Kapuya kitanzini
KASHFA ya
kumbaka na kutishia kumuua msichana wa miaka 16 inayomkabili Mbunge wa
Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), imezidi kuchukua sura mpya
baada ya serikali kutoa kauli nzito ya kutaka kumfungulia mashitaka
mbunge huyo, Tanzania Daima Jumapili limebaini.(HD)
Mashitaka
yanayotajwa kumkabili mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri katika
awamu tofauti za uongozi, ni pamoja na ubakaji na kutishia kuua.
Kamishna
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliliambia
gazeti hili jana kuwa jeshi hilo halitakuwa na sababu ya kumuacha mbunge
huyo kuendelea kutamba mitaani huku akituma ujumbe wa vitisho kwa binti
wa miaka 16 anayedaiwa kumbaka.
Alisema
watachukua hatua za haraka kama mtoto huyo atakwenda kufungua jalada la
kutishiwa maisha katika kituo chochote cha polisi jijini Dar es Salaam
wakati wowote.
Kamishna
Kova alisema hadi jana jeshi lake lilikuwa halijapata malalamiko yoyote
kutoka kwa binti anayedai kubakwa na kutishiwa maisha na Profesa Kapuya,
kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi iliyosajiliwa kwa jina la
Profesa Kapuya na kuongeza kuwa muda wowote taarifa hizo
zitakapofikishwa polisi wataanza kuzifanyia kazi.
"Sisi
Polisi hatuna shamba hapa mjini zaidi ya kukabiliana na uhalifu... na
huyo binti mwambie aje afungue malalamiko yake, tena amuone RPC yeyote
katika mikoa ya kipolisi ya Dar es Salaam na si hili la kutishiwa tu,
hata hilo analosema la kubakwa na sisi tutamuwajibisha aliyefanya hivyo
katika makosa mawili tofauti," alisema Kamishna Kova.
Wakati
Kamanda Kova akisema hawatakuwa na ajizi na tuhuma za kubaka na kutishia
kuua zinazomkabili Profesa Kapuya, habari kutoka Ikulu ya Rais Jakaya
Kikwete zinaeleza kuwa kiongozi huyo wa nchi amekerwa na kauli ya Mbunge
huyo wa Urambo Magharibi kuwa serikali haiwezi kumfanya jambo lolote.
Ni
kutokana na kauli hiyo mtoa taarifa wetu alisema rais aliagiza vyombo
vya dola kufuatilia kwa karibu sakata hilo na kuhakikisha sheria
inachukua mkondo wake.
Juzi
gazeti hili lilinukuu moja ya ujumbe mfupi wa maneno kutoka katika simu
ya Profesa Kapuya kwenda kwa binti anayedai kubakwa na Kapuya, sehemu ya
ujumbe huo unasomeka kuwa: "Mkiuawa itakuwa vizuri....itawapunguzia
gharama za kuishi, usitake kugombana na serikali mtoto mdogo kama wewe,
sisi ndiyo wenye nchi yetu, mwenye hilo gazeti ni Mbowe, sasa mwambieni
nyumba ya kuishi si mmemuingizia hela leo? Mnatumika tu bure watu
wanaingiza hela nyingi, ila mmenitibua lazima niwaue wiki hii haitaisha
nitapiga kambi kote, jana si wamekuficha, tuone utalindwa milele, maana
washatengeneza hela lazima mvae sanda tu, hilo sio ombi ni wajibu wenu,
mnajitia na nyie mafia watoto siyo, watoto wetu wanauza unga nani
anawakamata? Nani atapingana nasi."
Pia kwa
upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), taarifa zinaeleza kuwa chama hicho
kimeamua kumtosa mbunge huyo aliyewahi kuongoza Wizara ya Elimu na
Ulinzi kwa nyakati tofauti baada ya kumtaka aache kukihusisha chama na
kashfa yake ya kubaka.
Mmoja wa
viongozi wa CCM aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotaja jina
lake kwa vile siye msemaji wa chama, alidokeza kuwa chama hicho
kilijaribu kulimaliza suala hilo kimya kimya, lakini lilikwamishwa na
Profesa Kapuya mwenyewe kwa kutofika kwenye vikao vya usuluhishi na
binti huyo.
Pia imebainika kuwa baadhi ya wabunge waliokuwa wanataka kumsitiri Profesa Kapuya aliishia kuwaona kama wabaya wake.
"Hapa
palipofika ahangaike peke yake, watu walijitahidi kadiri walivyoweza
hili suala limalizike lakini mwenzetu alikuwa mzito kushirikiana nasi,
sasa hakuna anayetaka chama kichafuke zaidi, amesubiriwa Dodoma na
watoto wiki mbili hatokei, hadi watoto wakashauriwa kwenda kuwaona
viongozi wakuu Dar es Salaam," alisema kiongozi huyo.
Juzi
gazeti hili lilichapisha habari kuhusu mwanafunzi huyo aliyesema kuwa
waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es
Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo ndani ya ofisi yake katika
Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa
kwenda kuchukua ada kwa mara ya pili.
Kutokana
na habari hiyo Profesa Kapuya kupitia kwa wakili wake, Yasin Memba,
alitishia kuliburuza gazeti hili mahakamani endapo halitamwomba msamaha
ndani ya siku saba.
Mbali na
kutishia kulipeleka gazeti hili na baadhi ya mitandao ya kijamii
mahakamani pia Profesa Kapuya alikana kumfahamu binti anayedai alibakwa
huku akikanusha kumiliki simu namba 0784993930 ambayo imekuwa ikitumiwa
kuwasiliana naye ikiwemo kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) wa
vitisho.
Uchunguzi
wa gazeti hili umebaini kuwa ni kinyume cha sheria za Mamlaka ya
Mawasiliano nchini mtu kugawa namba iliyosajiliwa kwa jina lake.
Katika
namna ya kushangaza, juzi Kapuya kupitia kwa wakili wake alidai kwamba
simu hiyo aliishaigawa miezi sita iliyopita, hivyo hahusiki kwa namna
moja ama nyingine na tuhuma alizopewa.
Wakati
Kapuya akikana kumiliki simu hiyo, Novemba 9, mwaka huu gazeti hili
liliwasiliana naye kupitia namba hiyohiyo anayodai kwamba alishaigawa
miezi sita iliyopita.
Tarehe
hiyo, gazeti hili liliwasiliana na mbunge huyo ili kuthibitisha tuhuma
zilizokuwa zikimkabili wilayani Kaliua za kumpiga makofi kiongozi mmoja
wa CCM.
Kapuya kupitia namba hiyo, alitoa utetezi wake ambapo gazeti hili lina sauti yake.
Utetezi
wa Kapuya pia unaongeza utata kwa kushindwa kufafanua namna alivyoweza
kugawa namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake kwa mtu mwingine, huku
ikiendelea kutuma fedha na vitisho kwa binti huyo.
Alilishutumu
gazeti hili kuwa lilimhukumu na kuchapisha tuhuma zake bila kumpa
nafasi ya kujitetea kama inavyoelekezwa katika tasnia ya habari.
"Kwa
sababu hiyo, amenielekeza niwapatie siku saba gazeti la Tanzania Daima,
mitandao ya kijamii ukiwemo wa Jamii Forum, Justina John na Vituko
Mtaani, ambao walichapisha habari hiyo, waombe radhi kwa uzito uleule la
sivyo atavishitaki mahakamani," alisema Memba wakati akizungumza na
waandishi wa habari juzi.CHANZO TANZANIA DAIMA.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni