JK ATOA YA MOYONI AWATAKA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA KUWEKA MASLAHI YA TAIFA MBELE, UBINAFSI NA CHUKI HAZINA NAFASI
Rais Jakaya Kikwete amewataka wajumbe watakaopata fursa ya
kuingia kwenye Bunge la Katiba kuweka mbele masilahi ya Taifa badala ya
makundi yao.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ripoti na
Rasimu ya Pili ya Mabadiliko ya Katiba jana, Rais Kikwete alisema
kuingiza hulka binafsi katika mchakato huo ni kuchelewesha upatikanaji
wa Katiba Mpya kwa muda uliopangwa.
Alisema alipofanya mazungumzo na vyama vya siasa
vya Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, aliwataka kuweka kando masilahi
ya vyama vyao na kutanguliza utaifa ili kupata Katiba yenye sura ya
taifa.
“Niliwaambia na leo (jana) narudia kuwa
watakapokuwa wakiijadili rasimu, watambue kuweka mbele masilahi ya
taifa, malengo ya vyama na asasi zao yawe ya pili. Kama hawatafanya
hivyo hatutapata Katiba,” alisema na kuongeza:
“Kama itashindikana kupata Katiba Mpya, hakutakuwa
na katiba ya mpito… hii tuliyonayo sasa itaendelea kutumika,
nawaelezeni na ikihitajika tena mchakato utatakiwa kuanza mwanzo na mimi
nitakuwa nimesshastaafu nipo kijijini Msoga (Chalinze, Pwani).”
Alisema Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
walitoka maeneo tofauti hivyo kutofautiana malengo, lakini kutokana na
uzito wa uundwaji wa Katiba, waliweka kando tofauti zao na ndiyo maana
rasimu waliyoiandaa ina sura ya kitaifa.
“Wajumbe wanatakiwa kuiga mfano wa Wajumbe wa Tume
ambao waliweka kando tofauti zao na leo hii wamekuja na rasimu iliyo na
sura ya kitaifa. Nanyi mnatakiwa kufanya vivyo hivyo,” alisema na
kuongeza:
“Mtambue pia kuwa hatima ya katiba iko mikononi
mwa wananchi, hivyo msifanye mnavyojua, isomeni rasimu kuanzia sura ya
kwanza hadi ya mwisho ili muweze kutoa maoni na mapendekezo kwa ufasaha
zaidi kuliko kuchagua maeneo ya kuchangia.”
Rais Kikwete alisema kukamilika kwa rasimu hiyo
kunatoa nafasi kwa mchakato wa kuwapata Wajumbe wa Bunge la Katiba ili
ifikapo Februari 11, mwakani Bunge hilo liwe limeanza.
No comments
Post a Comment