TBS YAWEKA VIWANGO 3,901, WAFANYABIASHARA WADOGO 1,683 WANUFAIKA
Na Mwandishi Wetu
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa viwango 3,901 vya bidhaa katika sekta mbalimbali na kutoa vyeti na leseni za ubora 3,940 kwa wazalishaji, wakiwemo wajasiriamali wadogo 1,683, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia mwaka 2021 hadi 2026.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, wakati akizungumza kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa waandishi wa habari na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Oktoba 27, 2026, jijini Dar es Salaam.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa nchini, kuwawezesha wazalishaji kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema TBS, iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha sekta za viwanda na biashara, hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria ya Viwango, Sura ya 130.
“Katika kipindi hicho, shirika limeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma, kuimarisha ukaguzi wa bidhaa, kusajili bidhaa na maeneo ya biashara pamoja na kutoa elimu kwa wazalishaji na wadau wengine kuhusu masuala ya viwango na ubora,” amesema.
Amesema katika kuboresha upatikanaji wa huduma, TBS inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji na makabidhiano ya mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara katika eneo la Njedengwa, jijini Dodoma, unaojulikana kama Viwango House–Dodoma, wenye thamani ya Sh bilioni 24.7.
Pia, shirika linaendelea na ujenzi wa ofisi na maabara katika eneo la Kiseke, Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza, kupitia mradi wa Viwango House–Mwanza, unaokadiriwa kugharimu Sh bilioni 12.1.
Aidha, TBS ipo katika hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa ofisi na maabara nyingine jijini Arusha, zitakazojulikana kama Viwango House–Arusha.
“Maabara za Dodoma zinatarajiwa kuhudumia mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, wakati maabara za Mwanza zitahudumia mikoa sita ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
“Uwekezaji huo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza gharama za upimaji, huku ukiongeza ufanisi katika upatikanaji wa majibu ya vipimo vya sampuli,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema katika hatua nyingine, Serikali kupitia TBS imetumia zaidi ya Sh bilioni 9.8 kuimarisha ofisi tisa za kanda pamoja na ofisi za mipakani, bandarini na viwanja vya ndege.
Ofisi hizo zinahusisha kanda za Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Pwani na Geita, pamoja na maeneo mbalimbali ya kuingilia bidhaa nchini.
Amesema uboreshaji huo umehusisha kuongeza ofisi, wafanyakazi na vitendea kazi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa sokoni na mipakani ili kupunguza uwepo wa bidhaa hafifu na kulinda afya na usalama wa walaji.

No comments
Post a Comment