HESLB YATUNUKIWA CHETI CHA UBORA CHA ISO 9001:2015.
Na Mwandishi Wetu:DAR ES SALAAM
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, amesema kuwa hatua ya kupata Cheti cha Ubora cha Kimataifa cha ISO 9001:2015 ni chachu ya kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa wanafunzi wa elimu ya juu na wananchi kwa ujumla.
Pia, Ameeleza kuwa ni kuimarisha ubora, ufanisi na uwajibikaji ni mambo muhimu katika kutekeleza majukumu ya bodi hiyo.
Dkt. Kiwia amepokea cheti hicho kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, katika hafla iliyolenga kutambua juhudi za HESLB katika kuimarisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi
Akizungumza mapema leo jijini Dar es Salaam watika hafla hiyo, Dkt.Ashura Katunzi amesema kuwa upatikanaji wa cheti hicho ni hatua muhimu itakayoiwezesha HESLB kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ubora wa huduma na kuongeza tija katika utendaji kazi wake.
Aidha, amempongeza Dkt. Kiwia pamoja na uongozi mzima wa HESLB kwa kufikia hatua hiyo ya kutimiza viwango vya kimataifa vya ubora, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha viwango hivyo katika utoaji wa huduma.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, ameishukuru Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ushirikiano wake katika kufanikisha upatikanaji wa Cheti cha Ubora cha Kimataifa cha ISO 9001:2015.
Amesema hatua hiyo ni chachu ya kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma, kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya juu wanapata huduma bora na kwa wakati.
Aidha, amesisitiza dhamira ya HESLB ya kuendelea kuzingatia viwango vya ubora na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake.
Cheti cha ISO 9001:2015 ni kiwango cha kimataifa kinachohusu mifumo ya usimamizi wa ubora, kikilenga kuboresha michakato ya kiutendaji, kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi zinatoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja na wadau wake.
Hatua hiyo inaweka msingi wa kuendeleza juhudi za HESLB katika kuboresha huduma zake na kuimarisha ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kusaidia upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu nchini.

No comments
Post a Comment