KAPALATA AISHAURI SERIKALI KUREJEA MUUNDO WA WIZARA YA MADINI NA SHERIA YA MADINI ILI KUAKISI NA KUTAFSIRI SEKTA YA MADINI KUENDANA NA MSTAKABALI WA DIRA YA MAENDELEO TAIFA HADI 2050 NA MAONO YA WIZARA YA MADINI HADI 2030 KAMA MOJAWAPO YA SEKTA ZA KIMKAKATI ZA MAENDELEO YA TAIFA

🇹🇿 Asema kwa kuwa sekta ya madini inakua kila kukicha na inatafrisiwa kwa kauli mbiu kuwa madini ni maisha na utajiri kama ilivyo sekta ya kilimo ni uti wa mgongo wa taifa, ni muhimu sana bila kuchelewa kurejea muundo wa wizara ya madini na sheria ya madini ili kuakisi na kutafsiri sekta ya madini kuendana na mstakabali wa dira ya maendeleo ya taifa hadi 2050 na maono ya wizara ya madini hadi 2030 kama mojawapo ya sekta za kimkakati za maendeleo ya taifa ili kuleta tija kwenye tasnia ya madini na kuitafsiri tasnia hii kibiashara pia na sio kirasilimali kama ilivyo sasa kwa kuongeza nguzo (pillars) mpya za maendeleo ya madini ili pamoja na mengineyo nguzo zilipo na nguzo mpya ziwe imara na thabiti kwa kulenga kila aina ya madini yanayopatikana nchini.
🇹🇿 Aeleza kuwa tume ya madini iliyopo sasa pamoja na mengineyo iwe na idara kubwa mbili, yaani idara ya rasilimali madini (mineral resource and reserves department) ambayo kazi yake kubwa itakuwa ni kutafuta, kuratibu, kulinda, kusimamia na kutafsiri tasnia ya madini kirasilimali na idara ya maendeleo ya madini (minerals development department) ambayo kazi yake kubwa itakuwa kubuni, kuratibu, kuendeleza, kusimamia na kutafsiri tasnia ya madini kibiashara zaidi.
🇹🇿 Atamka kuwa kama ilivyo kupitia sekta ya kilimo kuna kauli mbiu kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa hivyo basi sekta ya madini iendelee kuwa na kauli mbiu kwamba madini ni maisha na utajiri kwani sekta hii inakua na kuajiri watu watu wengi hasa vijana ambao ni taifa la kesho kila kukicha na hivyo basi pawepo na mtaala wa somo la madini kuanzia ngazi ya shule ya msingi na ya sekondari ili katika vyuo vya kati mpaka vyuo vya juu wigo wa uelewa wa sekta hii na kutengeneza wataaluma thabiti kila kukicha ufikiwe.
🇹🇿 Atoa maoni kuwa kupitia idara ya maendeleo ya madini pamoja na mengineyo tafiti yakinifu zifanyike juu ya muundo wa wizara kitendaji, kiwajibu na kimajukumu kwa kuongeza mnyororo wa maamuzi ndani ya tume au wizara ili kuwe na ofisi ya afisa madini wa wilaya ambayo itafanyakazi chini ya ofisi ya afisa madini wa mkoa na ofisi ya afisa madini wa kata ambayo atafanyakazi chini ya afisa madini wa wilaya katika kusimamia, kuratibu, kuwajibika na kuendeleza sekta ya madini kwa mfanano au vinginevyo wa majukumu yaliyopo katika ofisi ya madini ngazi ya mkoa kwa sasa kwenye ngazi ya wilaya na ngazi ya kata kama zilivyo sekta nyingine mfano kilimo, mifugo, wanyamapori, misitu, maendeleo ya jamii, afya na kadhalika ili kufungamaisha sekta hii na zingine kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla ili kuleta tija endelevu kwenye sekta hii kwenye mambo mengi pamoja na utoaji wa vibali, utozaji wa kodi na tozo zote zinahusu sekta ya madini kwa nia ya kuleta mabadiriko kwenye sera ya madini na kuitafsiri sera yake kuendana na wakati kijiolojia, kijiografia, kiteknolojia, kijamii, kisiasa, kiusalama, kimazingira na kiuchumi kwa ukweli kuwa madini yanaisha kutokana na kasi ya uchimbaji huku yakichukua muda mrefu sana kuumbika kijiolojia, kufanyiwa utafiti hadi kuchimbwa na kuchenjuliwa.
