Mhogo; Dhahabu nyeupe inayooza ardhini *linazalisha bidhaa zaidi ya 300 *bei ya unga ni dolla 2 kwa kg
Na Mobini Sarya,ANSAF
ZAO la mhogo ni miongoni mwa mazao
yasiyopewa kipaumbele kikubwa hapa nchini,huku likibainika kuwa ni sawa na dhabu
nyeupe inayooza ardhini.
Msimu wa kilimo unapowadia wakulima wengi
huanza kufikilia kulima mahindi kama zao la chakula na biashara kisha hufuatiwa na mazao mengine ya
biashara, mhogo
ukionekana kama la ziada katika baadhi ya mikoa.
Hata
hivyo imebainika kuwa zao la mhogo licha ya kwamba linalimwa kwa wingi
hapa nchini lakini faida yake haijaonekana kutokana na jnsi
linavyoandaliwa na kusababisha mkulima kupata faida kidogo.
hivyo kama wazalishaji
wa viwandani wakiamua kukaa na wakulima wakapeana elimu ya kusindika unga wa
mhogo unaotakiwa kwenye viwanda vyao Tanzania inaweza kumaliza tatizo la njaa
na umasikini kwa wakati mmoja.
zao
hilo linaweza kushindana na madini ya dhahabu kama likitumika vizuri
kwani lina utajiri wa ajira tangu linaandaliwa shambani hadi kuvunwa na
kusindika unga wake ambao utazalisha bidhaa mbalimbali huku serikali
ikipata kodi tafauti na ilivyo sasa ambapo serikali haipati chochote.
Hiyo ni kutokana na utafiti uliofanyika nchini Italia
kuhusiana na zao hilo na kuonyesha kuwa zao la muhogo linaweza kutumika kwa
matumizi mbalimbali zaidi ya 300 yakiwemo chakula na bidhaa kama tambi,bisukuti,mafuta
ya lishe,keki,sabuni ya unga, kuni, mboga,huksi pamoja na bidhaa nyingine
nyingi.
Matumizi yote yaliyotajwa yanatakikana hapa
nchini na viwanda vyake vipo,lakini cha kusikitisha kama sio usaliti wa wenye
viwanda hivyo wamekuwa wakiagiza unga huo kutoka nje ya nchi.
Lakini pia wakati zao hilo kwa wananchi walio wengi
linachukuliwa kama zao la kinga ya njaa hali iliyosababisha mikoa yenye
chakula kingi kuliacha likiozoea shambani wakisubiri kipindi cha njaa
imefahamika kuwa linaweza kumuingizia mkulima kipato cha haraka kama soko lake
likitangazwa vizuri .
“Kikwazo kikubwa sio upatikanaji wa unga wake
bali ni namna wanavyouandaa ili
sumu yake iweze kutoka ndani ya masaa 12 uwe umepatikana unga
mweupe”anasema Julias Wambura ambaye ni msambaza wa nafaka kwenye masoko.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa
Kilimo ulioandaliwa na Jukwaa la mkulima ANSAF, Mkurugenzi wa kampuni ya Frabho
Enterprises, Julias Wambura anasema kuwa amepata soko la kuuza unga wa mhogo
tani 400 kwa mwezi kwenda china lakini unga huo umekosekana.
“Soko la mhogo ni kubwa kuliko zao lolote
hivi sasa sema wakulima wetu
hawajandaliwa…..mimi mwenyewe nimepata soko la kuuza unga huo tani 400 kwa mwezi lakini umekosekana
wachina waliniambia nikiweza watanilipa dolla 2 kwa kilo ambayo ni sawa na
shilingi 3200”anasema Wambura
mihogo |
Anasema katika utafiti wake amegundua
kuwa Tanzania inalima tani Milioni 7 za mhogo kwa Mwaka hivyo kama wakulima
wangeandaliwa vizuri na kupewa mashine ya kusindika unga wenye ubora Tanzania
ingepiga hatua kubwa kimaendeleo kwasababu zao hilo linastawi haapa nchini na
halihitaji gharama kubwa kulilima.
Wambura anasema kuwa nchini Nigeria
Serikali ilitunga sheria kwamba ni laima kila anayekaanga mikate kiwandani
achanganye na unga wa mhogo kama njia ya kulinda soko la unga wa mhogo na
kuwapa wakulima hamasa ya
kuendelea kulima zao hilo.
