Zinazobamba

TAKUKURU ILALA YATOA ELIMU YA MAADILI NA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA KWA WATUMISHI WA ATCL


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ilala imetoa elimu kwa watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuhusu maadili ya utumishi wa umma na mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 21, 2026, kando ya semina iliyofanyika katika Makao Makuu ya ATCL jijini Dar es Salaam, Muelimishaji wa Umma wa TAKUKURU, Herman Malima, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea watumishi uelewa kuhusu aina mbalimbali za makosa yanayoweza kujitokeza katika maeneo yao ya kazi.

Amesema makosa hayo yanaweza kuhusiana na shughuli za manunuzi, uhasibu, pamoja na masuala ya kiufundi na uhandisi.

“ Kupitia mafunzo haya, watumishi wanatarajiwa kufahamu viashiria vya vitendo vya rushwa, makosa yanayoweza kujitokeza katika utendaji wao na namna ya kuyazuia kabla hayajatokea,” amesema Malima.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa watumishi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kufuata msemo wa Kiswahili usemao, ‘Kinga ni bora kuliko tiba,’ unaosisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kuzuia vitendo vya rushwa badala ya kusubiri vitokee ndipo hatua zichukuliwe.

Aidha, amesema elimu hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uwajibikaji, uadilifu na uzingatiaji wa taratibu katika utendaji wa watumishi, ili kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa kuzingatia misingi ya maadili na sheria zinazohusika.

Halikadhalika, kupitia mafunzo hayo, watumishi wamehimizwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kusababisha ukiukwaji wa maadili na sheria.

No comments