UHURU KENYATA ANAPOLILIA LUGHA YA KISWAHILI, ASEMA ANGEPENDA KITUMIKE KUWAUNGANISHA WANA AFRIKA MASHARIKI.
Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito Kiswahili kitumiwe kuleta umoja baina ya
wananchi wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu
awali. Picha/PPS
RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito Kiswahili kitumiwe kuleta umoja baina ya
wananchi wa mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akihotubia wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) waliokuwa katika
Bunge la Kitaifa Nairobi Jumanne, rais alisema utumizi wa Kiswahili
baina ya wananchi wa EAC ni njia mwafaka ya kudumisha utambulisho wa
pamoja ulio wa kipekee.
“Mungu ametupatia sauti inayoweza kuleta umoja baina ya wananchi wote
Afrika Mashariki, na tunafaa tuitumie ipasavyo kupitia vyombo tofauti
vya habari ili kutimiza utangamano,” alisema.
Hata hivyo, kinaya iliyodhihirika ni kuwa alitoa hotuba yake yote kwa
Kiingereza.
Rais Kenyatta alitoa hakikisho kuwa juhudi za kutimiza umoja kati ya
mataifa ya EAC ziko sambamba, ingawa hakuna usawa kati ya mataifa katika
utekelezaji wa mikakati ya kukamilisha juhudi hizo.(BMCL)
Alitoa wito kwa wabunge hao wajitahidi kupitisha sheria zitakazodumisha
umoja wa EAC, hasa zinazohusu uendelezaji wa biashara kati ya mataifa
husika.
Spika wa bunge la EALA Margaret Zziwa alimmiminia sifa Rais Kenyatta kwa
kusema amedhihirisha kujitolea kwa Serikali anayoongoza katika kutimiza
maazimio ya EAC.
Kulingana na Bi Zziwa, hatua ya Serikali kukabiliana na changamoto
zilizokuwa zikiwakumba wafanyabiashara wanaopitisha mizigo katika maeneo
ya mipaka na katika bandari ya Mombasa ni ishara ya kujitolea kwa
Serikali kutimiza malengo ya EAC.
“Hatua hii imeboresha biashara na hakika, wafanyabiashara katika mataifa
ya EAC tayari wanafaidika kwenye biashara zao,” alisema.
Mwenyekiti wa wabunge wa EALA kutoka Tanzania Adam Kimbisa, alimshauri
Rais Kenyatta awe “mtumwa” kwa wananchi.
“Maisha yako sasa yamebadilika kutoka uhuru na kuwa utumwa. Ukiwa mtumwa
kwa wananchi, hiyo ni taadhima na baraka kwako, na Mungu atakubariki
sana,” alisema Bw Kimbisa.
Vijana
Alitumia muda aliopewa kumsifu Rais Kenyatta kwa kujitolea kwake kuleta
umoja baina ya mataifa ya bara la Afrika.
Alizua kicheko bungeni alipomwambia Rais Kenyatta ashauri viongozi
wenzake wa mataifa ya Afrika kuhusu jinsi ya kutawala kama vijana.
“Nadhani itakuwa msaada sana ukionana na marais wenzako na kuwaambia
“waoneni hawa vijana”, nao waweze kuchangamka,” alisema.
Rais pia alisifiwa kwa mipango ya kipekee iliyoanzishwa na Serikali,
kama vile mradi wa kupeana vipakatalishi kwa watoto wa shule za msingi.
“Kuna mataifa mengi Afrika ambayo yameshindwa kununulia wanafunzi kitabu
na kalamu, ilhali wewe unafuata mkondo wa dijitali kwa elimu,” alisema
Bw Kimbisa.
Alikariri msimamo wa EALA kuunga mkono Muungano wa Afrika (AU) kuhusiana
na kesi zinazomkabili rais na naibu wake William Ruto katika Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
No comments
Post a Comment