 2015.
Wajue kuwa humo wamo wanaotafuta umaarufu
wa kutangaza majina yao, wako wanaotumiwa na makundi ya kusaka madaraka lakini
mbaya zaidi wako waliopandikizwa kwa fedha chafu za wapinzani wao kisiasa ili
waingie kuwavujishia siri za CHADEMA.
Kwa hiyo, iwapo Heche na
wasaidizi wake watadanganyika na umaarufu wa mgombea, kuzunguka kwake mikoani
kwenye ziara za chama, kutoa matamko mengi alipokuwa chuoni, bila kuzingatia utiifu
wake, mapenzi mema kwa chama na uwezo wake binafsi katika kukieneza CHADEMA,
BAVICHA itakufa na wao waaibika.
Sio kazi ya Heche wala katibu
mkuu wake, Deogratius Munishi au kiongozi yoyote wa BAVICHA taifa, kujigeuza
mshauri nasaa wa kuwapigia ramri baadhi ya wagombea na kuwaelekeza wawanie
nafasi fulani. Kiongozi anaye wania nafasi ya kulazimishwa, kamwe hawezi
kuitumikia kwa dhati.
Huyu atababishwa, atarubuniwa,
atanunulika na huyo hawezi kuisongesha BAVICHA katika kuiongoza CHADEMA kutwaa
madaraka 2015.
Makala ijayo, nitawataja wagombea
ambao kwa upeo wangu nadhani wanaweza kuivusha BAVICHA endapo watapata ridhaaa
ya kuchaguliwa.
Kila la kheri Heche na wenzako
katika kupata warithi wenu.

No comments
Post a Comment