KASHFA MPYA DAWA ZA KULEVYA

Raia wa
Nigeria aliyefukuzwa Kenya miezi minne iliyopita kwa kuhusishwa na
biashara ya dawa za kulevya, amekamatwa tena nchini humo akiwa na pakiti
425 za heroin, akiaminika kwamba alipitia Tanzania.
Mtu huyo
aliyetajwa kwa jina la Enobemhe Emmanuel Peter inaaminika alishukia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea
Nigeria na kisha kwenda Kenya kwa barabara, kupitia mpaka wa Namanga
mkoani Arusha.(hd)
Peter
alikamatwa pamoja na mwanamke ambaye ni raia wa Kenya, usiku wa Ijumaa
iliyopita jijini Nairobi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Raia huyo
wa Nigeria ni kati ya wageni waliofukuzwa nchini humo Juni mwaka huu
kwa agizo la Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliyeamuru raia wa kigeni
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya wafukuzwe nchini humo.
Mkuu wa
Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha Kenya, Dk Hamisi Massa
alisema uchunguzi zaidi wa dawa hizo utafanyika kabla mtuhumiwa huyo
kufikishwa mahakamani.
"Ni kati
ya watu waliokuwa wamefukuzwa nchini katika nyumba aliyokamatiwa
kulikutwa pia na pakiti 425 za heroin," alisema Dk Massa.
Mtu huyo
amekamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa zilizoonyesha kuwa, watu wengi
waliofukuzwa Kenya kutokana na kujihusisha na biashara hiyo sasa
wamerejea tena.
Julai 9
mwaka huu, Ofisa Uhamiaji wa nchi hiyo, Edward Kabiu Njau alifikishwa
mahakamani na kushtakiwa kwa kumruhusu Anaeke Chimenze, aliyefukuzwa
nchini humo, kurejea tena.
Chimenze
ambaye ni raia wa Nigeria mwenye pasi ya kusafiria namba 02743350, pia
anadaiwa kurudi nchini humo kupitia mpaka wa Namanga.
Uhamiaji Tanzania
Msemaji
Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna, Abbas Irovya alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yupo nje ya ofisi. "Mtafute Tatu ndiye
mtu wa habari zaidi, kama atakuwa amepata hizo taarifa atakueleza,"
alisema.
Mwananchi
ilipomtafuta Tatu Iddi alisema hajapata taarifa hizo na kutaka
mwandishi amtumie barua pepe ikiwa na maelezo ya mtu huyo aliyekamatwa
ili aweze kutafuta taarifa zaidi.Naye Kaimu Msemaji wa Idara ya
Uhamiaji, Mbaraka Batenga alisema hayuko kwenye nafasi nzuri ya
kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hakuwa ofisini kutokana na kuugua.
Hata hivyo, alisema kwa kawaida mtu akifukuzwa kwenye nchi moja isitafsiriwe kuwa haruhusiwi kwenda nchi nyingine.
"Naomba
nikusaidie kitu kimoja kama kwa ajili ya kuelewa zaidi mambo haya, mtu
akifukuzwa kwenye nchi moja haina maana kuwa hawezi kwenda kwenye nchi
nyingine, sisi tukimfukuza mtu itakuwa kosa kama atarudi tena
Tanzania,"alisema na kuongeza:
"Kwa hiyo
kama huyo mtu alifanya kosa huko Kenya na akafukuzwa Kenya ni kosa
kurudi Kenya, hapo hata ofisa aliyemruhusu kurudi huko itabidi
akamatwe," alisema Batenga.
Kwa
upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za
Kulevya, Godfrey Nzowa alisema mtu akifukuzwa nchi moja haimaanishi kuwa
haruhusiwi kwenda nchi nyingine.
Alisema
kama kikosi cha kupambana na dawa za kulevya cha Kenya kingekuwa
kinashirikiana na kile cha Tanzania, ingekuwa rahisi kuwadhibiti watu
hao.
"Wenzetu
wangekuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano na sisi ingesaidia sana,
wakimkamata mtu wanatuambia. Huyo mtu alipita tu Tanzania," aliongeza
Nzowa.
Nzowa
alitahadharisha kuwa kumfukuza sio kigezo cha kumzuia mtu kupita
Tanzania kwani haijulikani alifukuzwa kwa kosa lipi huko Kenya.
:CHANZO MWANANCHI
No comments
Post a Comment