🇹🇿 Asisitiza kuwa ni muhimu wizara kuweka mazingira rafiki yatayomuwezesha mmiliki wa haki madini katika kumiliki, kutafiti, kuendeleza, kuchimba na kuchenjua madini kwa gharama ndogo inayowezekana kila kukicha, mfano upunguzaji ukubwa wa mwisho wa eneo la utafiti la haki madini kuwa kilometa za mraba 100, muda wa umiliki wa haki madini katika utafiti ili iwe miaka 10 kabla ya kuisha umiliki wa awali ili pamoja na mengineyo kuweka muda unaotosha kufanya utafiti na upembuzi yakinifu kwenye eneo la haki madini ya utafiti, ili kuongeza idadi ya haki madini za utafiti na washiriki wake kwenye sekta ya madini ambao ni walipa kodi na tozo wa uhakika.
🇹🇿 Anena kufanya tafiti makini zitakazolenga kuboresha eneo la haki ya umiliki wa ardhi na haki ya umiliki madini pamoja na wizara fungamani na wadau ili kuweka utaratibu mzuri utakaotatua changamoto zilizopo na kuleta utaratibu thabiti wa kisheria utakaolenga kutatua migogoro inayowahusu wamiliki wa haki ardhi na haki ardhi kwa waledi wa kisheria uliobora kwa pande zote mbili kwa kuboresha utaratibu uliopo katika uendelevu madhubuti.
🇹🇿 Aungana na wajumbe wengine kuelezea umuhimu wa kuundwa kwa bodi ya kisheria ya kijiolojia itayokuwa na wataaluma mahiri wa jiolojia kama ilivyo kwenye bodi zingine kwa mujibu wa sheria ili pamoja na mengineyo kupanua wigo wa wamiliki wa haki madini kupata huduma za mikopo kutoka taasisi za kibenki kutokana na taarifa mahiri za kijiolojia zitakazopimwa kijiografia, kiteknolojia, kisiasa, kijamii, kiusalama, kimazingira na kuichumi. 
*DODOMA*.
Mbunge wa jimbo la Nzega vijijini na mjumbe wa kamati ya kudumu ya nishati na madini ya bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Neto Paul Kapalata, ameishauri serikali kurejea muundo wa wizara kwa kufanya tafiti yakinifu ili kuakisi na kutafsiri dira ya maendeleo ya taifa hadi 2050 na maono ya wizara ya madini hadi 2030 kwa kubaini mazuri na mapungufu halafu kutengeneza muundo mpya itakaoendana na wakati kwa ubora na ushidani wa ndani hadi nje ya nchi kijiolojia, kijiografia, kisiasa, kijamii, kiusalama, kimazingira na kuichumi kwa kujenga misingi imara yenye kesho bora kisekta.
Mheshimiwa Kapalata amesema wizara ya madini inapaswa kuendelea kuwa na mifumo madhubuti ambayo itaboresha udhibiti wa madini wa ndani hadi nje ili kuweza kukizi vigezo vya maendeleo ya madini kama rasilimali na biashara kuanzia hatua ya uvumbuzi, utoaji vibali, utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, ukarabati wa mazingira, ushiriki kwenye jamii, uuzaji, ulipaji kodi na tozo kama hatua thabiti ambazo zitasaidia kubaini changamoto zinazowakumba wadau wa tasnia ya madini na taifa mapema ili kuongeza tija kwenye kila nyanja kwa kuhakikisha taifa na wadau wananufaika ipasavyo kupitia rasilimali madini ili kukuza sekta hii kibiashara huku ikijiendesha yenyewe kupitia mifumo imara.
Mwisho mheshimiwa Kapalata amemshukuru mwenyekiti wa kamati husika ya bunge ambaye ni mbunge wa jimbo la Bagamoyo, mheshimiwa Subira Khamis Mgalu pamoja na makamu wake mheshimiwa Simon Songe Lusengekile ambaye ni mbunge wa jimbo la Busega kwa uongozi mzuri na kipekee amempongeza mheshimwa Anthony Peter Mavunde ambaye ni waziri wa madini na mbunge wa jimbo la mtumba kwa ubunifu na umahiri katika wizara yake bila kusahau timu yake yote iliyoko wizarani na viambata vyake.
Wakati akijibu hoja na maswali mbali mbali kutoka kwa wajumbe wa kamati mheshimiwa Mavunde, amempongeza mheshimiwa Kapalata kwa ushauri mzuri na amekiri kuwa wizara imepokea ushauri na itaufanyiakazi kwa nia thabiti ya kuboresha utendaji wa wizara ili kunufaisha taifa na wadau wa tasnia ya madini kinagaunaga kila kukicha.




No comments
Post a Comment