Zinazobamba

MAKUBWA YAFICHUKA BANDARI DARESALAAM, MWAKYEMBE ADAIWA KUMLINDA MADENI KIPANDE

mwakyembe 6075a
SIRI ya mgogoro kati ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliyovunjwa hivi karibuni imewekwa hadharani, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Waraka ulionaswa na gazeti hili ulioandaliwa na mmoja wa waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo, umeainisha kuwa hatua ya Waziri Mwakyembe kuivunja bodi hiyo kulilenga kumlinda Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Madeni Kipande, ambaye bodi hiyo ilipanga kumng'oa madarakani.(HD)
Kwa mujibu wa waraka huo unaodaiwa kuandaliwa na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya TPA, John Ulanga, uliovuja katika mtandao wa Jamiiforums.com hivi karibuni, umebainisha kwamba sababu kubwa ya Dk. Mwakyembe kuvunja bodi hiyo ilikuwa kumuokoa Kipande ambaye bodi ilishamuona hafai kuongoza mamlaka hiyo na kutaka kumuokoa.
Katika waraka huo mrefu, Ulanga ameanisha sababu na uwezo wa kisheria wa bodi kumuondoa Kipande, waraka ambao haukujadiliwa kutokana na Dk. Mwakyembe kuivunja bodi siku moja kabla ya kuwasilishwa kwake.
Hata hivyo, Ulanga ambaye ni mwanasheria anayeongoza taasisi inayoheshimika ndani na nje ya nchi ya Foundation for Civil Society, anaelezwa na watu walio karibu naye kwamba amekerwa kuvuja kwa waraka huo, hasa baada ya yeye kuwa mmoja wa watu waliokuwa wakituhumiwa na Kipande kuwa ni wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutokana na msimamo wake.
Mmoja wa wajumbe wa bodi ya sasa ameliambia gazeti hili kwamba hata wao hawana uhuru wala amani kwa kuona kilichozipata bodi zote mbili zilizopita na ambazo zote anaamini ziliundwa na watu makini lakini zikashindwa kufanya kazi chini ya Waziri Mwakyembe.
Katika waraka huo, imeelezwa kwamba Kipande ameonyesha kiburi na dharau kwa bodi kwa kushindwa kufuata maagizo (mapendekezo) ya bodi na badala yake amekuwa hata akiwadhalilisha wajumbe wa bodi kama anavyofanya kwa baadhi ya wasaidizi wake.
Tuhuma nyingine zilizoanishwa dhidi ya Kipande ni pamoja na; jinsi alivyoendesha uajiri wa viongozi wa juu kinyume cha maagizo ya bodi; ubaguzi dhidi ya wafanyakazi, watu wa makabila tofauti; chuki na Wana CHADEMA; kuingia kwenye mikataba bila kufuata taratibu hasa kwenye suala la e-CTN; kuchelewesha utekelezaji wa "Big Results Now" na
kumdanganya waziri kuhusu mapato ya TPA.
Kwa kutumia takwimu za Kipande ambaye hakuwa akiwashirikisha wataalamu wake, Waziri Mwakyemba amekuwa akitangaza kwamba Bandari ya Dar es Salaam imeongeza makusanyo yake kutoka sh bilioni 28 hadi sh bilioni 50 huku akijua kuwa si sahihi.
Mamlaka ya Bandari imekuwa ikizingirwa na tuhuma luluki huku wananchi wakiendelea kuaminishwa kwamba hali ni shwari.
Hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi, kutokana na bandari kuwa lango kuu la uchumi kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bandari.CHANZO TANZANIA DAIMA

Hakuna maoni