Zinazobamba

ZARA KUWAPELEKA WATANZANIA KILELE CHA MLIMA KILIMANJARO MSIMU WA TANO.

Na Mussa Augustine:Dar es Salaam

Kampuni ya Zara Tanzania Adventures imezindua msimu wa tano wa kampeni ya ‘Twenzetu Kileleni’, inayolenga kuwahamasisha Watanzania kushiriki utalii wa ndani kwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio mbalimbali nchini.

Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba 10,2026, katika Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam,ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika,huku kaulimbiu ikiwa ni “Twenzetu Kileleni–msimu wa Tano,Miaka 65 ya Uhuru,Taifa Moja,Kilele Kimoja,Paa la Afrika.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Zara Tanzania Adventures, Zainab Ansell,amesema kwamba  zaidi ya watu 200 wanatarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Marangu,huku vijana wanaounga mkono kampeni hiyo wakifanya idadi ya washiriki kufikia zaidi ya 400.

Aidha Amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha Watanzania kutambua,kuthamini na kutumia fursa za vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani na kuitangaza Tanzania Kimataifa.

Amesema wageni kutoka nje ya Tanzania wamekuwa wakifika kwa wingi kupanda Mlima Kilimanjaro,hivyo ni muhimu kwa Watanzania nao kutumia fursa hiyo kujifunza na kujionea utajiri wa rasilimali za utalii nchini.
Amesema kabla ya kuanza safari hiyo, washiriki watashiriki shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo upandaji miti.
Kwa Watanzania ambao hawataweza kupanda mlima, alisema watapata fursa ya kutembelea vivutio vingine, ikiwemo Serengeti, Ziwa Manyara na Ngorongoro, kwa gharama nafuu.

Ansell amewahimiza Watanzania kutumia mwezi Desemba kutembelea Mlima Kilimanjaro na Serengeti ili kujionea utajiri wa rasilimali za utalii nchini.

Naye Faustin John kutoka Zara Tanzania Adventures,amesema kampuni hiyo imejipanga kutoa huduma bora kwa washiriki, ikiwemo mavazi, malazi, chakula, waongoza watalii wenye uzoefu na elimu kuhusu mazingira.

John amesema njia ya Marangu imechaguliwa kwa kuwa ina huduma za malazi na inafaa kwa msimu wa mvua unaotarajiwa,huku safari ikitarajiwa kuchukua siku sita kufika kileleni.

Hata hivyo amewaomba viongozi wa Serikali,wabunge,mawaziri,taasisi binafsi,mashirika ya dini,mabalozi na Watanzania kwa ujumla kushiriki kampeni hiyo kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani.
Halikadhalika Ofisa Masoko Bodi ya Utalii Tanzania(TTB)Albert Mboto amesema kampeni hiyo inachangia kukuza utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza sekta ya Utalii.

Vilevile Mwakilishi kutoka Chuo Cha Taifa Cha Utalii, Mary Maduhu amesema kampeni hiyo itawapa wanafunzi na watumishi fursa ya kupata uzoefu wa vitendo katika utalii wa Milimani, uhifadhi wa Mazingira na Usimamizi wa Urithi wa Taifa.

Nae mwakilishi kutoka TTCL Peter Mwambuga amesema huduma za mawasiliano zimeboreshwa kuanzia geti la  Marangu hadi kileleni mwa Mlima Kilimanjaro.



No comments