Zinazobamba

BINT ATOKA NDUKI BAADA YA KUOLEWA, MAUZAUZA YAMFANYA AKIMBIE NDOA


MAKUBWA! Mke wa mtu aliyejitambulisha kwa jina la Miinza Matoki (20), ameikimbia ndoa yake kisa kikielezwa kuwa ni mauzauza ya kichawi anayokutana nayo.


Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Minza ambaye ni mkazi wa Manyoni mkoani Singida alisema wazazi wake walimuozesha kwa ‘kibabu’ aliyemtaja kwa jina moja la Samson ambaye aliwahi kuoa wanawake nane kabla yake hivyo yeye kuwa wa tisa. 

Alisema siku chache baada ya kuolewa alianza kuona mauzauza usiku ambapo alidai alikuwa akichezewa mwilini na watu ambao hakuwafahamu wenye sura za kutisha huku wakiwa wamevaa nguo nyeupe. 


Mwanamke huyo alisema mchana alipokuwa akienda kuchunga ng’ombe akirudi nyumbani alikuta kinyesi cha binadamu kwenye begi la nguo zake.“Siku moja niliamshwa usiku saa kumi na kuambiwa niende kisimani kuchota maji, nikakutana na mtu aliyevaa nguo nyeupe, nikamsalimia hakuitika, nikachota maji na kuondoka, nilipotazama nyuma sikumuoana nikaanguka na kupoteza fahamu. 

“Nilijikuta nikiwa sehemu ambayo sikuifahamu, palikuwa na watu wengi waliovaa nguo nyeusi ambapo nilishikwa mkono na mtu ambaye nilikuwa namfahamu kwamba ni mtoto wa mjomba wangu, akanipandisha kwenye fisi huku nikiwa nimevalishwa nguo nyeusi na kufungwa hirizi mwilini, nikaamriwa nikamuue mama yangu na baada ya kupanda fisi tulienda kwa mama yangu, mtu niliyeongozana naye alikuwa na utaalamu wa kutosha. 

“Zoezi la kumuua mama lilishindikana ndipo nikaganda kwenye mlango na yule niliyeenda naye yeye aliondoka na kuniacha.
“Mama alipoamka asubuhi alinikuta mlangoni nikiwa sijielewi huku nimevaa nguo nyeusi ‘kaniki’ na kufungwa hirizi, alimwita mganga akanitoa pale na kuninywesha dawa lakini sikupona ndipo nikapelekwa kwa mchungaji kuombewa. 


“Baada ya hapo nilirudi kwa mume wangu na kuchukua nguo zangu na kutoroka ambapo niliomba lifti kwenye gari la mkaa na kushushwa Ubungo jijini Dar,” alisimulia mwanamke huyo huku akiapa kutorudi kwa mzee huyo ambaye hakupatikana kwani hana simu. 

Kwa sasa mwanamke huyo amehifadhiwa kwa Mwenyekiti Mtaa wa Shimo la Udongo, Kurasini kwa mama Felister Komba ambaye baada ya kufika kwake alimpeleka Kituo cha Polisi cha Kurasini na kufunguliwa faili la taarifa lenye namba KUR/340/2014.

Hakuna maoni