WANAWAKE WASHAURIWA KUACHA KUTUMIA SABUNI ZA KAISIKI KURUDISHA BIKRA ZAO KWANI ZINA MADHARA MAKUBWA
WANAWAKE wameshauriwa kuacha kutumia sabuni za kunawia sehemu za siri ambazo hudaiwa kurejesha ubikira kwani zina madhara makubwa ikiwemo kusababisha kansa ya shingo ya kizazi. Mkaguzi wa Dawa na Mfamasia wa Manispaa ya Dodoma Daria Mwanuka alisema hayo mwishoni mwa wiki katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi wakati wa uteketezaji dawa, vipodozi na vyakula visivyofaa kwa matumizi ya binadamu.
Kazi hiyo ilifanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Kati. Alisema kumekuwa na sabuni mbalimbali ikiwamo Kaisiki ambapo wanaoziuza wanadai zimekuwa zikisababisha bikira iliyopotea kurudi kitu ambacho si kweli.
“Sabuni
hizo zinapunguza tu majimaji yaliyo sehemu za siri za mwanamke jambo
ambalo husababisha wakati wa kufanya mapenzi mwanaume kupata ugumu
kwenye muingiliano kwa vile mwili unakuwa umekataliwa kutoa maji na
hivyo kuleta michubuko kitu ambacho ni hatari hasa wenye maambukizi ya
magonjwa,” alisema.
Alisema
michubuko inapotokea ni rahisi mwanamke kuambukizwa magonjwa ya zinaa
hata virusi vya Ukimwi. Mtaalamu huyo alisema sabuni hizo zinatengeneza
hali fulani ukeni lakini haiwezi kurejesha hali ya maumbile iliyopotea.
Alisema
wanaotumia sabuni hizo wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa
na hata kupata saratani ya shingo ya uzazi kwani kemikali zinazotumika
katika kutengeneza sabuni hizo zina athari kubwa kiafya.
Alisema
ni vyema wanawake wakatambua thamani yao na kuachana na matumizi ya
sabuni hizo ambazo hazina manufaa yoyote na badala yake zimekuwa na
madhara makubwa kwao.
Kwa
upande wake, Fredrick Luyangi , Mkaguzi wa dawa kutoka TFDA alisema
matumizi ya sabuni hizo huleta athari kubwa mwilini na wakati mwingine
kutengeneza kansa taratibu bila mhusika kufahamu.
Alisema
sabuni hizo husababisha kansa ya kizazi na kubainisha sabuni hizo licha
ya kupigwa marufuku zimekuwa zikiuzwa kwenye maduka ya vipodozi.
Alisema
mara nyingi kwenye operesheni zinazofanyika zimekuwa zikiondolewa
sokoni lakini hata hivyo zimekuwa zikiingizwa kwa wingi hali inayofanya
zoezi la kudhibiti kuwa gumu.
Alisema
ni muhimu kwa wanawake kuacha matumizi ya sabuni hizo ambazo zina
madhara makubwa sana kwao kwani zikikosa wanunuzi zitaondoka sokoni.
No comments
Post a Comment