CHUO CHA SERIKALI ZA MITAA CHAONGEZA UDAHILI KWA MWAKA WA MASOMO 2013/2014

AfisaUhusiano wa Chuo cha Serikali za mitaa Bw.Sebera Fulgence akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya chuo hicho ikiwa ni pamoja na kufanya mafunzo kwa Watumishi wa Serikali wapatao 4,913,wakati wa Mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano toka Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Bi. Rebecca Kwandu.
Chuo cha Serikali za Mitaa [The Local Government Training Institute] Hombolo , Dodoma kimedahili Wanafunzi 1603 kwa
mwaka wa masomo 2013/2014. Idadi hii inajumuisha Wanafunzi waliomaliza
kidato cha nne na kujiunga na Astashahada (Basic Technician Certificate
courses) na kidato cha sita wanaojiunga na Stashahada (Ordinaly Diploma
Courses) katika fani za Uhasibu na Fedha, Uongozi na Uendeshaji katika
Serikali za Mitaa, Maendeleo ya Jamii na Menejimenti ya Rasilimali Watu.
Idadi hii ya wanafunzi waliodahiliwa na wale wanaoendelea na masomo
inafanya Wanafunzi wote kufikia 2,491 kwa mwaka wa masomo 2013/2014.
Idadi hii ni sawa na ongezeko
la asilimia 96.5% ukilinganisha na jumla ya wanafunzi 86
waliodahiliwa katika mwaka wa masomo 2007/2008. Kimsingi Idadi ya
Wanafunzi wanaojiunga na Chuo hiki imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka
kuanzia mwaka wa Masomo 2007/2008, kwa sababu zifuatazo:-
- Kuongezeka kwa kozi kutoka kozi nne (4) za awali mpaka kozi nane(8) kwa sasa.
- Kuongezeka kwa Watumishi Wanataaluma na Waendeshaji kutoka 38 mwaka 2007/2008 hadi 108 mwaka 2013/2014
- Kuongezeka kwa miundombinu mipya ya kujifunzia na kufundishia kama ifuatavyo:-
- Mabweni (8) yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 1,620 jumla;
- Madarasa (8) yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 jumla;
- Ofisi (8) zenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watumishi 10;
- Maktaba yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kwa pamoja;
- Maabara ya kompyuta yenye uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 300 kwa pamoja;
- Bwalo la chakula na jiko la kisasa lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kwa pamoja;
- Nyumba za makazi ya Watumishi (15), yaani daraja A (5) na daraja B(10);
- Ukumbi wa kutolea mihadhara namba 3 ambao una uwezo wa kubeba watu 576;
- Kumbi za mihadhara namba moja na namba mbili zenye uwezo wa kubeba watu 400;
Aidha, Chuo kimeanza ujenzi wa Kituo cha Afya
cha kisasa kitakachogharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.8 Lengo kubwa
la ujenzi wa kituo hiki ni kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa
Wagonjwa wapatao 3000 wajumuiya ya Chuo ikiwemo wanakijiji waliozunguka
Chuo.
Chuo
cha Serikali za Mitaa ni miongoni mwa Taasisi zilizoko chini ya
OWM-TAMISEMI na kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 26 ya mwaka 1994
(Sura ya 396 toleo lililorejewa mwaka 2002). Lengo kuu la kuanzishwa
kwake ni kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kutoa huduma
bora zitakazowajengea wananchi uwezo wa kuimarisha utawala bora,
kuondokana na umaskini na kuboresha maisha yao.
Madhumuni
mahususi ya Chuo ni kuchangia katika uwezeshaji wa mchakato mzima wa
kupeleka madaraka kwa wananchi, kujenga na kukuza utawala bora, kukuza
uchumi na kuondoa umaskini katika ngazi mbalimbali za Serikali za
Mitaa hapa nchini.
Chuo
hiki kimesajiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (National
Council for Technical Education) ambalo ndilo lenye mamlaka ya kusimamia
ubora, viwango na uendeshaji wa Vyuo vya Elimu ya juu na Ufundi visivyo
Vyuo Vikuu hapa nchini.
Majukumu ya Chuo yamegawanyika katika sehemu kuu tatu:-
- Kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu juu ya taaluma, ujuzi, stadi na mbinu za uendeshaji wa Serikali za Mitaa kwa Viongozi na Watumishi walio katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa;
- Kutoa mafunzo juu ya mabadiliko yanayohusu Serikali za Mitaa kulingana na Mpango wa Uboreshaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa na;
- Kufanya utafiti na kutoa ushauri kwa Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika na watu binafsi juu ya masuala yote yanayohusu Serikali za Mitaa.
Vilevile kinashirikiana
na Vyuo au Taasisi nyingine katika kujiletea maendeleo ya kitaaluma na
pia maendeleo kwa wananchi. Vyuo na taasisi hizo ni kama vile Chuo cha
Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP – Dodoma), Chuo Kikuu cha Dodoma,
Taasisi ya SYD-Forum (Sweden), Chuo Kikuu Mzumbe, Taasisi ya Maendeleo
ya Maafisa wa Serikari za Mitaa (LOGODI – Local Government Officials
Development Institute) ya Korea na Chuo cha Uongozi cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere (Dar es Salaam).
Vilevile
kinashirikiana na jamii iliyo karibu katika utatuzi wa changamoto
mbalimbali zinazoikumba hususani suala la maji kwa wananchi walio
karibu na Chuo, kuchangia madawati na ujenzi wa shule za msingi, kutoa
ufadhili kwa wanafunzi wasiojiweza kifedha ili kuwawezesha kupata
mafunzo yatolewayo hapa Chuoni na huduma nyingine.
Pamoja
na kutekeleza majukumu tajwa hapo juu, Chuo kinakabiliwa na changamoto
mbali mbali kama vile ubovu wa barabara ya Ihumwa – Hombolo yenye urefu
wa kilomita 27 ambayo haijajengwa kufikia angalau kiwango cha
changarawe hali ambayo inafanya magari yanayotumia barabara hiyo
kuharibika mara kwa mara hivyo kuongeza gharama za matengezo.
Ombi letu kubwa katika suala hili ni barabara hiyo kutengenezwa kwa kiwango cha lami.
Imetolewa na:-
Ofisi ya Uhusiano
Chuo Cha Serikali za Mitaa, Hombolo Dodoma
24.10.2013
No comments
Post a Comment