MUMBILI KWA VITAMBULISHO SASA
MENEJIMENTI ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam,
imetangazautaratibu mpya wa wagonjwa, wafanyakazi na watu mbalimbali
kuingia hapo kwa shughuli zao ikiwa ni pamoja na kupata huduma ya tiba,
kufanya kazi na pia kuchukua maiti na kuona wagonjwa.
Kwa mujibu wa utaratibu huo, ambao pamoja na mambo mengine
umeweka mfumo mpya wa kuingia hospitalini hapo, wafiwa wanaokwenda
kuchukua au kuaga miili ya ndugu zao, sasa watapaswa kuwa na vitambulisho na
kumtambua marehemu kwa jina kabla ya kuruhusiwa.
Ili kurahisisha hilo, kwa mujibu wa utaratibu huo mpya ambao
ulianza kutumika Jumatatu, majina ya marehemu watakaoagwa au
kuchukuliwa katika siku husika, yatakuwa kwa walinzi langoni ili kurahisisha
shughuli hiyo.
Watakaohitaji kuaga au kuchukua miili ya wapendwa wao,
watatakiwa kutaja majina ya marehemu kwanza kwa walinzi wa lango kuu la
kuingilia na kama yatakuwa kwenye orodha ya wanaotarajiwa kuchukuliwa siku
hiyo, wataruhusiwa.
Mbali na utaratibu wa kuchukua na kuaga maiti, mfumo huo
mpya umeweka utaratibu wa kuhudumia wagonjwa na kuingia kutibiwa au kuona
daktari na pia kwa wanaopeleka chakula kwa wagonjwa, ataruhusiwa mtu
mmoja tu atakayezingatia muda uliowekwa wa kuona wagonjwa.
Kupitia utaratibu huo, wagonjwa wanaokwenda kutibiwa,
watalazimika kuonesha kadi zao za miadi kwa walinzi kabla ya kuingia,
zikionesha tarehe husika ya kliniki au barua ya rufaa inayoonesha kuwa
wanatakiwa kutibiwa hospitalini hapo.
Kwa wafanyakazi na wanafunzi wa hospitali hiyo, watapaswa
kuvaa
vitambulisho wakati wote wawapo hapo na sare zao za kazi
hadi muda wa
kazi utakapokwisha ambapo pia magari yatakayoingia hapo,
yatafanyiwa
ukaguzi maalumu na ya wafanyakazi yatabandikwa stika maalumu
kwa ajili
ya utambulisho.
Katika ukaguzi huo, dereva na abiria wataeleza wanakokwenda
na baada ya hapo, watafuatiliwa ili kuhakikisha walikosema ndiko kweli
waendako; lengo la yote hayo ni kukabiliana na vitendo vya uhalifu
vinavyojitokeza hospitalini hapo.
Tunapongeza hatua hiyo ya Muhimbili, kwani vitendo vya wizi
na
udanganyifu vimekuwa vikifanyika hapo kutokana na hospitali
hiyo kubwa nchini, kupokea watu wengi na magari mengi kwa wakati mmoja
huku wakijipenyeza wengine na kujifanya madaktari na kuibia
wagonjwa fedha.
Tunashauri utaratibu huu usimamiwe vizuri ili usitumike
vibaya na
watumishi wachache wasio waadilifu, kunyanyasa wananchi na
hususan wagonjwa wanaofika hapo kupata huduma za kiafya na zingine
zenye maslahi kwao.
Ni kawaida sehemu yoyote panapoanzishwa utaratibu unaobana
watu, wapo wachache ambao hutafuta kila mbinu kuhakikisha taratibu hizo zinahujumiwa na hatimaye kuondolewa na hilo mara nyingi
husababisha watu kukamuliwa hata fedha ili tu ukiukwaji uweze kuhalalishwa.
Mathalan kuna watu wengine watataka kuingia kuona wagonjwa
wao kwa kundi na watakapokataliwa watatafuta uwezekano wa kuhonga ili
waruhusiwe kuingia na inapofanikiwa huku walinzi wakinufaika kifedha,
basi ‘uhalalishwa’ na kuwa utaratibu wa kawaida ‘kulipia’ kuingia
Muhimbili.
Sisi tunaamini kama utaratibu uliowekwa na Muhimbili
utaheshimiwa na kufuatwa kama inavyotakiwa, malalamiko ya wizi wa vyombo vya
usafiri na
udanganyifu ambao umekuwa ukifanywa na vitendo vya madaktari
feki kuvinjari vitamalizika.
Ni vema wananchi wanaopata huduma Muhimbili wakatoa
ushirikiano katika
kuheshimu na kufuata taratibu hizi, lakini pia walinzi
watumie busara, utu, uaminifu na uadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya
kuhudumia Watanzania wenzao lakini pia wageni walioko nchini.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni