LUHENDE AIPONGEZA FEMA MININGI & DRILLING

Mbunge wa Jimbo la Bukene mkoani Tabora, John Luhende, amewataka wananchi na wachimbaji wa madini kutumia fursa ya Maonesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita kupata elimu, maarifa na teknolojia zitakazowasaidia kuongeza tija na kuboresha shughuli zao za uchimbaji.
Luhende ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambako maelfu ya wananchi pamoja na wachimbaji wadogo na wakubwa wamekusanyika kujionea teknolojia, zana na mbinu mbalimbali za kisasa zinazotumika katika shughuli za madini.
Amesema maonesho hayo hayapaswi kutazamwa kama sehemu ya kutembelea pekee, bali ni fursa muhimu kwa wananchi na wachimbaji kujifunza kutoka kwa wataalamu na kuona teknolojia zinazoweza kutumika katika kuongeza ufanisi, usalama na tija katika shughuli zao.
“Nawasihi wananchi wa Geita pamoja na wachimbaji wote kutumia fursa hii adhimu kujifunza,” alisema Luhende.
Alisema matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta ya madini ni muhimu katika kuboresha namna ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini, huku akiwataka wachimbaji kuwa tayari kujifunza na kutumia maarifa mapya katika shughuli zao za kila siku.
Katika ziara yake, Luhende alitembelea mabanda mbalimbali ya washiriki wa maonesho hayo, ambako alijionea teknolojia za uchimbaji, uchenjuaji wa madini pamoja na vifaa na mbinu zinazolenga kuongeza usalama na ufanisi katika maeneo ya kazi.
Aidha, aliwapongeza waandaaji wa maonesho hayo kwa kuendelea kutoa jukwaa linalowaunganisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini na kuwawezesha wananchi kupata elimu na taarifa kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Wito wa Luhende unakuja wakati ambapo maonesho hayo yameendelea kuwa sehemu ya kukutanisha wachimbaji, wataalamu, kampuni zinazotoa huduma za madini na wananchi, kwa lengo la kubadilishana maarifa na kuoneshana teknolojia mbalimbali zinazoweza kutumika katika shughuli za uchimbaji.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Afya na Mazingira Mahala pa Kazi wa Kampuni ya FEMA Mining, Victor Mkono, alisema kampuni hiyo imeshiriki tena katika maonesho hayo ikiwa miongoni mwa wadhamini, huku akieleza kuwa ushiriki wao unalenga kuwafikia wachimbaji na wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu huduma na teknolojia zinazotumika katika shughuli za uchimbaji.
Mkono ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia maonesho hayo kila mwaka, akisema yamekuwa jukwaa muhimu kwa kampuni na wadau wengine wa sekta ya madini kuonesha huduma, teknolojia na fursa mbalimbali.
Alisema kupitia maonesho hayo, kampuni hiyo inapata nafasi ya kuwaelimisha wananchi na wachimbaji kuhusu huduma inazotoa, pamoja na kuwapa fursa ya kujionea teknolojia zinazotumika katika maeneo ya uzalishaji.
“Tunawaomba wananchi watembelee banda letu ili kupata elimu kuhusu masuala ya uchimbaji pamoja na teknolojia tunazotumia katika shughuli za uchimbaji wa madini,” alisema Mkono.
Aliongea kuwa FEMA MININGI & DRILLING ni kampuni ya kizawa kwa asilimia 100, inayojihusisha na huduma mbalimbali za uchimbaji madini, ikiwamo ucholongaji wa miamba, ulipuaji wa miamba na uchimbaji kwa kutumia mashine za kisasa.
Kwa mujibu wa Mkono, ushiriki wa kampuni hiyo katika maonesho hayo unatoa nafasi kwa wananchi na wachimbaji kufahamu zaidi huduma zinazotolewa na namna teknolojia inavyoweza kutumika katika kuboresha shughuli za uchimbaji.
Alisema Maonesho hayo yanaendelea kutoa jukwaa kwa wadau wa sekta ya madini kuonesha teknolojia na ubunifu, huku wananchi na wachimbaji wakipata fursa ya kujifunza mbinu mbalimbali zinazoweza kusaidia kuongeza ufanisi, usalama na tija katika shughuli za madini.
No comments
Post a Comment