Wakati zao limebainika kutumika kuzalisha
bidhaa zaidi ya 300 nchini Tanzania katika Soko la Dar es Salaam,mhogo umebaki
kuwa kitafunio cha chai pekee, au unaweza kuambulia kupata unga wake kwenye
maduka makubwa ya supermarket hivyo kufanya soko lake kuwa dogo.
Hivyo wadau wanashauri serikali kuwapa elimu
ya kusindika unga wa mhogo kwa teknojia ya kisasa na kuzuia uingizaji wa unga
huo kutoka nje kwani ni kuwasaliti wakulima wa ndani.
“Soko lipo kubwa ila mazingira yake ndio
hayajaandaliwa kwasababu bidhaa karibu
zote zinazotengenezwa na kampuni ya Azam, zinatumia unga wa mhogo yaani
mikate,juisi na Bisukuti,viwanda vyote vya pombe wanategemea unga huo lakini
unaweza kukuta wanaagiza kutoka nje”Anasema Wambura
Lakini faida ya Muhogo inaanza kwenye shamba kwani
zao hilo linalovumilia ukame. Baadhi ya wadudu na magonjwa pia huhitaji kiasi
kidogo cha rutuba. Muhogo ni zao la chakula na ni la nne kwa umuhimu katika
nchi zinazoendelea za Bara la Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.
Kwa miaka mingi sasa muhogo umekuwa ni zao linachukuliwa kama zao mbadala
na zao la kimaskini barani Afrika. Ajabu ni kwamba inapotokea ukame na baa la
njaa muhogo ndio mkombozi kwa watu wengi barani Afrika.
Hivi
sasa zao la muhogo limezidi kupata umaarufu zaidi, ambapo taratibi kadri siku zinavyosogoea
linabadilika na kuwa zao la
kibiashara. Katika nchi nyingi za
Afrika kama vile Afrika ya kusini,
Nigeria,Ghana, na kwingineko, kuna
viwanda vikubwa kwa ajili ya
kusindika mihogo.
Unga
wa mhogo huzalisha bidhaa tofauti mojawapo ya bidhaa kubwa
zinazotengenezwa katika viwanda hivyo ni pamoja na wanga kwa ajili
ya kutengenezea nguo, madawa,
kiungo cha kuongeza ladha kwenye
vyakula, pamoja na glucose
inayotokana na muhogo.
Mhogo unataajwa kuwa ni dhahabu nyeupe
inayoweza kushindana na madini kutokana na soko lake kupanuka kuanzia shambani
hadi sokoni huku zao hilo likitajwa kuwa halihitaji gharama kubwa kuwekeza.
“hapa nchini mhogo unahitaji kutengenezea
pombe, kwenye viwanda vya bia,syrup ya madawa,gundi vindoge makampuni
yanayotengeza juisi na biskuti wanaagiza nje kwa kuwa hapa ndani
haaipatikani”anasema Wambura huku akisisitiza kuwa umefika wakati serikali
itazame zao la mhogo.
Ofisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya
Songea mkoani Ruvuma Kasam Maswaga anasema elimu ya kusindika muhogo ikienea
katika maeneo mengi nchini miaka kumi ijayo zao la muhogo litakuwa ni zao kubwa
na lenye heshima katika kuinua kipato cha mkulima kwa kulifanya kuwa zao la
chakula na biashara.
“Sisi wataalam wa kilimo na serikali kwa
ujumla tumelenga kuhakikisha zao la muhogo kupitia usindikaji linafikia
kutumika kama zao la chakula na biashara kwa sababu hivi sasa tunaendelea kutoa
mafunzo ya namna ya kulisindika hili zao na namna ya kulitumia”,anasema
Maswaga.
Inatajwa kuwa Muhogo ni chakula kikuu cha karibu
watu billioni moja katika nchi zaidi ya 105 duniani. Zao hili huchangia
zaidi ya theluthi moja ya mahitaji ya virutubisho vya kuongeza nguvu mwilini
(calories); Utafiti umeonyesha kwamba zao la muhogo linaweza kusaidia nchi
masikini kukabiliana na uhaba wa chakula na nishati.
Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji
wakubwa wa muhogo barani Afrika. Karibu hektari 670,000 za ardhi ya kilimo
zinatumika kuzalisha muhogo. Muhogo ni zao muhimu la chakula baada ya
mahindi. Zao hili linachangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima.
Inakadiriwa kuwa takribani kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini Tanzania.
Lakini Wambura anasema kuwa pamoja wingi wa
uzalishaji huo bado takribani viwanda vyote haapaa nchini huagiza unga wa mhogo
kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutegengenezea bidhaa zake huku wakulima wetu
wakiachwa bila chochote.
Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza,
Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kogoma, Pwani na Karibu maeneo
yote ya Zanzibar. Ukanda wa Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na
ukanda wa kusini. Mkoa wa Ruvuma huzalisha kati ya 5-10% ya uzalishaji wote
Tanzania.
Nchini Tanzania, muhogo unatajwa kuwa zao la pili kwa kuchangia pato la
taifa kwa asilimia 19 baada ya mahindi.
Pamoja na hayo, zao la muhogo lina faida nyingi sana ambazo humtoa mkulima
katika wasiwasi wa kutumia fedha nyingi katika kununua dawa za mimea.
Zao
hili lina faida nyingi kijamii na hata kiuchumi na kwa maendeleo ya nchi. Ni
zao ambalo linaweza kuzalisha bidhaa zaidi ya 300, zikiwemo zile za chakula na
ambazo si za chakula viwandani. Unga wake hutumika kutengeneza vyakula
mbalimbali, baadhi ni uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, biskuti, na
maandazi. Majani yake hutumika kama mboga na dawa pia.
Katika viwanda, mazao yanayopatika katika
mzizi wenyewe, miti na majani
huweza kuzalisha bidhaa anuwai. Baadhi ni vifaa vya nguo, karatasi, mafuta,
kilevi, dawa za binadamu, na
plastiki. Vilevile wanga wa muhogo hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi
katika samani, rangi za awali katika kuta za nyumba na sukari(Sugar syrup).
Kwa mara ya kwanza zao hili lililetwa na wareno, hapa Afrika.
Zao hili hulimwa nchi zaidi ya 34 za Afrika kwenye eneo lenye ukubwa wa zaidi
ya ekari milioni 200.
Kilimo cha mihogo huhitaji ujuzi kidogo sana na ni rahisi kulima. Zao hili hustahimili ukame
na huweza kubakia ardhini kwa muda mrefu kuepukana na baa la njaa. Upatikanaji wa mavunoni wa uhakika kuliko
mazao ya nafaka. Mizizi ya mihogo ndio tegemeo kubwa la wakulima. Mihogo huwa
na kiasi kikubwa sana cha VITAMINI ‘A’
na kiasi
kidogo cha protini. Ulaji wa mihogo huwasaidia walaji kuepukana
na ugonjwa wa ukavu macho.
Pia majani ya mihogo huweza kutumika kama mboga za majani maarufu kama KISAMVU. Kuna kemikali iitwayo CYNOGENIC
GLUCOSIDE ambayo inaweza kuwa sumu kama mihogo isipoandaliwa vizuri. Mihogo
mitamu
ina kiasi kidogo sana cha kemikali hii na huweza kuliwa hata Mibichi.
Mpaka
sasa hivi kuna aina mbili za mbegu bora ambazo zimethibitishwa kwa wakulima. Mbegu hizi huvumilia magonjwa, (batobato na matekenya), pia huzaa sana ukilinganisha na mbegu za kienyeji.
Naliendele Huzaa tani 19 kwa hekta moja, na inaweza kuvunwa
kuanzia miezi 9 toka ipandwe. Kiroba; Huzaa tani 25 – 30 kwa hekta moja,
na inaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka ipandwe.
Maoni 4
Elimu nzuri sana hii. Je, ni wakulima wangapi wataona makala haya? Muda utaamua. Ubarikiwe na endelea kutupa elimu.
Nashukuru kwa makala yako nzuri, lakini me nnashida moja ya kupata soko la muhogo au kiwanda chochote kinachochakata au kufanya any other kind of processing ya muhogo. kama unamjua mtu naomba anitafute kwwenye no 0672297498 tufanye biashara
Hekari moja bei gani
Nahtaji kujua soko la kilimo nipo kigoma 0752527611
Chapisha Maoni